USISIKILIZE DHIHAKA ZA SHETANI, ZITAKUKWAMISHA.

by Admin | 29 November 2019 08:46 pm11

Usisikilize dhihaka za shetani, zitakukwamisha.

Nehemia 4:1 “Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi.

2 Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto?

3 Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, HATA HIKI WANACHOKIJENGA, ANGEPANDA MBWEHA, ANGEUBOMOA UKUTA WAO WA MAWE.”

Ni kawaida ya shetani sikuzote huwa akishaona anakaribia kushindwa anazidisha ujasiri wake kwa kiwango cha hali ya juu sana, kiasi kwamba usipokuwa na moyo mkuu ni rahisi kukiacha kile unachokifanya au unachokiamini mara moja. Huwa anatumia mbinu ya kukishusha thamani kile kitu na ujione kama vile ulikuwa unafanya kazi bure, au umepoteza uelekeo wa Maisha yako mazuri moja kwa moja..

Ndivyo ilivyotokea kwa Daudi pale alipokutana na Goliathi. Utakumbuka Goliathi alimwambia Daudi maneno haya “Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.”.. Unaona lakini Daudi hakuogopa badala yake alirudisha mapigo na kumwambia..

1Samweli 17:45 “Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.

46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.”

Unaona? Ndivyo shetani alivyo sikuzote, Hata alipomwona Nehemia anafanya bidii kuukarabati ukuta wa Yerusalemu ambao ulikuwa umeshaharibika wa Nyumba ya Bwana..japo kweli walikuwa wanaonekana kama vile kazi ile hawataimaliza kwa jinsi walivyokuwa wachache na kwa jinsi walivyozungukwa na maadui…Shetani hakuweza kutulia kwasababau alijua yapo mafanikio makubwa sana katika ujenzi ule kuliko ujenzi wowote unaofanyika duniani kwa wakati ule hadi wakati wa mbeleeni..Hivyo kama kawaida alichokifanya ni kuwavunja tu moyo wakina Nehemia na kuwaambia…

Hicho wanachokifanya hata angepita Mbweha juu ya ukuta huo ungebomoka..Ni dhihaka za shetani kubwa kiasi gani, kumbuka mbweha ni mnyama mwepesi sana, hana hata uzito wa kumfikia mbwa wa kawaida…walau wangesema tembo ingekuwa sio dhihaka za shetani kubwa sana..Licha ya kwamba Nehemia na watu wake walikuwa wanafanya kazi kubwa usiku na mchana kuujenga ukuta. Lakini hapo hapo wanatokea watu na kuwaambia wanachofanya ni kazi bure, hata mbweha akipita juu ya ukuta ule utaanguka.

Lakini Sisi tuonaishi kizazi hiki ndio tunaojua vizuri kama ile kweli ilikuwa ni kazi bure au La!..Kama ulikuwa hujui ukuta ule waliokuwa wanaujenga wakina Nehemia sehemu yake ipo mpaka leo, na hapo ni Zaidi ya miaka 2,500 imeshapita (Tazama picha chini)…Katika wakati wao yalikuwepo majengo mazuri na imara Zaidi ya ule, lakini yalipita, yakaja mengine nayo, yakapita,. Yakaja tena mengine mapya nayo yakapita lakini sehemu ya ukuta ule inadumu mpaka sasa. Ndio ule ukuta uliyo Jerusalemu ambao leo hii maelfu na maelfu ya wayahudi wanakwenda kila mwaka kufanya ibada zao hapo, mbele ya ule ukuta kule Jerusalemu ujulikanao kama ukuta wa maombolezo (wailing wall)..Na ndio ukuta ulio maarufu Zaidi ya kuta zote sasa hivi duniani..

Je! Ukuta huo kweli ulikuwa ni dhaifu?

Ukishaokoka na kumwamini Kristo, shetani hawezi kuvumilia kukuona kuwa siku moja utakuja kuwa msaada mkuu kwa wengine katika mambo ya rohoni. Hivyo leo hii ni lazima atanyanyua tu maudhi na dhihaka fulani fulani ili tu kukukatisha tamaa usisonge mbele, uikane Imani. Ukishaona hivyo, wewe puuzia tu songa mbele..

Unaweza kuchekwa na kuambiwa umepoteza dira ya Maisha. Ukiona hivyo basi ndio ujue upo kwenye njia sahihi, unaweza kuambiwa umelogwa au umerukwa na akili…Ukishaona hivyo usiyatafakari sana hayo maneno yatakuumiza kichwa..ujue tu kuwa ni shetani huyo anatafuta njia ya kukutasha tamaa usisonge mbele kwasababu ameshaona kuna kitu kikubwa kinajiandaa kutokea mbele yako…Puuzia endelea na wokovu wako. Vilevile unaweza ukawa ni mgonjwa na shetani anakuambia huo ugonjwa mwaka huu humalizi utakufa….wewe usimsikilize ni lazima aje kwako kwa ujasiri mkubwa wa namna hiyo, ndio asili yake hiyo, ili tu akufanye uache kuamini…Wewe ziba masikio ikiwezekana mjibu kama vile Daudi alivyomjibu Golithi, “sitakufa bali nitaishi, wewe ndio utayekufa kwenye lile ziwa la moto kuzimu”.

Kwa kufanya hivyo utaweza kuizimisha hiyo mishale yake ya moto. Kumbuka Biblia inasema ufalme wa mbinguni unaanza kama chembe ya haradali…lakini ikishakuwa kuwa kubwa, ndege wa angani wanakuja kutua chini ya uvuli wake (Mathayo 13:31-32)..Lakini ulianza tu kama chembe ndogo sana ya kudharauliwa..Leo hii utaona wokovu wako kama vile hauna faida…Lakini ni jambo la muda tu..Vumilia, kubali kuchekwa, kubali kudharauliwa, kubali mashutumu yote, hayo hayakwepeki…Lakini kuna wakati utafika hiyo mbegu itakuwa mbuyu..

Ikiwa wewe upo ndani ya Kristo, nakutia moyo zidi kumwangalia yeye na songa mbele. Ikiwa bado haujamkabidhi Kristo Maisha yako, kumbuka wakati wa neema ndio huu. Na mlango bado upo wazi lakini hautakuwa wazi kwako siku zote, fanya maamuzi haraka kwasababu biblia inasema saa ya wokovu ni sasa, ukidhamiria kweli kuyasalimisha Maisha yako kwa Bwana, atakupokea na kukutengeneza na kukufanya kuwa mwana wake..

Yohana 3: 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

YUDA ISKARIOTE! MTUME ALIYECHAGULIWA NA BWANA YESU.

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

BUSTANI YA NEEMA.

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/29/usisikilize-dhihaka-za-shetani-zitakukwamisha/