KWANINI BWANA YESU ALISULUBIWA NA WEZI WAWILI?

by Admin | 5 December 2019 08:46 pm12

Naomba kuuliza mtumishi ni Kwanini Yesu alisulubiwa na wezi wawili pale msalabani?


JIBU: Ni kweli Ilikuwa inajitosheleza kabisa Bwana wetu YESU kufa mwenyewe pale msalabani, lakini kulikuwa na sababu nyingine ya ziada Mungu kuruhusu Bwana wetu asulibiwe na wezi wengine wawili pamoja naye…

Awali ya yote tunapaswa tufahamu kuwa Bwana Yesu alikuja duniani kwa lengo la kutafuta kilichopotea, hiyo ndiyo iliyokuwa kazi yake kubwa.

Mathayo 18:11 [Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa kilichopotea.]

Hivyo kama Yesu alikuja kukiokoa kilichopotea, basi tufahamu kuwa alimaanisha kweli kweli kusema vile…, kiasi kwamba hata katika dakika ya mwisho ya uhai wa watu waovu Mungu alimweka katikati yao, atimize kusudi lake hilo la kuokoa.. Na ndio maana utaona aliwekwa katikati ya wale wezi wawili kabla ya kufa kwao..Kwasababu Mungu alitamani na wao pia waokolewe hata kama hawakupata neema ya kumsikia akifundisha katika masinagogi, au hekaluni au mijini au vijijini, bali hata hapo pia ipo fursa ya kuokolewa ikiwa watamwamini..

Hiyo inafunua nini?..

Hata sasa, Kristo hatimizi lengo la kuokoa kwa wale watu ambao pengine wanayo Maisha marefu ya kuishi,… hapana bali pia analitimiza lengo hilo kwa wale ambao anajua wapo katika dhambi nyingi na siku zao za kuishi hapa duniani zinakaribia kuisha, anachofanya huwa anajisogeza karibu sana na wao, kiasi kwamba wakati mwingine anajidhihirisha hata katika mateso wanayopitia ili tu wamwamini yeye waokolewe wasipotee..Kama vile alivyofanya kwa wale wezi wawili, alipitia katika mateso yao yale yale ya kusulibiwa ili tu wamsikilize..

Lakini sasa, cha ajabu ni kuwa katikati ya makundi haya mawili wapo wanaokubali na kugeuka haraka sana..lakini pia wapo ambao badala ya kukubali ndio wanakwenda mbali Zaidi na Mungu, badala ya kutubu ndio wanakufuru Zaidi..

Ndio hapo utasikia mtu anasema, sijui yule kahaba alijuaje juaje siku zake, wiki iliyopita tu, alikwenda kanisani akatubu leo hii tumesikia amepata ajali amekufa,… ukiona hivyo ujue alimtii Kristo katika saa zake za mwisho kama vile yule mwizi wa kwanza..

Mwingine utasikia anasema, alimfukuza mhubiri fulani nyumbani kwake juzi alipokuja kumletea vipeperushi vya injili, na leo hii kwa ghafla tu tumesikia kafa kwa stroke..Mwingine utasikia lisaa limoja lililopita alipokuwa hospitalini anaendelea tu vizuri, mwinjilisti mmoja alikuja akamuhubiria akakubali kutubu, na sasa hivi tunasikia amekufa…n.k. n.k shuhuda kama hizo utazisikia zipo nyingi…utagundua wapo wanaokufuru, wapo wanaotii..

Fursa ya injili;

Na ni mara nyingi wanaobahatika kupata hiyo fursa kusikia injili muda mfupi kabla ya kuondoka kwao ni wale ambao hawajawahi kusikia kabisa injili hapo kabla! Au waliisikia kwa juu juu tu, na hawakupata kujua zaidi ingawa walitamani….Hivyo Mungu anawaletea wokovu mpaka ile siku ya kufa kwao. Ili wasife kabla hawajampokea Yesu.

Lakini kwa wale ambao walishasikia na kupuuzia, inakuwa ni ngumu sana kupata hiyo nafasi,….Wakati Bwana Yesu anasulubiwa pale msalabani kulikuwepo na watu wengine mahali pengine wanakata roho..kulikuwepo na watu wengine mahali pengine labda wanachomwa moto kutokana na wizi wao..lakini hawakupata hiyo fursa ya kusogelewa na Bwana wakati wa kifo chao kama ya hawa wezi wawili waliosulubiwa pamoja na Bwana..

Hata sasa Bwana anafanya hivyo;

Hata mimi na wewe hatujui ni mangapi yapo mbele yetu, pengine tumebakisha wiki, au mwezi, au mwaka, lakini tunaona Kristo anatuhubiria injili kwa nguvu katika hali ya uzima tuliyonayo sasa, katika hali ya kufanikiwa tuliyopo sasa.. pengine kuliko hata alivyowahi kutuhubiria hapo nyuma, Tukiona hivyo tusianze kupuuzia, au kukejeli au kudharau Neno la Mungu, badala yake tukubali kutii na kugeuka haraka sana kama ilivyokuwa kwa yule mwizi wa kwanza,…tukichelewa chelewa, tujue kuwa tunajiweka wenyewe hatarini..Kwasababu katika dunia ya sasa hakuna mtu akifika kule atasema sikusikia injili..Karibi kila mtu kashasikia habari za Yesu…

Kama unaisikia injili sasa ukiwa mzima na unaidharau, mlango wa kutubu wakati wa kufa kwako unakuwa ni mwembamba sana. Ndio maana Biblia inasema saa ya wokovu ni SASA!..Sio kesho wala baadaye..SASA!!

Na Bwana Yesu hafanyi hivyo ili apate sababu ya kutuhukumu hapana badala yake ni ili atupe uzima wa milele na atuepushe na jehanamu..Hivyo kama wewe hujatubu bado na upo nje ya Kristo , muda ndio huu fanya hivyo sasa mpe Kristo Maisha yako, na yeye atakutengeneza na kukufanya kuwa kiumbe kipya..jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Ubarikiwe.

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.

BUSTANI YA NEEMA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/05/kwanini-bwana-yesu-alisulubiwa-na-wezi-wawili/