MKUU WA ANGA.

by Admin | 19 December 2019 08:46 am12

Mkuu wa anga ni nani?


Shalom karibu tuongeze maarifa ya kumjua Mungu wetu..na sio tu kumjua Mungu wetu bali hata kumjua adui yetu…Hata wanyama wa porini wasio na akili huwa wanajifunza kuwatambua marafiki zao na kadhalika maadui zao…Nyumbu atakakula nyasi pamoja na pundamilia na swala, lakini akimwona tu simba kwa mbali basi atakimbia kuyanusuru maisha yake..kwanini? ni kwasababu huko nyuma tayari alishajifunza kumjua adui yake ni nani…na rafiki yake ni nani. Na sisi wakristo tunapaswa tuwe hivyo hivyo…

Leo tutajifunza kwa ufupi juu ya wakuu wa anga…Sasa wapo wakuu wa giza na kadhalika wakuu wa anga..hizo ni roho mbili tofauti. Wakuu wa giza wapo saba…na wakuu wa anga wapo wengi.

Mkuu wa giza aliyepo sasahivi ni wa saba na wa mwisho. Huyu ndiye Pepo mwenye nguvu kuliko wale sita waliotangulia..na kazi zake rasmi zilianza kudhihirishwa mwanzoni mwa karne ya 20 na mpaka leo bado anaendelea kutenda kazi. Kazi yake kubwa huyu ni kuchochea giza Nene duniani..kwa kuwafanya watu wawe vuguvugu, ndiyo jukumu kubwa alilokabidhiwa na shetani.

Shetani anajua tunaishi katika siku za mwisho na muda wake umekaribia kuisha sana..hivyo anachokifanya ni kuwafanya watu wawe vuguvugu sana, na tageti yake sio mtu asiyeamini hapana, tageti yake ni mtu anayeiona kuwa ni mkristo…Anamfanya mtu awe nusu mshirikina nusu mwungwana..Nusu mwombaji nusu mzinzi, nusu mwimbaji wa nyimbo za kumsifu Mungu nusu mshabiki wa mambo na nyimbo za kidunia…Nusu mchungaji nusu mzinzi n.k Hataki kuwafanya watu wawe wazinzi moja kwa moja kwasababu anajua wakiwa baridi kabisa ni rahisi kushtuka usingizini na kutubu…anataka wawe vuguvugu ili iwe rahisi wao kujihesabia haki, na mwisho wa siku watakapokufa wajikute jehanamu badala ya mbinguni…

Ndio maana leo hii..utamwona mtu kavaa kikahaba, na ukijaribu kumwuliza umeokoka atakuambia ndio mimi nimeokoka na jana tu nilikuwa kanisani…huyo huyo ukiiangalia simu yake anaboyfriend ambaye anatembea naye..na ukijaribu kumwambia usipotubu utakwenda hukumuni atakwambia unamhukumu…na atakufunulia maandiko baadhi tu ilimradi ajionyeshe yeye yupo sawa…Sasa hilo ndio lengo kuu la shetani.

Lakini ukimfuata kahaba ambaye hana mpango kabisa na Mungu wala hajui habari za Mungu..ukimwambia tu kidogo habari za dhambi anazozifanya na kwamba asipogeuka atapotea..jambo la kwanza atakiri kuwa yeye ni mwenye dhambi, na hiyo inamfanya iwe rahisi kwake kutubu hata kwa kulia …Sasa shetani ndio kitu ambacho hakitaki hicho…anajua watu baridi kabisa ni rahisi kuigeukia injili…hivyo anafanya juu chini watu wawe vuguvugu. Ili iwe ngumu kumgeukia Mungu wao…

Na faida nyingine shetani anayoipata pindi watu wanapokuwa vuguvugu ni kutapikwa na Mungu…Anajua Mungu hapendezwi na watu vuguvugu..anasema ni heri mtu angekuwa baridi kabisa..yaani angekuwa mwasherati moja kwamoja au kahaba au muabudu sanamu moja kwa moja kuliko kuwa vuguvugu..amesema atamtapika.

Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Hiyo ndiyo kazi ya mkuu wa giza hili..Sasa chini yake wapo wapo wakuu wa anga…hawa kazi yao ni kukusanya taarifa za watu na kushinikiza kueneza uvuguvugu duniani kote..Ni kama Raisi alivyo na wakuu wake wa mikoa…ambao kazi yao ni kuifanya kazi ile ile ya Raisi katika mikoa waliyopo..ni kama wawakilishi wa Raisi huko katika majimbo yao.

Wakuu wa anga wanatumia anga kuleta madhara yao..Kama vile sisi wanadamu tutumiavyo anga kuharakisha maendeleo yetu..kwamba tunatumia anga kusafiri haraka kwa chombo kama ndege..tunatumia anga kurusha wawimbi yetu ya redio na tv pamoja na internet..kiasi kwamba mtu yupo Ulaya unaweza kumwangalia mtu mwingine hapa Tanzania mubashara dakika hiyo hiyo…Kadhalika tunatumia anga kuhifadhi vyombo vyetu kama satellite..ambayo hiyo inatusaidia kutabiri hali ya hewa, mabadiliko ya tabia ya nchi..kufuatilia maeneo tuliyopo..kwa kutumia tu simu yenye program ya satelaiti tunaweza kujiona mahali tulipo..mahali tunapokwenda hata tunaweza kuona mabati ya nyumba zetu…mbali na hayo hata vita vya siku hizi vikuu ni vya angani n.k

Sasa wakuu wa anga nao wanafanya mambo kama hayo kwa kutumia elimu zao za giza…wao hawatumii sayansi..lakini wanatumia elimu yao ambapo wanauwezo wa kujua kiwango cha uvuguvugu uliopo duniani..wanauwezo wa kumjua mtu mmoja mmoja..wana uwezo wa kujua wanadamu wanaomcha Mungu na wasiomcha Mungu..

Sasa mambo yote hayo wanaweza kuyajua kwa kutumia anga..ndio maana wanaitwa wakuu wa anga..Na lengo lao kubwa ni lile lile kuifanya dunia iwe vuguvugu..

Wanafanya vita na wakristo waliookoka na waliosimama kweli kweli…wanatafuta kila njia ya kumwangusha..ili awe vuguvugu!..watamtumia watu ili kumshawishi afanye uasherati…na maroho ambayo yatamwamshawishi na kumwambia mbona Daudi alifanya na akasamehewa?..Na wewe nenda kafanye uasherati utatubu tu!..Na mtu akishaingia huko kufanya dhambi za makusudi kama hizo baada ya kuujua ukweli Mungu anamtapika…Na siku zote hakuna mtu anayeweza kurudia matapishi yake..

Kadhalika mtu ni mlevi..shetani atamwambia usiwe mlevi siku zote hivyo..angalau toa toa sadaka…Na Yule mtu kwa kusikiliza ushawishi huo badala ya kutubu kabisa na kuacha ulevi ndipo akamtolee Mungu wake….yeye atakwenda kujifunza kumtolea Mungu sadaka na hali yake ya ulevi ile ile..akiamini kuwa moyoni Mungu anapendezwa na yeye…Na ukijaribu kumwambie atubu anasema yeye ni mkristo na ni mtoaji…ukiendelea zaidi anakwambia usimhukumu..Mtu wa namna hiyo tayari kashatimiza lengo la mkuu wa giza hili…(Soma Mhubiri 5:1) soma tena Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake”.

Mwambie mtu mizaha na matusi ni dhambi..usengenyaji ni dhambi, rushwa ni dhambi..atakwambia mimi naendaga kanisani na naijua biblia yote na natoa fungu la 10..Hicho ndicho kiburi shetani anachopambana kila siku kukiingiza ndani ya watu.

Bwana atusaidie sana shetani asitupate kwa njia hizo..Je! bado unamtii mkuu wa anga hili kwa kuendelea kuwa vuguvugu?..Au umesimama na kuwa moto?..bado unaendelea kuvaa vimini na huku unahudhuria kanisani?..bado unaendelea kupaka wanja, na kuvaa mawigi na unakwenda kanisani na unajiona upo sawa na Mungu…Yesu anakuambia..unajiona u utajiri lakini ni maskini, na mnyonge na mwenye mashaka…Lakini ametoa shauri kwamba utubu nawe utakuwa tajiri.

Waefeso 2:1 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;

2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;

3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine”.

Na kumbuka Mkuu wa anga hili na mkuu wa giza hili hatuwashindi kwa kuingia kwenye maombi ya mfungo..wala kwa kurusha mishale ya moto angani…Tunamshinda tu kwa kuamua kubadilika na kumgeukia Kristo kikamilifu..kwa kuzikataa kazi za shetani zote…kama ulikuwa ni mwasherati unaamua kugeuka, ulikuwa mlevi unageuka na kuacha ulevi kwa imani…Na baada ya kugeuka, unatubu na kwenda kubatizwa..kisha Roho Mtakatifu ndani yako atakuongoza na kukutia katika kweli yote ya kimaandiko.

Na silaha nyingine ya kumshinda wakuu hao ni kulifahamu Neno, ambalo hiyo inatokana na kujifunza kusoma biblia mwenyewe na kujifunza sehemu nyingine tofauti tofauti..Ndani ya Biblia utajifunza kuhesabiwa haki kwa Imani..utajifunza kuukulia wokovu na kusimama thabiti..pamoja na kujua nguvu iliyopo katika jina la Yesu na damu ya Yesu.

Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;”

Bwana akubariki sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MKUU WA GIZA.

JE VIBWENGO NI KWELI VIPO?

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

ASKOFU MKUU NA MCHUNGAJI MKUU NI NANI?

MTINI, WENYE MAJANI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/19/mkuu-wa-anga/