HAPANA HATA MMOJA ATAKAYEIONJA KARAMU YANGU.

by Admin | 26 December 2019 08:46 pm12

“Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”


Tukisoma Luka 14 kuanzia mstari wa 16-24. Tunaona Bwana Yesu akitoa mfano wa mtu mmoja aliyefanya karamu kubwa sana. Na siku ilipofika ya sherehe muda wa chakula akatuma mtumwa wake kwenda kuwaita wale waliolikwa waje karamuni lakini mwitikio wao siku hiyo ulikuwa ni tofauti, badala ya kuja kila mmoja akaanza kutoa udhuru mmoja akasema mimi nimenunua shamba ni sharti niende kulitazama nisije nikawa nimeuziwa bonde, hivyo nisamehe, mwingine akasema nimenunua ng’ombe hivyo ni sharti niende kiwajaribu nisije nikawa nimeuziwa vilema na wagonjwa, mwingine akasema nimeoa nitakwenda honey-moon siwezi kuja nisamehe..

Lakini yule mtu alikasirika sana..Ukisoma pale kwa makini utagundua kuwa hakukasirika kwa waliokuwa wamepanga kuyafanya, hapana lakini alikasirika kwa wao kupuuzia mwaliko wake. Kwasababu udhuru zao hawakuzitoa mwanzoni kabisa walipoalikwa kabla hata sherehe kuanza, Bali walisubiria wazitoe siku ambayo kila kitu kipo tayari,.. mahali ambapo mwenye kualika hawezi kuahirisha na kufanya wakati mwingine ambapo wote watakuwa free. Hiyo ni kuonyesha kuwa walikuwa hawataki kabisa kuhudhuria sherehe ya yule aliyewaalika tangu mwanzo, na ndio maana wakazihifadhi sababu zao wasizitoe tangu siku nyingi na kuzitoa siku ile ya sherehe yenyewe, walijifanya kama wamepatwa na emergency hivi kumbe mambo hayo walikuwa wanayatambua tangu mwanzo..

Lakini sasa tunaona mwisho wa mfano ule, Bwana YESU anasema maneno haya:

Luka 14:24 “Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.

Hapa ndipo kiini cha somo kilipo..

Kwanini aseme tena hivyo “wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.”

Kulikuwa kuna maana gani ya kusema hivyo wakati tayari walishaikataa tangu mwanzo?..Embu jaribu kufikiria mtu amekualika unakataa halafu anakuapia hutaonja sherehe yake…Si unaweza kumwona kama ni Mwenda wazimu?. Lakini ukiwa na akili utajiuliza maswali Fulani kichwani kwako kwanini aniambie vile??

Kipindi Fulani nyuma, kuna Rafiki yangu ambaye alipomaliza masomo yake alikwenda katika mafunzo ya jeshi kwa matumaini kuwa akimaliza aajiriwe kule, lakini kwa bahati mbaya walikaa kule muda mrefu, sana, wakisubiria ajira kwa muda mrefu lakini hazikutoka..Mpaka wakati wa mafunzo ulipoisha sasa wanalazimika kila mmoja arudi nyumbani kwao, ni kama vile alikata tamaa akiangalia ameshapoteza miaka kadhaa kule jeshini na leo hii anaambiwa arudi nyumbani!!..

Lakini wakiwa huko nyumbani, tamko linatolewa na raisi kuwa kuna mgodi mahali Fulani unahitaji ujenzi wa kuzungushwa ukuta mgodi wote, na wanaohitajika kwa shughuli hiyo ni walewale vijana waliokuwa katika mafunzo ya jeshi, lakini kwa sharti kuwa hakuna malipo, wala posho bali ni kitendo tu cha kujitolea..hivyo anayetaka kwenda na aende, na asiyetaka vilevile ni sawa.

Wengi wao waliposikia hivyo hawakutaka hata kufuatilia habari hizo, wengine walidhihaki, wakagoma, wakaona kama ni mambo yaleyale, kwenda kupoteza muda halafu mwisho wa siku hautazamwi unarudishwa nyumbani kukaa.Lakini huyu Rafiki yangu na wenzake wachache sana, wakaamua tu kwenda kujitolea kufanya kazi hiyo, wakitumaini pengine labda wataangaliwa wakishamaliza ujenzi huo, lakini walifanya kazi ile kwa shida ananiadithia, kwasababu ilikuwa ni ngumu na walipewa kipindi kifupi sana cha kuimaliza..

Wakafanikiwa kuimaliza, kisha wakapewa kila mmoja cheti, wakitumaini wataitwa walau jeshini, lakini wakaambiwa asanteni kwa msaada wenu rudini nyumbani..Basi wakarudi nyumbani, muda ukapita wale wengine wakaanza kuwacheka, na kuwakejeli, lakini sasa baada ya ujenzi ule kukamilika na serikali kuona imefanikiwa kukusanya mapato mengi kwa kipindi kifupi kwasababu ya ujenzi wa ukuta ule,.kukomweshwa kwa vya utoroshaji madini. Ndipo raisi akakumbuka Je! Wale watu waliojengwa ule ukuta wamefanyiwa fadhila gani?..Akatoa tamko la siku 2 wale vijana wote waliojenga ukuta ule wafike makao makuu ya polisi wakiwa na vyeti vyao mkononi wapokee ajira zao za kujiunga na Jeshi.

Sasa wale wengine ambao walikataa kujitolea waliposikia hivyo, matumbo yalijaa moto, wakaanza kuhangaika huku na huko wengine wanatafuta namna ya kufoji vyeti vile, wengine wakatafuta namna ya kutoa rushwa, wengine siku ile ile na wao pia walifunga safari wakiungana na wale wenzao kwa ajili ya udahili, wakitumainia kuwa na wao pia watapata rehema ya kuruhusiwa kujiunga na wenzao..Lakini pamoja na kwamba safari zao kuwa ndefu, kutoka kila mkoa nchini.. waliishia kufukuzwa tu getini pale..wengine wakaanza kulia na kulaumu, wakiona wale ambao walikuwa wanawacheka sasa sio wenzao tena..Wenzano wanapata ajira wao wanarudi nyumbani..Wengine wakawa wanajuta ni kwanini walikataa mwaliko ule wa kuujenga ukuta wa mgodi..waliokuwa wanawaambia nyimbo za mizaha leo hii wao ndio wanalia..

Na ndivyo itakavyokuwa katika karamu ya mwana-kondoo. Leo hii wengi wanaalikwa mamilioni kwa mamilioni takribani karibu kila mtu duniani anaalikwa ili tu kuingia katika karamu ile ya mwana-kondoo, lakini wanaouitikia mwaliko huo ni wachache sana, tena sana, pengine hao ambao hawaitikii wana sababu zao za msingi sana za kusimamia..wengine wanasema wokovu hauna faida, wengine wanasema unanifanya niwe maskini, wengine wanasema, nilichonacho sasa kinanipa faida kuliko hicho ninachokitazamia kuja huko mbeleni..Wengine wanasema siwezi kuacha biashara yangu hii haramu, ni sharti nitafute fedha kwanza kisha Mungu uzeeni, nikishastaafu…Wengine wanasema nimeujaribu wokovu huo kwa muda mrefu na sijaona faida yake hivyo sitaki kuusikia…Wote hawa wanaosababu zao, na pengine ni sababu za msingi sana..

Lakini nataka nikuambie, leo hii hutaki, lakini siku moja kibao kitakugeukia wewe.. utatamani hicho ulichokikataa lakini utakuwa tayari umeshachelewa?. Ni kwasababu gani utamani kukipata tena hicho ulichokikataa? Ni kwasababu utaona mambo yaliyo kinyume na matarajio yako.

Wale waliopewa mwaliko na kuanza kutoa udhuru wa kununua ng’ombe wengine shamba wengine wameoa..waliidharau ile karamu na Zaidi ya yote walijua hata wakienda kwenye ile karamu watagharimika gharama nyingine za kutoa zawadi..Lakini kinyume chake pengine yule Bwana arusi aliwaalika kwenye karamu yake aliwaalika kwenda kuwapa zawadi waalikwa wake na si kupokea zawadi..Utajisikiaje unaikataa harusi ambayo ulidhani unakwenda kutoa zawadi kumbe ndio unakwenda kupewa zawadi?..Unaona wenzako waliokwenda wanapewa majumba, mashamba, magari, mang’ombe n.k … utatatami kwenda kujiunga lakini utashindwa..?

Ndivyo itakavyokuwa siku watakatifu watakapokwenda mbinguni…Wewe uliyeudharau mwaliko leo..Utaona kwa mbali uzuri ambao Mungu amewaandalia watu wake, milele, utaona hiyo miili mipya waliyoandaliwa wateule wa Mungu milele jinsi ilivyo mizuri yenye utukufu mwingi, na wewe huna, utaona hiyo miji mizuri na majumba mazuri walioandaliwa watakatifu na wewe utakuwa huna chochote, utaona mambo ambayo hata wale walioitikia mwaliko, hawajawahi kuyaona, wala kuyasikia, wala kuyategemea..Siku hiyo utajuta utasema ni kwanini sikuitikia mwito ule wa karamu ya mwanakondoo..

Utafanya bidii kweli uingie lakini hutaweza..Ndio hili Neno litakapotimia juu yako..

Luka 14:24 “Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu: yangu”.

Ndugu Parapanda ipo karibuni kulia, UNYAKUO ni tendo tunalolitazamia sasahivi mbele yetu,..Ukiendelea kuutazama huu ulimwengu ambao haukuahidii kitu chochote baada ya kufa, utapata hasara ya nafsi yako mwenyewe. Ushauri wangu ni kuwa Chukua hatua tubu dhambi zako mgeukie Kristo, maadamu wakati wa kuitikia wito mwaliko unao, kabla siku za hatari hazijakukuta..

Ufunuo 19:9 “Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu”.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

NGUVU ILIYOPO KATIKA MAAMUZI.

WAZAZI WA YOHANA NA YAKOBO.

HALI ZETU JINSI ZINAVYOWEZA KUATHIRI UTOAJI WETU.

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

USIWE NA HAKI KUPITA KIASI.

Rudi Nyumbani:

 

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/26/hapana-hata-mmoja-atakayeionja-karamu-yangu/