NAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA!

by Admin | 1 January 2020 08:46 pm01

Shalom. Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe…

Ni kwa Neema za Bwana tumeuona tena mwaka huu mpya wa 2020. Si wote waliovuka lakini sisi tumevuka..Utukufu na heshima na shukrani zina yeye. Amina.

Nakutakia mafanikio katika huu mwaka ulioanza. Mafanikio ya roho yako..ambayo hayo yatazaa mafanikio mengine yote yaliyosalia..kama maandiko yanavyosema katika..

3Yohana 1:2 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo”.

Katika Mwanzo wa mwaka wana wa Israeli waliachiliwa kutoka katika nyumba ya utumwa, wakawa huru, Hivyo Bwana akuachilie nawe pia kutoka katika nyumba ya utumwa wa Ibilisi katika jina la Yesu Kristo. Kila aina ya mikakati na vifungo vya Ibilisi Bwana akaviweke mbali nawe katika mwaka huu wa 2020. Ulioanza. Kila kilichokuwa kigumu Bwana akakifanye kuwa kilaini.

Pale ulipokuwa huwezi kusonga mbele katika Imani kutokana na majaribu mazito ya Adui..Bwana akayazuie katika mwaka huu katika jina la Yesu Kristo.

Mwaka huu ukawe mwaka wa Bwana, na kila ufanyalo kwa ajili ya Bwana, na kwa ajili yako binafsi likafanikiwe na kustawi.

Nakumbuka mwaka Fulani nyuma..tulikuwa tunafanya kila siku jioni ibada ndogo nyumbani..Tulikusudia kupitia vitabu vyote vya biblia sura baada ya sura, kila siku sura moja..Sasa miezi michache kama miwili na nusu hivi nyuma kabla ya mwaka huo kuisha tulianza kujifunza kitabu cha Zaburi..ikawa kila siku tunasoma mlango mmoja…hivyo hivyo, kama kawaida kesho tunafuata mwingine..maana yake baada ya siku 30 tulikuwa tumeshasoma Sura 30 za kitabu hicho…

Hatukuacha hata siku moja..Wakati tunaendelea kila siku kukichambua kitabu hicho, hapo ni baada ya kumaliza baadhi ya vitabu vingine vya nyuma, sasa ilipofika tarehe 31 Disemba usiku tulikuwa tumefika sura ya 65 ya kitabu hicho cha Zaburi..Siku hiyo hatukusoma tukatenga siku hiyo iwe maalumu kwa kumsifu Mungu na kumshukuru na kumwimbia..Hivyo tukasema tutaisoma hiyo sura ya 65 kesho yake yaani tarehe 1.. Tulimwimbia Mungu na kumsifu kwa namna isiyo ya kawaida, Ilipofika terehe moja jioni, tukakusanyika tena tuendelee na kitabu chetu hicho ambacho siku hiyo tulikuwa tumefika mlango wa 65. Je! Unajua katika mlango huo ndani yake tulikutana na nini?

Tusome..

Zaburi 65:9 “Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.

10 Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.

11 UMEUVIKA MWAKA TAJI YA WEMA WAKO; Mapito yako yadondoza unono”

Mstari huo wa 11 unaosema “Umeuvika mwaka taji ya wema wako”.. ndio ukawa neno la Mwaka wetu..

Ilitufariji sana…hatukujua kuwa sura hiyo ya 65, inazungumzia habari ya mwaka mpya…hivyo ukawa ndio uthibitisho Mungu kazungumza na sisi, na kutupa Neno la Mwaka….Tukafahamu kumbe, ibada zetu zote zilikuwa zinahesabiwa!..Kumbe kila sura ilikuwa inahesabiwa..na hivyo Mungu ameilengesha ile siku ya tarehe moja katika mlango ule.

Na mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa wema kweli wa Mungu kwa wote tuliokuwepo pale..Bwana alitufanyia wema mwingi sana sana kupita kiasi..kulitimiza Neno lake hilo alilotuambia.

Hivyo leo hii neno hili pia liwe lako. Bwana akauvike mwaka wako “taji ya wema wake”. Ukaone maajabu ambayo hujawahi kuyaona katika Maisha yako. Bwana akaufanye mwaka wako huu uwe mwaka wa Pentekoste, mwaka wa kumzalia matunda, mwaka ya kuishi maisha yampendezayo mwaka wa furaha na mafanikio. Akakubariki kila unapoingia na kila unapotoka.

Lakini Pamoja na Baraka hizo zote, pia nakukumbusha mwaka huu walee wanao katika njia iliyobora Zaidi ya kumcha Mungu kuliko mwaka jana. Usimnyime mwanao mapigo pale panapostahili kwasababu biblia inasema hatakufa!. Na pia mwaka huu fanya bidii kupiga hatua moja mbele, usiwe mvivu wa kufunga, pale ikupasapo kufunga na kuomba.. Usikubali kiwango kile kile cha rohoni ulichokuwa nacho mwaka jana, uwe nacho tena mwaka huu..Zidisha kiwango chako cha usafi na utakatifu..Anza mwaka wako na Bwana, Mwaka huu hesabu matunda utakayomletea Bwana yawe ni mara 10 zaidi ya mwaka jana..Yaani kwa ufupi kila kitu ulichokizembea mwaka jana usikiruhusu kivuke mwaka huu..

Na kwa kufanya hivyo Mungu kama alivyosema katika Neno lake, atakujilia na kukustawisha na kukutajirisha sana, na kisha ATAUVIKA MWAKA WAKO TAJI YA WEMA WAKE.(Zaburi 65)..Ndivyo itakavyokuwa kwako kwa jina la YESU KRISTO.

Amen.

Heri ya mwaka mpya 2020.

Mada Nyinginezo:

NI NINI KINAKUPATA UNAPOIPUUZIA INJILI?

TUMTOLEE MUNGU VILE VINAVYOTUGHARIMU ZAIDI.

OKOA BADALA YA KUANGAMIZA!

SAA YA KIAMA.

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/01/nakutakia-heri-ya-mwaka-mpya/