MTU ASIYE PAMOJA NAMI YU KINYUME CHANGU.

by Admin | 9 January 2020 08:46 am01

Jina kuu la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe…Karibu tena tujifunze maandiko…kwa kuwa jukumu kuu tulilonalo kila siku ni kumjua sana Yesu Kristo mwana wa Mungu na kuhakiki kila siku ni nini kimpendezacho sawasawa na Waefeso 4:13 na 5:10.

Leo tutayatafakari maneno ya Bwana Yesu Kristo aliyoyasema katika kitabu cha Mathayo.

Mathayo 12:30 “Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya”.

Ukianzia mstari wa juu kidogo utaona kuna tukio Fulani lilifanyika ambapo likamsababisha aseme hayo maneno..Lakini tukiyatafakari maneno hayo kwa undani tunaweza tabia mojawapo ya Mungu na hivyo kuchukua tahadhari kwa kila tunachokifanya..

Sasa mstari huo Bwana Yesu anasema… “Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu”…na… “Mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya”..Hizo ni sentensi mbili zinazozungumzia kitu kimoja.

Nimewahi kukutana na mtu anasema mimi simwamini Bwana Yesu lakini natenda haki, nasaidia maskini, sinywi pombe, siibi, situkani n.k..Je Mungu atanihukumu kwa sababu tu simwamini Yesu Kristo?..Mwingine atakuambia mimi simwamini Yesu lakini nampenda na namuheshimu na simpingi…..Nataka nikuambie ndugu yangu..kitendo tu cha wewe kutokuwa upande wa Yesu Kristo hata kama unatenda mema kiasi gani..mbele zake tayari upo kinyume chake..haijalishi unafanya mema mengi kiasi gani..kitendo tu cha wewe kujiepusha na yeye tayari upo kinyume chake..roho ya mpinga-kristo ipo ndani yako. Tayari unahesabika kama mtu unayempinga Kristo ..kwasababu anasema.. “Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu”

Kadhalika kama huifanyi kazi ya Mungu na umepewa hiyo neema…na unasema “aa mimi sifanyi kazi ya Mungu lakini siipingi kazi ya Mungu”…Nataka nikuambie kitendo tu cha wewe kutoifanya kazi ya Mungu na huku umepewa hiyo Neema…mbele zake unaonekana unaitapanya kazi yake…kwasababu anasema “Mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya”..Na wewe hukusanyi pamoja na Mungu, hivyo ni wazi kuwa unakusanya sehemu nyingine ambayo inakinzana na Mungu..Kitendo cha wewe kukataa kuifanya kazi ya Mungu na kuendelea kufanya mambo yako mengine, tayari unaiharibu kazi ya Mungu…Kwahiyo kuna madhara makubwa ya kukaa kutokuifanya kazi ya Mungu..kwasababu mbele zake tunaonekana kama tunaitapanya.

Ndio maana kuna mfano mmoja Bwana aliutoa na kusema..

Luka 13:6 “Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.

7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, MBONA HATA NCHI UNAIHARIBU?

8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;

9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”.

Nataka uuone huo mstari unaosema ..“Mbona hata nchi unaiharibu”..Maana yake ule mti ambao hauzai matunda kitendo tu cha kuendelea kuwepo pale tayari unaiharibu nchi/ardhi. Unaweza kusema si ubaki tu kwani usipozaa unaathari gani? …Biblia inasema “kwa kuendelea kuwepo pale unaiharibu nchi”.

Vivyo hivyo kuwepo kwako kama hufanyi kazi ya Mungu basi fahamu kuwa Unaiharibu kazi ya Mungu bila kujua…Kuwepo kwako kama hufanyi mapenzi ya Mungu basi unaiharibu kazi ya Mungu…kadhalika unaishi maisha ya kuvaa nusu uchi,kuvaa suruali na nguo zinazobana na fupi, na kupaka lipstick, wanja, kuvaa mawigi na hereni ni kweli una moyo mzuri unasaidia watu, una huruma na wakati mwingine unakwenda kanisani, na wala hutukani, wala huibi, …ni kweli unafanya mambo mazuri mengi lakini kwa mavazi yako unaiharibu kazi ya Mungu..kwasababu wakati Roho wa Mungu anafanya kazi kwa nguvu kuwahubiria watu waepukane na mavazi hayo ya kikahaba na mambo ya kidunia..wewe unafanya kazi ya kuwahubiria waendelee kuvaa kwa jinsi wanavyokuona wewe unavyoyavaa,…

Wakati Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa nguvu kuwaonya watu waache kupaka hivyo vitu usoni na kichwani na wajiepushe na hukumu inayokuja…wewe unawahubiria mambo hayo ni sahihi kufanya kwa jinsi unavyoendelea kuyafanya….Hivyo unakwenda kinyume na kazi ya Mungu (unaiharibu kazi ya Mungu…) “Unakuwa hukusanyi pamoja na Kristo bali unatapanya”.. na hivyo unahesabika kwamba upo kinyume na Kristo (yaani mpinga-kristo)…haijalishi unafanya mema mengi kiasi gani.

Bwana akubariki.

Kama hujaokoka, mlango wa Neema upo wazi fanya hivyo leo..Tunaishi katika siku za mwisho, na Siku yoyote parapanda inalia, na watakatifu watanyakuliwa kwenda mbinguni..Na biblia inasema “ufalme wa Mungu unapatikana kwa nguvu”..Nao wenye nguvu ndio watakaouteka…Hivyo si wakati wa kujivuta vuta tena, Si wakati wa kuhubiriwa injili ya kubembelezwa..ni wakati wa kujitwika msalaba wako na kumfuata Kristo pasipo kuangalia nyuma au kuangalia ndugu au Rafiki anasemaje.

Hivyo unachopaswa kufanya sasa ni kutubu kwa kumaanisha kabisa…maana yake unaacha maisha yote ya dhambi uliyokuwa unaishi ambayo yalikuwa yanaifanya kazi ya Mungu iharibike..Unaacha ulevi, usengenyaji, wizi, rushwa, utukanaji, unaacha kujichua, unaacha visasi, wivu, uvaaji mbaya, unakwenda kuchoma vimini vyote na suruali na vipodozi vyote ulivyokuwa unatumia na mambo mengine yote yasiyofaa.

Na baada ya kufanya tendo hilo la Imani, utakuwa umemtii Kristo, na hivyo Neema ya kipekee itaachiliwa juu yako ambayo hiyo itakusaidia kushinda dhambi bila kutumia nguvu nyingi..utajikuta tu ile hamu na nia ya kufanya dhambi inakufa yenyewe…lakini sharti kwanza uamua kuacha wewe mwenyewe kwa vitendo ili Bwana aione Imani yako.

Na mwisho, tafuta kanisa la kiroho ambalo linamhubiri Yesu Kristo wa kwenye biblia jiunge hapo na pia ulizia ubatizo, ili ukabatizwe kama hujabatizwa,..kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji mengi..na kwa Jina la Yesu Kristo sawasawa na (Matendo 2:38)..zingatia hilo sana..Na Bwana atakuongoza kufanya mengine yaliyosalia ikiwemo kukuuongoza na kukutia katika kweli yote ya maandiko.

Bwana akubariki sana.

Mada Nyinginezo:

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Ulinzi wa daima (eternal security) Je! ni neno la kimaandiko?

Je! mtu aliyeokoka anaruhusiwa kumiliki Lodge ambayo ina Bar ndani yake?

Je kuzalishwa na mkunga wa kiume ni dhambi?

HAJANENA KAMWE MTU YE YOTE KAMA HUYU ANAVYONENA.

UFUNUO: Mlango wa 1

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/09/mtu-asiye-pamoja-nami-yu-kinyume-changu/