HAJANENA KAMWE MTU YE YOTE KAMA HUYU ANAVYONENA.

HAJANENA KAMWE MTU YE YOTE KAMA HUYU ANAVYONENA.

Yohana 7:45 ‘’Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta?

46 Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.

47 Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika?

48 Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?

Amen. Leo hii tujiulize ni kwanini mtu aliye maarufu kuliko wote duniani kwa wakati wote na vizazi vyote ni YESU KRISTO?.

Ukiona hivyo ujue si bure kuna kitu alichokuwa nacho ambacho hakuna mtu mwingine duniani anacho,. Leo hii kitabu kinachosomwa kuliko vitabu vyote duniani ni biblia, kinachofuata chini yake hakikaribii hata chembe, na katika hiyo hiyo biblia ni miongoni mwa vitabu vinavyosomwa zaidi ni vitabu vya injili vinavyozungumzia maisha ya YESU, na maneno ya Yesu Kristo kwa ujumla. Ukiona hivyo ujue si bure bure tu, lipo jambo watu wameona ndani yake.

Wale watu waliotaka kwenda kumkamata Yesu na kumfunga, wakidhani yule alikuwa ni mtu wa kawaida tu labda pengine ni mwana mapinduzi ametokea anataka kuipundua nchi, au mwanasiasa Fulani kama wengine, au mwanaharakati huru, au jasusi, lakini walipokutana na maneno yaliyotoka kwenye kinywa chake..Matarajio yao yaligeuzwa, Nia zao zilibadilishwa, fahamu zao zikafunguliwa..Na wakakiri kwa vinywa vyao.

Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena…, Kauli hiyo inathitisha kuwa walizunguka sehemu nyingi kushughulika na watu wa namna yake, wamekutana na wengi, wamewasikia wengi, na kufanikiwa kuwakamata, lakini walipofika kwa huyu, na kusikia maneno yale.. walikiri kwa vinywa vyao, hawajawahi kuona mtu aliyenena kama yeye..Maneno yaliyojaa neema, na uweza, na nguvu, na matumaini, na faraja, na elimu, na maarifa, na uzima, na roho.

Sasa ni miaka 2000 imepita, lakini kila kizazi, kinashuhudia hajatokea mtu yeyote mfano wa Yesu Kristo mwenye maneno ya kipekee kama yeye. Walikuwepo wengi wameondoka…Lakini kwa Kristo maneno yake yaliposikiwa yalipenya mpaka kwenye vilindi vya mioyo ya watu.

Embu fikiria mtu anayekuambia maneno haya;

Mathayo 11:28 “ Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi..”

Anakuambia tena.

Yohana 4:13 ‘’Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;

14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

Maneno hayo ni matamu sana…”

Sikia na haya..

Yohana 11:25 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

26 naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?”

N.k N.k. Yapo mengi..Hakuna kiongozi yeyote wa dini alishawahi kuahidi maneno kama haya na akayatelekeza, hata sasa hakuna..Na ndivyo inavyojulikana kwa watu wote, na dini zote, hakuna kama YESU KRISTO, Na kamwe hatakuwepo mtu anayenena maneno yaliyojaa neema kama yeye.

Maneno yake yamewabadilisha maelfu kwa maelfu, mamilioni kwa mamilioni, yamehakikishwa, yamethibitishwa ni kweli..Hakuwa mwanasiasa yule, kuahidi mambo ambayo hawezi kuyatimiza, Hata wewe leo hii ukiamua kumwamini na kumfuata kweli kweli, zile chemchemi za maji ya uzima alizozisema miaka 2000 iliyopita zitaanza kutiririka ndani yako leo..

Kama umelemewa na mizigo ya dhambi, na masumbufu ya maisha haya mpaka umekata tamaa ya kuishi, ukimfuata, atakupumzisha kweli kweli, kama alivyoahidi,..Utapata tumaini jipya, na mwanzo mpya wa maisha, hakuna aliyekwenda kwake akajuta..utafutaji wa mali hautakupa faraja!..Umezitafuta miaka yote je zimekufariji?..zaidi sana zinakutia presha kuliko kukufariji..

Na ndio maana maandiko yanasema..

Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini”.

Onja na wewe, Yesu anayehubiriwa ulimwenguni kote, anaokoa kweli maisha ya watu, usimwache akupite.

Ikiwa bado unatanga tanga na ulimwengu..unasubiri nini? .Ikiwa bado unatazamia mtu mwingine atakayekutamkia maneno mazuri na ya faraja Zaidi ya Kristo, nataka nikuambie hautampata na hatakuwepo,. Tubu dhambi zako leo anza mwanzo mpya na Kristo. Hapo ulipo Bwana anaweza kukuokoa ikiwa utamaaanisha kweli kutubu. Unachopaswa kufanya ni kupiga magoti na kumweleza Kristo kuwa unahitaji msamaha wake na msaada wake. Na kwamba umemaanisha kuwa kuanzia leo na kuendelea utakuwa mwanafunzi wake, na utamfuata kwa gharama zote..Sasa Ukishatubu kuwa kumaanisha kabisa, ujue kuwa Kristo ameshakusamehe, kwasababu yupo hapo pembeni mwako kukusikia..

Unachopaswa kufanya, hatua inayofuata ni kuonyesha toba yako kwa vitendo, na tendo la kwanza ni kuacha yale mambo maovu uliyokuwa unayafanya nyuma, kukaa mbali nayo,..yote pamoja na vichochezi vyake.. pili unatafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, kama hujabatizwa hivyo… na tatu ni kutafuta ushirika wakristo wa kweli walio karibu nawe na kujumuika nao..ili uweze kujifunza Neno la Mungu, kumega mkate na kusali kwa pamoja.

Na Kwa kufanya hivyo utakuwa umemdhihirishia Mungu toba yako kuwa ni kweli kwa Matendo yake..Na yeye akishaona hivyo atakuhakikishia ulinzi wa daima ikiwa hutatia nia ya kugeuka nyuma..atahakikisha anakupa uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu. Hiyo ikiwa na maana kuwa atakuvika uwezo wa kufanana na Yesu Kristo, kwa neema zake. Na kuanzia hapo utaweza kuishinda dhambi kirahisi kwasababu Roho wa Mungu atakuwa ameshaachiliwa juu yako.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MTETEZI WAKO NI NANI?

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

UFUNUO: Mlango wa 1

SAUTI NI SAUTI YA YAKOBO, LAKINI MIKONO NI YA ESAU.

Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments