JE! WEWE NI MWAKILISHI MWEMA?

by Admin | 21 January 2020 08:46 pm01

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe…

Tunasoma Bwana wetu Yesu Kristo alipoanza huduma yake alianza peke yake…lakini akiwa katikati ya huduma hiyo, kama wengi wetu tunavyojua aliwatafuta wanafunzi ambao hao baada ya yeye kuondoka wataiendeleza kazi aliyokuwa anaifanya yeye. Aliona kuwa mavuno ni mengi na yeye peke yake hatoshi inahitajika jeshi kubwa. Hivyo aliwatafuta wanafunzi wengi sana…idadi yao haijulikani lakini ni wengi…Miongoni mwa hao wanafunzi wengi aliokuwa nao akawatenga mitume 12..Kwaajili ya madarasa maalumu…Kuna mambo ambayo mitume 12 walikuwa wanaambiwa na Bwana ambayo wanafunzi wengine walikuwa hawaambiwi..

Lakini ilifika kipindi Mitume wakapelekwa mazoezini kama vile wanafunzi wa vyuoni wanavyopelekwa field leo..Bwana aliwatuma wazunguke kila mahali, watoe pepo wafufue wafu n.k…lakini na hiyo Bwana aliona haitoshi pia akawaagiza tena wanafunzi wengine 70 waende wakafanye kazi zile zile za Mitume 12..

Luka 10:1 “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na KILA MAHALI ALIPOKUSUDIA KWENDA MWENYEWE.

2 Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.

Sasa nataka tuone huo mstari unaosema “wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe”.

Kuna mahali ambapo Kristo anakusudia kwenda mwenyewe lakini anatutuma sisi tuende kwa niaba yake….Kumbuka hatuendi mahali sisi tunapotaka kwenda bali yeye alipokuwa anataka kwenda mwenyewe…Ikiwa na maana kuwa tunakwenda kutimiza kusudi, na malengo ya mtu mwingine…Na sio malengo yetu. Sisi ni mawakili tu..Ni sawa Raisi amtume mtu fulani amwakilishe kwenye sherehe fulani aliyoalikwa kwenye Taifa lingine…Yule aliyetumwa ni mwakilishi tu…anapeleka pongezi, au shukrani au maombi kwa niaba ya yule aliyemtuma…hana la kuongeza wala la kupunguza kutoka kwenye nafsi yake mwenyewe.

Kadhalika tunapokuwa wakristo sisi ni wa wakilishi wa Yesu Kristo mahali tunapotumwa…Hatuna hati miliki ya injili, hivyo tunapaswa tuseme kile anachotaka sisi tukiseme..tunapaswa tufikie malengo yale anayotaka yeye afikie…Kwa ufupi tufanye kazi ile ile ambayo angekuwa yeye yupo hapo angeifanya.

Lakini tunapokuwa wakristo halafu hatuifanyi kama anavyotaka yeye…maana yake sisi ni waasi. Mtu asiyekuwakilisha vyema kama ulivyomwambia akuwakilishe maana yake huyo mtu tayari kashakuwa adui yako. Unakwenda na kuwahubiria watu injili ambayo Yesu Kristo hakuihubiri ni kujitafutia laana badala ya baraka..Biblia inasema hivyo katika..

Wagalatia 1:6 “Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.

7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.

8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe”.

Bwana Yesu alihubiri toba na ubatizo lakini wewe unasema hayo sio ya msingi..hapo unajitafutia laana…Bwana Yesu alihubiri kwamba tusishindane na mtu mwovu, tuwaombee wale wanaotuudhi, na tuwapende adui zetu..wewe unahubiri mlaani adui yako na mchukie anayekuchukia..Bwana Yesu alifundisha kwamba tusilale usingizi bali tukeshe katika roho nasi tuwe kama watu wanaomngojea yeye..Wewe unahubiria watu na kuwawekea mazingira ya kuzidi kuzama katika ulimwengu,..Bwana Yesu alihubiri mtu amwachaye mkewe na kwenda kuoa mwingine azini..wewe unafungisha ndoa za watu waliowaacha waume wao au wake zao, Bwana Yesu alifundisha kutawadhana miguu ni jukumu la Kila mwamini, lakini wewe unafundisha ule ulikuwa ni mfano tu wa rohoni n.k.

Je hayo unayoyahubiri Kristo angekuwa yupo hapo angewahubiria watu hayo unayoyahubiri wewe?..angewavumilia watu wanaowaacha wake zao na kwenda kuoa wengine?…angekuwa anafanya fanya mizaha unayofanya fanya leo madhabahuni au unapotumika? comedy..je angewahubiria watu waje kupokea magari na majumba na huku wanaangamia kwa uasherati wao na anasa zao?…

Je wewe ni mwakilishi mwema?..Bwana atusaidie tuwe wawakilishi wema kila siku katika kazi yake.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255789001312

Mada Nyinginezo:

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

CHAPA YA MNYAMA

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/21/je-wewe-ni-mwakilishi-mwema/