by Admin | 24 February 2020 08:46 pm02
Yesu Kristo Bwana wetu…Amefufuka kweli kweli..
Kila tukio lililokuwa linatendeka wakati wa kusulubiwa kwa Bwana Yesu, wakati wa kuzikwa kwake na wakati wa kufufuka kwake lilikuwa na makusudi maalumu na lilikuwa lina ufunuo mkubwa sana..Hakuna tukio hata moja lililokuwa linatokea kwa bahati mbaya au nje ya mpango wa Mungu.
Mpaka tukio la Bwana Yesu kubeba msalaba wake kuelekea Goligotha huku akiwa na majeraha mwili mzima ni tukio ambalo lilikuwa tayari limeshatabiriwa… “lilifananishwa na kondoo anayepelekwa machinjoni”
Isaya 53:7 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake”.
Tukio la Bwana kuchomwa mkuki ubavuni lilishatabiriwa (katika Zekaria 12:10), na lilikuwa linamaana kubwa katika roho na katika mwili..Katika Roho lilifunua utakaso wa damu na maji,. Kwa damu yake tunatakaswa dhambi zetu na kupata msamaha kabisa kabisa..na katika maji tunatakasika kwa Neno la Mungu (Waefeso 5:26)..
Na Kusudio lingine la kimwili, Bwana kuchomwa mkuki ubavuni wakati akiwa pale Kalvari..Ni kuhakiki kifo cha Bwana Yesu..Asingechomwa mkuki ubavuni watu wangesema alishushwa pale msalabani akiwa bado hajafa vizuri, na alipokwenda kupelekwa kaburini alikuwa hajafa vizuri hivyo uzushi mkubwa wa uongo ungezushwa wakati wa kufufuka kwake..
Kwahiyo Mungu wa mbingu na nchi alilijua hilo ndio maana akaruhusu wamchome mkuki Ubavuni ili wahakiki wenyewe kwamba amekufa…kwasababu katika hali ya kawaida hakuna mtu atakayeweza kuchomwa mkuki wa ubavu ukaingia mpaka ndani ya moyo halafu akabakia kuwa hai. Warumi walikuwa wanatumia njia hiyo kummalizia mtu ambaye hajafa vizuri.
Vivyo hivyo tukio la Pilato kuandika anwani kwa lugha tatu juu ya msalaba wa Bwana Yesu, tukio hilo halikuwa la bahati mbaya bali lilikuwa na maana kubwa sana katika roho..Kwani lilikuwa ni unabii kwamba siku zijazo Kristo atahubiriwa na kutangazwa kwa mataifa yote na kwa lugha zote.
Yohana 19:19 “Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.
20 Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa KIEBRANIA, NA KIRUMI, NA KIYUNANI.
21 Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
22 Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika”.
Baada ya siku chache, siku ile ya Pentekoste…wale walioshukiwa na Roho Mtakatifu..walisikika wakinena kwa lugha mpya za mataifa yote yaliyokuwa yanajulikana duniani. Ikimaanisha kuwa wakati umefika habari za kufa kwa Yesu na kufufuka kwake kuhubiriwa ulimwenguni kote kwa kila lugha, na kila jamii ya watu. Tangu huo wakati injili ilianza kusambaa ulimwenguni kote. Wakati huo zilikuwa tu hizo lugha tatu maarufu duniani, kiebrania, kirumi na kiyunani…Lakini leo tuna lugha Zaidi ya elfu 6 duniani…Na katika hizo zote Kristo kashatangazwa.
Kadhalika kwanini Bwana alipowekwa kaburini liliwekwa jiwe kubwa kulifunga kaburi na juu ya jiwe hilo pakawekwa muhuri? ambapo kazi ya muhuri huo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba kaburi limefungwa lote kisawasawa hakuna nafasi ya kupenya mtu au kitu chochote kile kuingia ndani. Na jiwe lile lilikuwa ni la uzani mkubwa sana..halikuwa kama yale yanayoonekana kwenye tamthilia..lilikuwa ni kubwa mno kiasi kwamba ilihitajika kukodi wanaume kadhaa kulisogeza..Ndio maana wale wanawake pamoja na idadi yao kuwa kubwa siku ile ya kwanza ya juma walipokuwa wanakwenda kaburini bado walihitaji mtu/watu wa kuwasaidia kulisogeza lile jiwe..
Marko 16: 2 “Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;
3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?
4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.”
Na malaika yule hakuliviringisha jiwe karibu na mlango kama filamu zinavyoonesha…bali liliviringishwa mbali na kaburi.
Luka 24:1 “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.
2 Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi”
Unaona ni mbali na kaburi..na si mbali na mlango …Ikiwa na maana kuwa lile jiwe lilihama kabisa kutoka katika yale mazingira ya makaburi.…jiwe walilikuta mbali kabisa, mahali ambapo hawakulitegemea…mahali ambapo si mazingira kabisa ya kusogezwa na mtu.
Kwahiyo Mungu aliruhusu liwe jiwe kubwa litumike, ili litakapoviringishwa mbali na kaburi..watu waamini kwamba hakika kuna kitu cha kimiujiza kimetendeka pale kaburini. Ni kweli Yesu kafufuka.
Na pia aliruhusu wale walinzi wawili wamwone yule malaika akishuka mbinguni kama umeme na waende kutoa habari za kufufuka kwake kwa wakuu wa makuhani (Mathayo 28:1-4)..maana pasingekuwepo mashuhuda upande wa makuhani pia, kungezuka uzushi mkubwa Zaidi ya ule uliozuka pale.
Sasa mambo hayo yote yalitokea ili sisi (mimi na wewe) tuamini kwamba ni kweli Yesu alisulubiwa, akafa na akafufuka kutoka katika wafu. Ukiamini hivyo leo hii basi utaokoka..Kama umeshawishika leo kuamini kwamba Kristo yupo hai leo, hayupo kaburini na kwamba anaweza kukuokoa maisha yako na wewe ukafufuka katika wafu… basi unachopaswa kufanya ni kutubu dhambi zako zote leo na kumwomba rehema..ulikuwa katika dhambi yeye anataka akusafishe na kukutakasa kwasababu anakupenda…
Upendo wake haupimiki wala haulinganishiki na kitu chochote..yupo tayari kukusamehe haijalishi umetenda dhambi ngapi kubwa..yeye atakusamehe zote na kusahau kabisa..na mbele zake utaonekana kama hujawahi kutenda dhambi kabisa….Sasa unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.
EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE,
NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.
Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithibitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, kama ulikuwa mwasherati usifanye tena uasherati, ulikuwa ni mtazamaji wa picha za ngono mitandaoni usifanye hivyo tena, ulikuwa mwizi, mtukanaji, mla rushwa, mtoaji mimba, muuaji, msagaji, mlawiti..usifanye hayo mambo tena…Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo namna hiyo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwabudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la BWANA YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.
Mungu akubariki, katika uamuzi wako wa busara unaoufanya..(huo ni uthibitisho wa kuamini kwamba Kristo amefufuka kweli kweli).
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789 001 312 jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?
Kwanini Bwana Yesu, aliruhusu yale mapepo yawaingie nguruwe?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/24/amefufuka-kweli-kweli/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.