JE! UMEFANYIKA KUWA MWANAFUNZI WA BWANA?

by Admin | 5 March 2020 08:46 pm03

Kuna mambo machache ya muhimu sana ya kufahamu pindi tu unapoamua kumfuata Yesu(kuwa mwanafunzi wa Bwana)..Mambo haya ni ya muhimu sana, ingawa wengi hawayajui na hata wakiyasikia wanaziba masikio yao wasitake kuyasikia wala kuyapokea. Na mojawapo ya hayo ni “kujikana nafsi”. Kama unasema umemwamini Yesu na bado hujajikana nafsi bado unakuwa hujaokoka.

Tafsiri ya kumfuata Yesu ni kujikataa wewe mwenyewe, kuyakataa mapenzi yako…kwamba hapo kwanza ulikuwa unapenda hichi na sasa unalazimika kukiacha, hapo kwanza ulikuwa unapenda kunywa hichi au kile na sasa unaamua kukiacha…hapo kwanza ulikuwa unapenda kufanya hivi au vile na sasa unakatisha, unaacha kufanya hayo mambo.

Hatua hiyo ukiikimbia kamwe huwezi kuzalisha chochote katika Imani.

Hali kadhalika, sio tu kuyakana mapenzi yako binafsi, bali pia na mapenzi ya Baba yako, au mama yako, au mwana wako… Baba yako hataki uokoke hapo huna budi kuyakataa Mashauri yake na kufuata ushauri wa biblia, mama yako anataka muende kwa mganga hapo huna budi kuyakataa mawazo yake hayo na kufuata ya kibiblia. Mtoto wako anakufanya usimtafute tena Mungu kama hapo zamani, unampenda kiasi kwamba upo tayari kula rushwa ili tu umpatie fedha za kwendea kwenye michezo…upo tayari kuiba na kutapeli au kufanya chochote kinachomchukiza Mungu ili tu umpatie mwanao kitu Fulani kitakachompendeza.

Bwana Yesu alisema maneno haya…

Mathayo 10:37  “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38  Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39  Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.

Usipojikana namna hiyo bado hujawa mkristo kabisa…Bwana amekukana, na wala huna ushirika wowote na wewe, haijalishi mchungaji wako atakufariji kiasi gani, haijalishi utafarijiwa na wapendwa kiasi gani, haijalishi utasoma mistari mingine ya biblia na kuona inakufariji kiasi gani, haijalishi utakuwa unahudhuria kanisani namna gani.…Lakini mbele za Kristo umekataliwa!.. Anasema mwenyewe hapo juu… “ukimpenda baba au mama au mwana kuliko yeye humstahili”..yaani maana yake haumfai. Anakwenda kumtafuta mwingine wewe haumfai.

Hutaki kuamua kuacha pombe, kuacha kuishi na mwanamke/ mwanamume ambaye hamjaona…yeye kakukataa, huna ushirika naye…unasema umeokoka lakini uasherati kwako ni kama chakula, haijalishi unalipa zaka, au unahudhuria ibada kiasi gani, au unaimba kwaya, au ni kiongozi wa maombi kiasi gani…Neno lake lipo pale pale… MTU ASIYECHUKUA MSALABA WAKE AKANIFUATA, HANISTAHILI.

Unasema umeokoka lakini unachati kwenye magroup ya ngono, magroup ya mizaha na matusi, unasema umeokoka bado unafanya mustarbation kwa siri, bado unavaa kama wanawake wanaojiuza. Hapo hujajikana nafsi..Hivyo HUMFAI!..kulingana na maneno yake mwenyewe. Hata sala zako hazisikilizi kwasababu wewe sio wake.. una mambo yako na yeye ana mambo yake…una mapenzi yako na yeye ana mapenzi yake…hamhusiani kwa lolote.. Yeye anatembea na kujidhihirisha kwa wale waliojikataa nafsi zao,.waliyoyakataa mapenzi yao na kuamua kuyafuata mapenzi yake yeye. Wengine wote walio nje na Neno lake hilo, kasema hawajui. Haijalishi ni mchungaji au muumini wa kawaida..kama hajajikana nafsi HAMFAHAMU.

Kama unaona aibu kuacha pombe, kama unaona aibu kumwambia ukweli huyo mwanamume/mwanamke unayeishi naye sasa kwamba umeokoka na hivyo Maisha ya dhambi huwezi kuishi tena…fahamu wewe na Bwana Yesu ni vitu viwili tofauti, kama unaona aibu kuacha kuvaa suruali na nguo zinazobana na na vimini kupaka make-up kwamba unaogopa/unaona aibu utaonekanaje mbele za wale waliozoea kukuona hivyo, au utaonekanaje mbele ya mume wako.. Kama unaogopa kufanya hivyo…tayari Kristo hayupo na wewe.

Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.

24  Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.

25  Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?

26  KWA SABABU KILA ATAKAYENIONEA HAYA MIMI NA MANENO YANGU, MWANA WA ADAMU ATAMWONEA HAYA MTU HUYO, ATAKAPOKUJA KATIKA UTUKUFU WAKE NA WA BABA NA WA MALAIKA WATAKATIFU”

Kama ulikuwa hujajikana nafsi na ulikuwa unadhani unaye Yesu moyoni mwako..Tubu tena leo!..Na baada ya kutubu, GEUKA! Acha yale maovu uliyokuwa unayafanya pasipo kutazama kwamba utamkwaza mtu au utachukiwa na mtu, au utagombana na mtu…acha ulevi, acha rushwa, acha uasherati, acha kujichua, acha kampani za marafiki wabaya..Wengi wanasema wamejaribu kuacha kufanya uasherati na kujichua wameshindwa hivyo wanahitaji maombi…nataka nikuambie bado hujajikana nafsi! hakuna maombi yoyote ya kuondoa hiyo tabia ndani yako..ni wewe kuamua kuiacha!…mbona hulali na kuku anayekatiza hapo pembeni yako, au mbuzi au ndugu yako wa damu, au mzazi wako? Hata ile hamu tu haipo!..hapo umeombewa na nani mpaka ukaishinda hiyo hali?..Umeona? hivyo hata hayo mengine usitafute kuombewa..Ni kutoyaendekeza tu na kuyaacha kabisa.

Na baada ya kutubu, usifanye tena hayo, ndipo Roho Mtakatifu atakuongezea uwezo wa kuyashinda hayo. Bwana anakupenda sana.

Bwana akubariki sana.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

NI KWANINI MUNGU HAONEKANI?

NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

KUOTA MTU AMEKUFA/NDUGU AMEKUFA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/05/je-umefanyika-kuwa-mwanafunzi-wa-bwana/