by Admin | 5 April 2020 08:46 pm04
SWALI: Chapa zake Yesu ni nini? Kama tunavyosoma katika Wagalatia 6:17?
JIBU:
Wagalatia 6:17 “Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.”
Kuna mambo machache ya kuzingatia hapo. 1) jambo la kwanza ni chapa 2) mahali Inapochukuliwa.
Chapa ni alama..Chochote kilichopigwa chapa maana yake kimewekwa alama inayokitambulisha kitu hicho kuwa ni milki ya kitu kingine. Kila bidhaa inayouzwa lazima ina chapa ya kampuni husika, au anayeizalisha. Sasa katika mstari huu Mtume Paulo anasema “tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.”..Maana yake ni kwamba “anachukua alama za Yesu katika mwili wake”..zingatia hilo Neno “mwilini mwake”..maana yake alama alizokuwa nazo Yesu na yeye anazichukua..kama uthibitisho wa kuwa milki ya Yesu.
Sasa kwanini Mtume Paulo alizungumza Sentensi hiyo kwamba TANGU SASA MTU ASINITAABISHE?
Ukianza kusoma kuanzia juu kidogo mstari wa 12 wa kitabu hicho cha Wagalatia utaona kuwa Mtume Paulo alikuwa anawazungumzia wayahudi ambao walikuwa wanawafundisha watu kuwa KUTAHIRIWA ndio uthibitisho au alama ya ki-Mungu…Kwamba alama au chapa pekee katika mwili ya kuonyesha kwamba wewe ni mtu wa Mungu ni KUWA UMETAHIRIWA, kama hujatahiriwa basi wewe huna chapa ya kiMungu au alama ya kiMungu. Hivyo wakawa wanawahubiria watu wengi mafundisho hayo potofu na hivyo kuwataabisha watu wengi hususani watu wa Mataifa. Sasa Paulo ndio akawa analisahihisha hilo na kusema, watu hao nia yao ni kutafuta kuona fahari au kupata wafuasi juu ya watu ambao watatahiriwa, lakini mioyoni mwao hata hawana mpango na Mungu..Na hapo ndio Paulo akasema mpaka sasa “tangu sasa mtu asinitaabishe kwa maana ninachukua katika mwili wangu chapa zake Kristo”..maana yake alama za Kristo kama uthibitisho wa kuwa Mkristo..
Sasa alama katika mwili wa Yesu ni zipi?..si nyingine Zaidi ya zile za Mateso, makovu ya misumari katika mwili wake, makovu ya viboko katika mgongo wake, uso uliotemewa mate, msalaba juu ya mwili wake n.k. Hizo ndizo alama au chapa za Yesu. Na hapa Mtume Paulo anasema naye pia anazichukua katika mwili wake…maana yake hizo ndizo zitakazomthibitisha kwamba yeye ni milki ya Yesu. Na sio KUTAHIRIWA.
Ndio maana utaona Paulo alijikana nafsi katika viwango vikubwa sana. Kama Bwana Yesu alivyochapwa viboko vingi, Paulo naye alichapwa idadi ya viboko 39 mara 5..
2Wakorintho 11:23 “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.
24 Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
25 Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi”.
2Wakorintho 4:8 “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
9 twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;
10 siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ILI UZIMA WA YESU NAO UDHIHIRISHWE KATIKA MIILI YETU.
11 Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti”
Hizo ndizo chapa za Yesu ambazo Mtume Paulo na mitume wengine walizozichukua katika miili yao. Hawakujisifia kutahiriwa kama wayahudi, wala hawakujisifia mavazi marefu na meupe katika miili yao kama alama ya kuwa watu wa Mungu, wala vyakula bali mateso katika Imani ndio iliyokuwa alama yao kuwa wao ni watu wa Mungu.
Je ni wao tu waliopaswa kuzichukua chapa za Yesu katika miili yao au pia ni kwa watu wote?
Jibu ni kwamba kila mtu aliyeokoka ni lazima azitwae chapa hizi..wengi hatupendi kusikia hivi kwasababu tunafikiri Ukristo ni kupata tu raha na burudani katika haya Maisha…Bwana Yesu alisema mtu yoyote akitaka kunifuata sharti ajitwike msalaba wake na ajikane nafsi yake ndipo amfuate…Maana yake huo msalaba atakaojitwika ndio utakaompeleka msalabani… msalaba alioubeba Bwana ulimpeleka kufa pale Kalvari kifo cha mateso…wewe na mimi ni misalaba gani tunayoibeba ambayo mwisho wa siku itatupekea kuifia Imani, au kuteswa kwa ajili ya Imani?..Misalaba unayovaa shingoni ni urembo tu.
Soma maandiko machache yafuatayo..ambayo yatakusaidia kujua kuwa Ni wajibu wetu wote kubeba chapa zake Yesu katika miili yetu..
Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; 30 mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba ninayo hata sasa.”
1Wathesalonike 3: 3 “mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo”.
Warumi 5: 3 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;”
2Wathesalonike 1:4 “Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili.
5 Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa”
Je umebeba msalaba wako na kumfuata Yesu?..kumbuka kubeba msalaba sio kuvaa mkufu wa msalaba shingoni bali ni kuukataa ulimwengu kama Yesu, kuishikilia Imani bila kuangalia ni nani anakubaliana na wewe au hakualiani na wewe…Kwa ufupi kama tukio lile lile lililotokea kwa Bwana nasi pia linapaswa lijirudie katika Maisha yetu.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.
WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.
UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE.
MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.
NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.
Kwanini Ibrahimu analitaja jina la YEHOVA wakati Musa anasema hakujifunua kwa jina hilo kwao?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/05/chapa-zake-yesu-ni-zipi-hizo/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.