by Admin | 9 April 2020 08:46 pm04
SWALI: Katika Luka 10:18, tunasoma Bwana Yesu alimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme..na katika Ufunuo 12:7-9 Biblia inasema kulikuwa na vita mbinguni na shetani akatupwa chini..Sasa ni wakati gani ambao shetani alitupwa chini? Kabla ya dunia kuumbwa au wakati wa Bwana Yesu akiwa duniani. Na je shetani sasa yupo kifungoni?.
JIBU: Katika Luka 10 tukianzia juu kidogo mstari wa 17 unasema…
“Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.”
Hivyo mstari huu hauzungumzii vita vilivyokuwa vinaendelea mbinguni kabla ya dunia kuumbwa..ambapo shetani alitaka kujiinua na kutaka kuwa kama Mungu, na hatimaye akafukuzwa mbinguni na kutupwa chini duniani..Bali unazungumzia habari za shetani kutoka katika nafasi ya juu aliyonayo juu ya watu wa Mungu na kushushwa chini..Ndio maana Bwana Yesu alizungumza maneno yale mara tu baada ya wanafunzi wake kutoka huko na huko kuhubiri injili na kutoa pepo wengi…Sasa kitendo hicho cha kwenda kufungua watu, na mateka kuwaacha huru, wale waliofungwa na nguvu za giza za shetani na mapepo yake hilo ndilo anguko la shetani kutoka juu mpaka chini, ambalo Bwana alikuwa analizungumzia hapo.
Hali kadhalika tukio tunalolisoma katika Ufunuo 12:7-9..Ndilo tukio la vita vilivyotokea mbinguni kabla ya dunia kuumbwa ambapo shetani alijiharibia nafasi aliyokuwepo ikasababishia kutupwa chini duniani.
Ufunuo 12:7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;
8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.
9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye”.
Hivyo maanguko ya shetani yapo mawili…Lile la kwanza ambalo lilitokea kabla ya sisi wanadamu kuumbwa, ambalo lilimfanya asiwe na uwezo tena wa kurudi mbinguni. Na anguko la pili ni la hapa duniani ambalo tangu wakati wa Bwana Yesu mpaka sasa linaendelea… na litakamilika katika mwisho wa dunia ambapo wale wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele watakapomalizika kuingia ndani na mlango wa Neema kufungwa (Hiyo ndiyo siku ambayo shetani ataanguka kikabisa kabisa)..
Siku hiyo ni siku ambayo shetani hatakuwa na chembe hata moja ya ngano mkononi mwake, atakuwa na makapi tu ambayo yatakwenda kuteketezwa kwa moto(Mathayo 3:12). Siku hiyo ndio atakuwa ameshindwa mbinguni na duniani.
Hivyo hata wakati huu tunapokwenda kuhubiri injili,kutoa pepo, kufungua watu, kuwafariji, kuwajenga kiimani na kuwatoa sehemu moja hadi nyingine, kama Mitume hawa walivyofanya…katika ulimwengu wa roho ni tunamnyang’anya shetani mateka kwa kasi sana na hivyo tunakuwa tunamwangusha katika ile nafasi aliyonayo ya juu na kumshusha chini..kwasababu nguvu ya shetani ipo katika idadi ya watu wa Mungu anaowateka sasa..
Hivyo ni muhimu sana kuhubiri injili kwa watu wote..
Sasa utahubirije injili?..Kwa maisha yako utahubiri injili, kwa uvaaji wako utahubiri, kwa mwenendo wako, kwa uimbaji wako, kwa maombi yako na kwa mchango wako wowote ule wa kifedha katika kazi ya injili utakuwa umeihubiri injili.
Na shetani hajafungwa sasa, bado yupo anafanya kazi atakuja kufungwa miaka 1000 baada ya mwisho wa dunia.
Bwana akubariki.
Maran atha
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Neno I.N.R.I kwenye msalaba wa Yesu maana yake ni nini?
Roho Mtakatifu ni nani?.
NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI.
Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?
Je ni wakina nani ambao hawataonja mauti mpaka siku ya kuja Bwana?
Je! Shetani alitolea wapi uovu?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/09/ni-wakati-upi-ambao-vita-vilipiganwa-na-shetani-kutupwa-chini/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.