Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

by Admin | 23 April 2020 08:46 pm04

SWALI: Habari mtumishi, naomba kujifunza habari hii ya kwamba, agano la kale ni kivuli cha agano jipya.., sasa ile habari ya Yusufu ilikua ina ufunuo gani kwa agano jipya?


JIBU: Ni kweli kabisa agano la kale ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika agano jipya biblia inatuambia hivyo katika (Waebrania 10:1, Wakolosai 2:17)

Kwa msingi huo basi ipo habari iliyojificha nyuma ya maisha ya Yusufu ambayo tukiijua tutafungua siri nyingi za Mungu zinazoendelea katika wakati huu wa sasa wa agano jipya.

Maisha ya Yusufu ni mfano wa Maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo kabisa tangu alipozaliwa hadi anakufa na hadi atakapokuja tena kuwaokoa wayahudi..

Kama tunavyofahamu, Yusufu mara baada ya kuwaeleza ndugu zake, kuhusu zile ndoto kuwa atakuja kuwatawala, mambo yalikuwa tofauti badala ya kumpenda walimchukia, na mwishowe wakamuuza kwa watu wa mataifa..

Mfano hai wa Bwana wetu Yesu alipokuja duniani, alikuja kwa watu wake(wayahudi), lakini walio wake hawakumpokea (Yohana 1:11), kinyume chake ndipo walipozidi kumchukia pale alipowaambia kuwa yeye ni mfalme, hivyo walichokifanya wakamweka mikononi mwa mataifa ili auawe,..

Na kama vile, Yusufu, alivyokwenda kuuzwa, Misri, na matokeo yake baada ya kutoka gerezani akavikwa mavazi ya kifalme na kuketi mkono wa kuume wa Farao na kukubalika na wamisri wote, akawa mkubwa sana, kule Misri, akajulikana sana na kuwa mkuu,..Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu, alipokataliwa na ndugu zake, wayahudi, akauzwa, na kuuawa na kuzikwa na kuwekwa katika kifungo cha kaburi kwa siku tatu…alipotoka kaburini kama vile Yusufu alivyotoka gerezani, hakuwa dhaifu tena…Bwana wetu Yesu aliketi mkono wa kuume wa Mungu baba kama vile Yusufu alivyoketi mkono wa kuume wa Farao.

Na kama vile mataifa yote ulimwenguni yalivyokuja kumwangukia Yusufu, na Bwana Yesu baada ya kufufuka kwake mataifa yote ulimwenguni yanamwangukia yeye sasa..Nafaka yote inatoka kwake mkuu wa uzima Yesu Kristo.

Hivyo kitendo cha Wayahudi kumkataa Yesu kimekuwa neema kwetu. ambapo mpaka sasa sisi tunaifurahia neema hiyo.. (Matendo 13:46-52)

Lakini wakati ulipofika wa Njaa kuipiga dunia na ndugu zake Yusufu kuona umuhimu wa kwenda kutafuta chakula cha uzima, ikawabidi washuke Misri kununua huko, ndipo wakakutana na ndugu yao Yule Yule ambaye walimuuza zamani..

Ndivyo ilivyo sasa, wayahudi wengi bado hawamwamini Bwana Yesu Kristo kama ndiye Yule masihi wao aliyetabiriwa atakayewaokoa, Leo hii ukiwaeleza habari za Yesu, wanaweza hata wakakupiga na hiyo yote ni kwasababu Mungu aliwapiga upofu kwa makusudi kabisa ili sisi watu wa mataifa tupate wokovu biblia inasema hivyo katika (Warumi 11:11-27)..Lakini utafika wakati ambao sasa upo karibuni, njaa ya kiroho itakuwa kali sana kwao…kiasi kwamba watahitaji maji ya uzima..na siku hiyo watamrudia Kristo naye atajifunua kwao tena kwa namna isiyokuwa ya kawaida, nao watamwamini..

Lakini jambo moja la kujifunza katika habari ile ya Yusufu ni kuwa, ule wakati ambao anataka kujifunua mbele ya ndugu zake, aliwaondoa kwanza watu wote wa nyumbani kwake, akiwemo mke wake, walipelekwa mbali na pale,..ndipo akajifunua mbele za ndugu zake..

Tusome..

Mwanzo 45:1 “Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze.

2 Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia”.

Vivyo hivyo kabla Kristo hajajifunua kwa watu wake wayahudi, litatangulia kwanza tukio la UNYAKUO, Kristo atamwondoa kwanza bibi-arusi wake kwanza, na ndipo atakapojidhihirisha kwa wayahudi..

Na ndio huo wakati wayahudi watalia sana,na kumwombolezea waliyemchoma kama tunavyosoma katika Zekaria 12:10-14..kutakuwa na maombolezo makubwa Yerusalemu, wayahudi watatubu dhambi zao kwa kumaanisha.., Na ndio huo wakati Mungu ataipigania Israeli kama ilivyokuwa zamani.. huo wakati hakutakuwa na neema tena kwa watu wa mataifa,..Kitakachobakia ni dhiki tu..

Hivyo tunaweza kuona, ni muda mfupi kiasi gani tumebakiwa nao..Hii neema hivi kwetu sisi watu wa mataifa ipo karibuni inaondoka kwetu na kurudi kwa waliokusudiwa kupewa tangu zamani, lakini sisi bado tunauchezea wokovu. Biblia inatufundisha wazi kabisa mambo yatakayoendelea huko mbeleni ni ya kutisha, hizi ni siku za mwisho.. Na leo hii tunayashuhudia, hivyo huu sio wakati wa mtu kubembelezewa wokovu, ni wakati wako sasa wewe uliyelala kuamka na kumgeukia Kristo katika hichi kipindi kifupi tulichonacho.

Maran Atha.

Mada Nyinginezo:

YONA: Mlango 1

UFANYE NINI KAMA MKRISTO WAKATI HUU WA JANGA LA CORONA?

SAUTI NI SAUTI YA YAKOBO, LAKINI MIKONO NI YA ESAU.

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

HISTORIA YA ISRAELI.

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/23/je-habari-ya-yusufu-inabeba-ujumbe-gani-kwa-agano-jipya/