HISTORIA YA ISRAELI.

HISTORIA YA ISRAELI.

Moja ya maswali yanayoulizwa na wengi ni kutaka kujua juu ya Historia ya Israeli/Taifa la Israeli/Wana wa Israeli..Lakini kiuhalisia historia ya Israeli ipo kwenye biblia. Ukisoma kitabu cha Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Kumbukumbu la Torati, hesabu, Yoshua, waamuzi pamoja na vitabu vya wafalme..vimeelezea vizuri sana kuhusu Taifa la Israeli/wana wa Israeli…

Hakuna mahali popote ambapo pameelezea vizuri historia ya Israeli kama kwenye Biblia takatifu..Hata kurasa kama Wikipedia na kamusi nyingine zote..zinatoa taarifa zao kuhusu Taifa la Israeli kwa kunukuu kutoka kwenye Biblia..Hivyo hakuna mahali pengine historia ya Taifa hilo inaweza kupatikana isipokuwa katika Biblia takatifu. Tatizo kubwa tulilonalo wengi wetu hatupendi kusoma Biblia, badala yake tunapenda kutafuta kusimuliwa au kufupishiwa habari fulani na watu ambao tayari wameshaisoma.

Hivyo hakuna tabia nzuri kama tabia ya kusoma Neno la Mungu..Matokeo ya kutolisoma Neno la Mungu (yaani Biblia) na kusubiriwa kutafsiriwa..Ni mwishowe kudondokea katika mikono ya mawakala wa shetani..ambao kazi yao ni kuipotosha kweli na kuingiza uongo katikati ya kweli. Na mtu akishadanganywa hawezi kujua kama kadanganywa au la..kwasababu hasomi biblia mwenywe.

Hivyo leo tuitazame kwa ufupi Historia ya Israeli.

Taifa la Israeli lilianza kwa ahadi…Yaani mtu mmoja aliyeitwa Ibrahimu alimpendeza Mungu, Hivyo Mungu akamwahidi kuwa atakuwa Taifa kubwa.

Mwanzo 12:1 “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;

2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;

3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”

Ahadi hiyo ilianza kutimia baada ya Ibrahimu kupata mtoto wa kwanza wa kiume..ambaye alimwita Isaka (Alikuwa na mwingine aliyemwita Ishmaeli lakini Ishmaeli hakuwa mwana wa Ahadi kwasababu alizaliwa na mwanamke mwingine)..Baadaye Isaka akamzaa Yakobo..Na Yakobo ambaye ni mjukuu wa Ibrahimu akazaa watoto 12. Hawa watoto 12 wa kiume waliozaliwa na Yakobo…waliitwa wana wa Yakobo…au watoto wa Yakobo…

Lakini ulipofika wakati fulani Yakobo jina lake lilibadilishwa na kuwa ISRAELI…Tafsiri ya jina Israeli ni “MSHINDI”. Hivyo kama jina lake limebadilika kadhalika na watoto wake hawakuitwa tena wana wa Yakobo bali wana wa ISRAELI. Na majina yao yalikuwa ni RUBENI, LAWI, ZABULONI, ISAKARI, NAFTALI, DANI, YUDA, SIMEONI, GADI, ASHERI, YUSUFU, na BENYAMINI.

Hawa wana 12, walioa wake na kuzaa watoto wengi..na watoto wao nao pia wakaoa na kuzaa watoto na wajukuu na vitukuu..Hatimaye Taifa likaanza kuwa kubwa na kufikia watu elfu 10, elfu 20, laki mpaka milioni..Kila kizazi kilichokuwa kinatokea kilirekodiwa asili ya Baba yake wa kwanza…kama ni Rubeni, au Lawi, au Gadi au mwingine yoyote alijulikana asili yake…Hivyo  majina ya Baba zao yakageuzwa na kuwa MAKABILA YAO. Hivyo kila mtu alikuwa na kabila lake miongoni mwa yale 12.

Sasa Kuna mambo waliyafanya wana wa Israeli yakawapeleka Misri, ambapo waliingia kwa amani lakini wakatoka kwa ushindani mkali. Baada ya kutolewa Misri na mkono wa Mungu mwenyewe…walianza safari ya kuelekea nchi ya Ahadi. Ijulikanayo kama KAANANI. Iliwachukua miaka 40 kukamilisha safari yao mpaka kufikia nchi ya Ahadi…Wakiwa njiani ndio huko huko Mungu akawa anazungumza nao na kuwapa AMRI za kuzishika na SHERIA ili wakafanikiwe wanapoiendea hiyo nchi ya Ahadi. Amri hizo zikiwemo kumtumikia na kumsujudia Mungu wao mmoja tu yeye peke yake aliyewatoa katika nchi Misri, nyumba ya utumwa…nyingine ni kuwaheshimu wazazi, kutokuiba, kutokuzini n.k

Walipoingia nchi ya Ahadi waligawanyiwa nchi hiyo kulingana na makabila yao.. kabila lenye watu wengi lilipewa sehemu kubwa ya ardhi, kadhalika lenye watu wachache lilipewa urithi mdogo.

Wana wa Israeli walipitia vipindi virefu vya kumsahau Mungu na kumrudia..Kizazi kilichofanya mabaya zaidi kiliadhibiwa na Mungu..na kile kilichofanya vizuri katika kuzishika amri na sheria za Mungu kilibarikiwa na kufanikiwa. Hivyo Mungu aliwafikisha katika nchi hiyo na kuwafanya kuwa wengi sana mamilioni..Na kutimiza Ahadi Mungu aliyemwahidia Ibrahimu.

Ilipofika wakati wa Ahadi ya Mungu kuuokoa ulimwengu..alimtuma mwanawe mpendwa ambaye alizaliwa katika Taifa hilo la Israeli…katika mnyororo wa kabila la YUDA. Yesu alizaliwa Maskini lakini alikuwa Mfalme..alikufa kifo cha aibu lakini alipofufuka alipata heshima…Yesu alifanyika kuwa wokovu kwa waisraeli wenyewe pamoja na watu wa mataifa.

Watu wa Mataifa ni watu wa mataifa mengine yote tofauti na taifa la Israeli. Waisraeli jina lingine wanaitwa WAYAHUDI..Wayahudi ndio hao hao waisraeli..hivyo uonapo mahali popote wanataja wayahudi basi fahamu kuwa ni hao hao waisraeli…sehemu nyingine wanatajwa kama Waebrania.

Taifa la Israeli lilijulikana kama Taifa teule la Mungu kwasababu ndio Taifa pekee duniani kote ambalo lilikuwa linamuabudu Mungu wa kweli YEHOVA. Aliyeumba mbingu na nchi…Mataifa mengine yaliyosalia yalikuwa yanaabudu sanamu, mizimu, miti na wanadamu. Ni Israeli pekee ndilo lililokuwa linamwabudu Mungu wa kweli..Ndio maana likaitwa Taifa Teule.

Mpaka leo Taifa hili bado lipo…na bado ni kipenzi cha Mungu…Ingawa wayahudi sasa hawamwamini Yesu kama Masihi.. lakini biblia imetabiri katika siku za mwisho watamwagiwa roho ya Neema na watamkubali Kristo.

Kijeografia, Taifa hili lipo katika Bara la ASIA, Eneo linalojulikana kama mashariki ya kati…Waisraeli kimwonekano wanakaribia kufanana na waarabu lakini si waarabu, wapo wayahudi pia wanaoishi mataifa mengine ya nje….Na nchi ya Israeli ni ndogo tu kama Mkoa wa Njombe wa Tanzania, lakini ina utajiri mwingi japokuwa asilimia kubwa ni jangwa…Na kwa sehemu watu wake wamejaliwa kuwa na uwezo wa ubunifu na uvumbuzi.

Idadi ya waisraeli waliopo Israeli sasahivi inakadiriwa kuwa Milioni 9. Nchi ya Israeli ndiyo nchi pekee duniani yenye idadi kubwa ya maadui kuliko nchi nyingine zote..Kwani imezungukwa na nchi za kiarabu pande zote ambazo zinalipinga vikali Taifa hilo.

Pamoja na maadui wote hao lakini bado Mungu anawashindania. Kwasababu anakusudi nao katika siku za mwisho. Kwani baada ya unyakuo wa kanisa kupita Mungu atalirudia tena Taifahilo kwa nguvu  na kuwapa watu wake moyo wa Toba…Wayahudi wote watatubu kwa machozi na maombolezo kwa uchafu wote wanaoufanya na kwasababu walimsulibisha Masihi wao…na Bwana atawaasamehe na kuanza kuwashindania tena kama nyakati za kale…na mataifa yote yatapanga vita dhidi ya Taifa hilo na Mungu atalishindia yote..

Hatuwezi kuandika mambo yote hapa kuhusu Taifa hilo…lakini kwa urefu kasome binafsi biblia hususani vile vitabu vitano vya Musa, ukihitaji kujua kama Israeli ilikuwa na mfalme au la kasome kitabu cha Wafalme..Ukitaka kujua kama Israeli ilishawahi kwenda utumwani tena kwa mara nyingine kasome kitabu cha Mambo ya nyakati..Ukitaka kujua kuhusu Hekalu la Mungu lililokuwepo Israeli kasome kitabu cha Wafalme…Ukitaka kujua Makuhani walikuwa ni wakina nani, na majukumu yao, na mavazi na kwa jinsi gani sadaka zilikuwa zinatolewa katikakati ya wana wa Israeli kasome kitabu cha mambo ya walawi…

Ukitaka kujua kwa urefu safari ya wana wa Israeli..mambo yaliyowakuta njiani wakati wanakwenda kaanani kasome kitabu cha Hesabu..Ukitaka kujua ni kwa namna gani walishindana vita na kutwaa urithi wao wakati wanaingia kaanani kasome kitabu cha Yoshua.

Ukitaka kujua sheria walizopewa, na hukumu pamoja na ahadi na aina ya vyakula walivyoamuriwa wale na vile walivyoambiwa wasile kasome kitabu cha kumbukumbu la Torati..Na ukitaka kujua ni kwa jinsi gani watarudiwa katika siku hizi za mwisho kasome kitabu cha Warumi.

Na mengine baadhi fungua masomo mengine mwisho wa somo hili..

Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Je umeokoka?..una uhakika wa kwenda mbinguni?..Kumbuka yeye ajaye anakuja upesi wala hatakawia.


Mada Nyinginezo:

WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.

NG’OMBE MWEKUNDU ALIYEZALIWA ISRAELI, ANAFUNUA NINI?

MAMBO YATAKAYOTOKEA ISRAELI SIKU ZA HIVI KARIBUNI.

BONDE LA KUKATA MANENO.

NITAFANYA YERUSALEMU KUWA JIWE LA KUWALEMEA .

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
M
M
2 years ago

Amina