OLE WAO WANAOJITAHIDI KUMFICHA BWANA MASHAURI YAO.

by Admin | 15 May 2020 08:46 pm05

Jina la Bwana Yesu libarikiwe ndugu yangu..Karibu tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima,

Biblia inasema..

Isaya 29:15 “Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?.

Mungu hapa anatupa onyo sisi tunaodhani kuwa kwa nguvu zetu wenyewe tunajitosheleza kuyaendesha maisha yetu,..tunasema hakuna haja ya Mungu kuingilia mipango yetu..hatuhitaji kumwomba Mungu, kwani yeye ni nani mbona hatumwoni akituongozea kitu chochote, Sasa ya nini kumuhusisha katika mambo yetu., Tunaweza tusiseme hivyo kwa midomo lakini moyoni mwetu tunawaza hivyo,..

Leo ninataka kwenda kuoa/kuoelewa ya nini nimwombe Mungu kuhusu mchumba mwema, wacha nikatafute tu anayevutia machoni pangu..Leo ninataka kufungua biashara mpya wacha nifanye tu yoyote nipendayo hata kama si halali ya nini kumshirikisha Mungu, leo nimepataka kazi nzuri ya nini kupelekea sadaka ya shukrani kanisani kwa aliyonitendea..Leo ninapokea mshahara mzuri, ninapata faida kubwa, ya nini kutoa fungu la kumi kwa kila mapato yangu, tendo hilo linaniongezea nini mimi?..Ya nini kuwapelekea wale wachungaji wapiga-dili wanaowaza kula sadaka zetu tu kila siku?…

Ukiamka asubuhi unachowaza, ni mipango yako tu, unasema hakuna Mungu,..,.Lakini unajua kabisa ukiumwa leo karibu na kufa utataka msaada kutoka kwa Mungu, unajua kabisa ukifa leo katika dhambi hujui utajikuta upande upi, unajua kabisa, upo mashakani kwa hofu za magonjwa, ajali, vifo vya ghafla n.k lakini bado kwako wewe habari za Mungu ni kama habari wa wajinga..za watu waliokataa tamaa za maisha, watu maskini, watu wasiokuwa na elimu, watu wavivu wa kufikiri..walioathiriwa na dini za wazungu,..Hivyo ndivyo unavyoyachukulia masuala ya imani.

Ndugu, Bwana anasema Ole,.. kumbuka sisi wanadamu ni mvuke tu ndugu, tushushe viburi vyetu dunia hii sio yetu, hata pumzi tulizonazo si zetu, ni kama tu tumekopeshwa na muhusika. Sasa kwanini uishi tu kama utakavyo?

Yakobo 4:13 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida;

14 walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.

15 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.

16 Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya”.

Tunapoishi maisha ya kama vile Mungu kwetu ni mtu-baki, hana umuhimu wowote, tujue kabisa tupo hatarini. Pale unapokutana na maneno ya Mungu halafu unatoa maneno ya mzaha,mzaha tu,au kejeli ni ujasiri gani unaokusukuma ufanye hivyo?

Unapokutana na Neno la Uzima, halafu unatukana, ni faida gani unapata, unaposhindana na sauti ya Mungu, hujui unajiharibu mwenyewe…Ayubu 40:2 “Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye”.

Kwasababu unaona Mungu amekaa kimya hafanyi chochote, ndio unajiamulia kuishi maisha unayotaka wewe,maisha yako yapo gizani, unaendelea kufanya dhambi kwa sirisiri ..Mungu amekuacha pasipo kujijua ndugu…Zaburi 81:12 “Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao”

Mithali 1:29 “Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.

30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.

31 Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

32 Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”

Ndugu, hata sisi tulikuwa hivyo tu lakini siku tulipoona haya maisha ni tambara bovu, tulimpokea Kristo na sasa tumeokolewa tunamtumaini na kumtegemea yeye, na mashauri yetu yote yapo kwake.

Na wewe leo, badilisha aina ya maisha unayoishi, mguekie Kristo, au kama ulikuwa ndani ya Kristo na umemsahau Muumba wako kwa kiwango hicho, ni wakati sasa wa kujinyenyekeza na kumkabidhi njia zako zote na mashauri yako yote,

Mithali 16:3 “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika”.

Hizi ni nyakati za kumalizia, tupo ukingoni kabisa wa muda, Kristo yupo mlangoni kurudi..Mguekie Yesu Mkuu wa uzima ayatawale maisha yako..Usimfiche mashauri yako, usimfiche chochote, hakikisha kila jambo lililo mbele yako Mungu ndio mshauri wako wa kwanza, hakikisha hufanyi chochote bila Bwana kuwa kiongozi wako.

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.

8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA

IFANYE KAZI YA MUNGU PASIPO HOFU!

USIJITAFUTIE KULAMBWA NA MBWA KWA DHAMBI YA KUTAMANI.

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

 

Mwaloni ni nini? Na je unafunua nini rohoni?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/15/ole-wao-wanaojitahidi-kumficha-bwana-mashauri-yao/