Kutoka 20:17 “Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako”.
Bwana ameweka msisitizo mkubwa sana, katika jambo hili ‘Usitamani’..Na utaona ni karibu nyanja ya vitu vyote alivyonavyo jirani yako.
Sasa Usitamani kunako zungumiziwa hapo sio kutotamani kuwa na kitu kama cha jirani yako, hapana, bali ni kule kutamani kile kitu (chenyewe) jirani yako alichonavyo, na hivyo unatafuta kila namna na kila mbinu ya kukipata..(yaani kukitwaa na kiwe cha kwako) Hiyo ndiyo Mungu anaichukia.
Dhambi hii inagharimu sana na ndio maana Mungu aliisisitiza….
Wapo watu wawili katika biblia tunaweza kuwachukulia kama mfano jinsi waliitamia dhambi hii na ikawagharimu vibaya mno,
(1)Wa kwanza ni Mfalme Daudi na
(2)Wa pili Ni Mfalme Ahabu.
Daudi alimtamani mke wa Huria, na kama tunavyojua ikamfanya atafuta kila njia ya kumwangamiza ili amchukue mke wake, kuifanya habari iwe fupi, leo hii hakuna mtu asiyejua madhara yaliyompata Daudi..ambayo yalimfanya ajutie tendo lile kwa miaka mingi sana, licha ya kufukuzwa tu na kuachwa na Mungu kwa muda, lakini pia masuria wake 10 walifanyiwa kitendo kilekile na mtoto wake mwenyewe aliyemzaa(Absalomu)..Jaribu kufiria ni aibu kiasi gani?..mtoto wako anawabaka wake zako mbele ya taifa zima (2Samweli 11-18)…
Vile vile mwingine ni Mfalme ahabu, yeye naye alitamani kiwanja wa Nabothi Myezreeli, baada ya kukiona ni kizuri na kipo karibu na ikulu yake, hivyo baada ya kunyimwa ikamfanya akose raha kwa muda mrefu mpaka mkewe Yezebeli, akaamua kwenda kumuulia Nabothi ili tu akichukue kiwanja kile..Na ahabu alipoona vile Nabothi ameshauliwa, hakuchukua hatua yoyote ya kutubu badala yake akaenda kukichukua kile kiwanja na kukifanya kiwe chake..Lakini tunaijua habari yake jinsi ilivyokuja kuishia mbeleni, jinsi mbwa walivyokuja kuiliamba damu yake mbele ya kiwanja kile kile cha Nabothi alichomuulia..(1Wafalme 21)
Tunapaswa tujiepushe na roho hii ya tamaa, kwamfano mwanamke mmoja ataenda nyumba ya jirani yake, halafu kule akamwona mfanyakazi wa jirani yake jinsi alivyo mzuri, mchapa kazi, mpishi mzuri wala hana usumbufu wowote..akiangalia huku nyuma , wa kwake ni mvivu, hafanyi kazi, Sasa, badala ajitahidi akatafute mwingine, mwenye vigezo kama vya yule wa jirani yake, yeye anaingiwa na tamaa, na kutafuta kila mbinu ya kumpata yule wa jirani yake, anaanza kumwahidia mshahara mkubwa, ili aache kazi kwa boss wake wa kwanza ahamie kwake..
Na kweli anafanikiwa lakini hajui kuwa na yeye mwisho wake utakuwa kama wa Ahabu wa kuliwa na mbwa, au kama wa Daudi wa kuabishwa na kufukuzwa..pale unapowatamani wake wa wengine..
Mwingine ni katika mambo ya biashara, anaona tu, mwenzake, Mungu anamfanikisha sehemu Fulani wateja wanakuja..Yeye naye anaingiwa tamaa, na kwenda kumwahidia mwenye pango kuwa atamlipa kodi kubwa Zaidi ili yeye aingie pale mwenzake alipokuwepo afanye biashara hapo..Hiyo ni tamaa yenye adhabu..
Na nyingine nyingi za namna hiyo..Na ndio maana Bwana alihitimisha na kusema.. “wala cho chote alicho nacho jirani yako”
Biblia inatuambia..
1Timotheo 6:6 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa”.
Tunapaswa tuwe watu wa kuridhika na vile tulivyonavyo..
Hivyo angalia je chochote, unachokitamani , Je, mwisho wa siku kitamuathiri jirani yako?. Kama ndivyo ni heri ukaacha..Uepukane na laana.. Na mapigo.
Ubarikiwe.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Ubatizo wa moto ni upi?
Kuota unafanya Mtihani.
“Ninyi ni chumvi ya dunia” Andiko hilo lina maana gani?
MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.
KWANINI MUNGU ALIMTUMIA MUSA KWA VIWANGO VILE?
Rudi Nyumbani:
Print this post