by Admin | 3 June 2020 08:46 pm06
SWALI: Mtu astahiliye hofu ni mtu wa namna gani kama tunavyosoma katika Warumi 13:7?
JIBU: Tusome,
Warumi 13:7 “Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima”.
Hofu inayozungumziwa hapo ni tofauti ni ile tuliyozoea kuitafsiri…Tafsiri ya hofu inayojulikana na wengi “ni ile hali ya kuwa na woga”..na hivyo kukufanya ukose ujasiri au ukose nguvu ya kufanya kitu Fulani…Kwamfano Mtu anapokutana ghafla na simba au kitu cha kumdhuru hofu Fulani inamuingia au woga, ambao unamfanya ahisi kwamba anakwenda kupatwa na madhara mbele yake. Sasa hofu ya namna hiyo sio inayozungumziwa hapo katika Warumi 13:7.
Hofu inayozungumziwa hapo inafanana na ile ya kumhofu Mungu/kumwogopa Mungu. Biblia inaposema tumwogope Mungu haimaanishi tumwogope kama tunavyomwogopa simba anapotokea mbele yetu, hapana!…Bali inamaanisha tumpe heshima ya hali ya juu sana, kwa kiwango ambacho tunaelewa madhara ya kutomheshimu ni kujipatia hukumu…Na hali hiyo haitufanyi kuwa waoga mbele yake bali inatufanya tuwe makini.
Sasa mstari huo ndio ulikuwa unazungumzia hofu na ya namna hiyo…”ya kumheshimu mtu kwa kiwango ambacho, unajua madhara yake endapo hutampa heshima hiyo”…Na ukianzia juu kidogo utaona Mtume Paulo alivyokuwa anazungumzia juu ya kuwatii wenye mamlaka…na hapa ndio anasema mwenye kustahili kodi apewe kodi (maana yake bodi za mapato kama TRA), wanastahili kodi zao, wenye kustahili ushuru wapewe, wenye kustahili hofu kama MARAISI, na Viongozi wengine wa nchi,..ambao wasipopewa heshima inayostahili wanayo mamlaka hata ya kumfunga mtu, wapewe hadhi hiyo.
Ni dhambi kutowaheshimu wenye mamlaka, ni dhambi kuwadhalilisha, ni dhambi kuwajibu bila hekima, ni dhambi kuwafanyia kiburi…maadamu hawaingilii imani yako, si sahihi kutowatii kwa vyovyote vile. Na sio tu viongozi wa nchi bali hata viongozi wa mashule kama waalimu, wahadhiri pamoja na viongozi wa mahali tunapofanyia kazi(yaani waajiri, ma-meneja na wakurugenzi).
Waefeso 6:5 “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, KWA HOFU NA KUTETEMEKA, KWA UNYOFU WA MOYO, KANA KWAMBA NI KUMTII KRISTO;
6 wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;
7 kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;
8 mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru”
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/03/mtu-astahiliye-hofu-ni-yupi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.