PETRO AKAMWAMBIA YESU “BWANA NA HUYU JE”?

by Admin | 4 June 2020 08:46 pm06

Tunajifunza kisa, ambacho kinamuhusu Petro, wakati wakiwa kule baharini yeye na wenzake, walipotokewa na Bwana,.. Swali la kwanza ambalo Petro aliulizwa na Bwana mara tatu ni Je! unanipenda?, Naye akajibu ndio Nakupenda,..Na hapo hapo Bwana akaanza akamweleza jinsi kifo chake kitakavyokuja kuwa siku atakapokuwa mzee, kwamba atafungwa na kuchukuliwa na watu asiowajua na kupelekwa kuuawa..

Lakini Petro aliposikia vile, hakuishia pale, alipeleka macho yake moja kwa moja kwa Yule mwanafunzi ambaye Bwana Yesu alimpenda [Ambaye ni Yohana], na Kumuuliza Bwana kuhusu habari yake naye, je! Na yeye Atakufaje?..Lakini maneno ya Bwana Yesu yalikuwa haya..

Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.

19 Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate.

20 Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?)

21 Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je?

22 YESU AKAMWAMBIA, IKIWA NATAKA HUYU AKAE HATA NIJAPO, IMEKUPASAJE WEWE? Wewe unifuate mimi.

23 Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe?

Utaona Petro alipomuuliza aliambiwa.., Ikiwa huyu nataka akae hata nijapo..Kwa lugha rahisi ni hii “Hata kama nikitaka huyu asife mpaka nijapo, Wewe inakuhusu nini? Unapaswa Unifuate mimi…

Hilo Neno “Imekupasaje wewe” Kwa Kiswahili fasaha ukiangalia katika tafsiri nyingine, limeandikwa kama ‘’Inakuhusu nini?’…

Hivyo Petro alikuwa anajaribu kijilinganisha njia yake na wengine, Lakini Kristo alikatisha maneno yake na kumwambia, hata nikiwa nataka Yohana aishi mpaka nijapo, wewe inakuhusu nini? , au inakuongezea nini kwenye niliyokupangia? Wewe fuata njia yako uliyowekewa.

Leo hii, tunajaribu kujifananisha na wengine, kisa mtumishi Fulani ahubiri namna hii, na mimi nihubiri hivyo, kisa Yule kafungua kanisa, na mimi nikafungue wakati huo huo, kisa Yule anahubiri kwa staili ile na mimi nikahubiri vile vile tunadhani ndio Mungu anavyotaka, au Yule anaimba namna hii na mimi ngoja nikaimbe kama yeye. Tunashindwa kukaa katika mapito ambayo Mungu ametuwekewa sisi, Ikiwa Yule anahubiri kwa kuandaa semina kubwa na kwaya nyingi, mimi ninayehubiri tu mtaani, Yale ya kwake yananihusu nini? Au yanaathiri vipi huduma yangu?

Kwanini niige kila anachokifanya yeye?.. Na kama ikitokea Mungu kamuandikia kifo kwa njia ile mwisho wa siku apigwe mawe, Je na mimi nitakuwa tayari kufa kama yeye?. Yeye amepangiwa kuishi miaka michache, hivyo kazi yake Mungu kampangia iende haraka haraka, lakini wewe umepangiwa miaka mingi ya kuishi uhubiri injili kwa miaka mingi, lakini pale unapoiga cha mwenzako na kuacha cha kwako, ndivyo unavyokwenda nje ya kusudi la Mungu.

Petro alipoona yeye, atakwenda kufa kwa namna ile, akasema ikiwa mimi nataondoka hivi, vipi kuhusu huyu ambaye aliyependwa na Yesu mpaka kuegema katika kifua chake, si ndo atakufa kifo cha utukufu zaidi yangu mimi?. Akadhani kila mtu ni wa kufa tu, ndio katimiza mapenzi yote ya Mungu.

Kila mmoja wetu kawekewa na Bwana jambo lake la kipekee, na njia yake ya kuifuata (kamwe hatuwezi tukafanana).. Kristo anasema nifuate, anamaanisha hivyo hivyo NIFUATE!..Hatutahukumiwa kwa sababu hutukuishi kama maisha ya mtu Fulani, au hutukufanya huduma kama ya mtume Fulani, bali tutahukumiwa pale ambapo hatukumfuata Yesu alipotuita kila mmoja wetu kwa njia yake.

Ukisimama kama wewe, iwe ni katika udogo, au katika wingi, maadamu upo katika mstari wa Bwana, hiyo inathamani kubwa sana kuliko kutumia kitu cha mtu mwingine kama kipimo cha utendaji wako kazi.

Bwana akubariki sana na atubariki sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu ni wakina nani?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Je! Ule mwiba uliokuwa katika mwili wa Paulo ulikuwa ni nini?

UZAO WA NYOKA.

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/04/petro-akamwona-akamwambia-yesu-bwana-na-huyu-je/