TUPO KATIKA ZAMU YA NNE YA MWISHO.

by Admin | 23 June 2020 08:46 pm06

Umewahi kujiuliza Zamu ya nne ni nini? Kama tunavyoisoma katika Mathayo 14:25?

Tusome,

Mathayo 14:25 “Hata wakati wa ZAMU YA NNE ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.

26 Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu”.

Miji ya zamani ilivyojengwa ni tofauti na miji za nyakati hizi zetu…Miji ya zamani ilijengwa huku imezungukwa na ukuta pande zote…na Mara nyingi ukuta huo ulikuwa ni mrefu sana na mageti yake makubwa kiasi kwamba hata gari la farasi liliweza kupita juu ya ule ukuta bila shida yoyote, mfano utaona ule ukuta wa Yeriko, ndivyo ilivyokuwa na miji yote mikubwa ni lazima izungushiwe ukuta, hata Babeli Pamoja na Yerusalemu ilijengwa kwa mifumo hiyo, na lengo la kuizungushia kuta ndefu ni kujilinda dhidi ya maadui…Mji ambao ulikuwa hauna ukuta ulikuwa unajulikana kama mji dhaifu..Na mageti ya mji usiku yalikuwa ni lazima yafungwe.

Na hilo tu peke yake lilikuwa halitoshi, katikati pia ya zile kuta Pamoja na pembezoni walikuwa wanatengeneza minara mirefu (iliyojulikana kama minara ya walinzi)..Minara hiyo walikuwa wanawekwa walinzi, ambao watakesha kwa zamu usiku kutazama pande zote kwa usalama wa mji.

Sasa walinzi hao walikuwa wanalinda kwa zamu (yaani kwa kupokezana)..masaa matatu matatu kwa vipindi vinne…zamu ya kwanza walikuwa wanaanza kulinda kuanzia saa moja jioni mpaka saa tatu usiku…kisha wanapokea wengine kulinda zamu ya pili kuanzia hiyo saa tatu usiku hadi saa sita usiku…kisha wanaingia wengine kulinda zamu ya tatu inayoanza saa sita usiku mpaka saa 9 usiku na mwisho inaingia zamu nyingine ya mwisho ya walinzi wengine kumalizia zamu ya mwisho ya 4, inayoanza saa 9 hadi saa 12 asubuhi.

Kwahiyo ilikuwa ni desturi tukio likitokea usiku, muda ule lilolotukia ulitambulika kwa ZAMU na si kwa masaa kama sasa nyakati zetu hizi tunavyofanya..

Hali kadhalika na sisi wakristo ni walinzi katika roho..tunamngojea Bwana arudi katikati ya hili giza nene la maasi na maovu ya dunia, na hatujui atarudi muda gani…hajaja katika zamu ya akina Petro ambao walikuwa macho wanakesha, mpaka wanaondoka duniani, halikadhalika hakuja katika zamu ya watu wa kanisa la pili na la tatu na la nne…na sasa tupo kanisa la mwisho la saba (lijulikanalo kama Laodikia kulingana na Ufu. 3:14)…ambapo ndio tupo ile zamu ya mwisho YA NNE, ni lazima Bwana aje katika hichi kipindi, hatujui siku, tarehe wala mwaka…lakini majira tunayajua…tupo wakati wa kurudi kwa Bwana mara ya pili.

Luka 12:36 “nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

37 Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia.

38 NA AKIJA ZAMU YA PILI, AU AKIJA ZAMU YA TATU, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

39 Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa.

40 Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu”.

Tupo katika dakika za hatari sana, kama katika watu ambao wangepaswa wawe macho juu ya suala la Unyakuo wa kanisa basi ni sisi, lakini cha ajabu ni kuwa wengi wetu tunachukulia kimzaha mzaha tu, tunaishi kama tunavyotaka,tukidhani na mbinguni pia tutaingia tu kama tunavyotaka..Tupo buzy ni shughuli za ulimwengu huu, hatuna habari na Mungu..Bwana atusaidie katika hili ili sote tujue zamu tuliyopo, kuwa ndio ile zamu ya nne ya mwisho, na kwamba zamu hii haitapita kabla Kristo hajarudi…Wakati umeenda sana ndugu.

Je! umesimama imara na wokovu.

Bwana atupe macho ya kuliona hilo.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

SI KWA FAIDA YA MWENYEZI, BALI KWA FAIDA YETU.

Kwanini wakristo wengi ni maskini?.

Ni kwa namna gani Yesu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka?

Ni uthibitisho upi unaoonyesha kuwa kuna MBINGUNI na KUZIMU?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/23/tupo-katika-zamu-ya-nne-ya-mwisho/