PARAPANDA ITALIA.

by Admin | 5 July 2020 08:46 pm07

Siku moja inapopita, ndivyo tunavyoikaribia ile siku kuu ya kwenda mbinguni, siku ile ya Parapanda kulia, ambapo watakatifu wote duniani wataisikia, hakika itasikiwa na wao tu, na sio kila mtu duniani kama wengi wetu tunavyodhani…Watu wenye dhambi wakati huo hawataisikia parapanda hiyo hata chembe..

Siku hiyo pengine itakuwa ni asubuhi kwa upande wetu, au jioni au  usiku wa manane ukiwa umelala.. Kama wewe ni mtakatifu utasikia sauti nzuri ya shangwe, ikiambatana na parapanda ya Mungu, na wale wafu waliokufa katika Kristo, wao nao pia wataisikia kutoka kule makaburini, na kufufuka na kuanza kutembea duniani, na wewe utawaona, halafu ghafla, tutaliona jeshi kubwa la malaika likitokea, likiambatana na Bwana, na wakati huo huo ghafla tutaona miili yetu ikibadilishwa kutoka katika miili hii ya unyonge ya mauti na kuwa miili ya utukufu, wakati hilo likuwa linaendelea katika kipindi kifupi sana cha kufumba na kufumbua tutajikuta mawinguni na Bwana YESU, huo ndio wakati tutaenda naye kule mbinguni kula naye ile karamu ya mwana kondoo aliyokwenda kutuandalia miaka 2000 iliyopita.

Unaweza kudhani jambo hilo ni bado sana, lakini nataka nikuambie mimi na wewe tunaishi katika yale majira ya kuja kwa Bwana mara ya pili. Dalili zote zinaonyesha, Angalia milipuko ya magonjwa mfano wa Tauni (Corona) yaliyotabiriwa na Bwana Yesu yakitokea ulimwenguni (Luka 21:11)..Hiyo ni dalili ya kwamba tupo ukingoni mwa wakati kuliko tunavyoweza kudhani, angalia tena kuchipuka kwa taifa la Israeli, yaani mtini, ndio kunathibitisha kabisa wakati wa majira ya mataifa(yaani mimi na wewe) upo ukingoni.

Jambo ambalo wakristo wengi hatufahamu, ni pale tunapodhani Mungu ana ile kauli ya “wengi wape”..Yaani, kwasababu ulimwengu huu uliojawa na uovu na waovu wengi Mungu hawezi kuuangamiza au kunyakua wale wachache walio waaminifu kwake..

Yesu alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, na kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, jiulize, waliookoka katika siku za Nuhu walikuwa ni wangapi kama sio 7 tu katika ya mabilioni ya watu waliokuwa ulimwenguni, vilevile waliookoka katika siku za Lutu walikuwa wangapi kama sio watatu katika ya Malaki ya watu waliokuwa katika miji ile ya Sodoma na Gomora,

Ukitazama tena kwa ukaribu utaona aliye nyakuliwa alikuwa  ni mtu mmoja tu (HENOKO) kati ya watu wote waliokuwa wanaishi kipindi chote kabla ya gharika, kwasababu ni yeye tu peke yake ndiye aliyempendeza Mungu.

Vivyo hivyo katika wakati huu watakaonyakuliwa ni wale tu watakaompendeza Mungu, hao ndio peke yao watakaosikia Parapanda ya Mungu ikilia kutoka mawinguni, hata kama watakuwa ni watu 100 katika ulimwengu mzima, hao tu ndio watakoenda, wengine wote waliosalia hawatajua chochote, watashangaa tu mbona kundi dogo la watu wachache sana halipo duniani..

Wengine watadhani, wameibiwa tu, wengine watadhani wametoroka, n.k. Lakini ulimwengu hautaelewa chochote kwasababu litakuwa ni kundi dogo sana, kumbe hawajui wenzao siku nyingi tayari wapo mbinguni wakila karamu ya mwana kondoo, lakini huku chini kitakachokuwa kinaendelea ni dhiki kuu ya mpinga Kristo. Na baada ya hapo ni maangamizo.

1Wathesalonike 4:16  “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.

17  Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18  Basi, farijianeni kwa maneno hayo.”

Ndugu yangu jiulize, Yesu akirudi leo utakuwa katika upande upi? Na injili zote hizi ulizosikia utajitetea vipi siku ile kusema hujaambiwa? Ishara zote hizi za siku za mwisho utajitetea vipi siku ile mbele za Mungu? Mungu ni mwingi wa rehema lakini pia ana ghadhabu nyingi.

Ili kufahamu vizuri ni jinsi gani tunaishi katika siku za mwisho angalia MADA nyingine, mwisho kabisa wa somo hili, uone ni wakati gani huu tunaishi..

Kama hujaokoka, basi huu ndio wakati wako wa kuyatengeneza mambo yako na Kristo, ili kusudi kwamba hata ikitokea paraparanda italia leo usiku basi uwe na uhakika kuwa na wewe utakwenda kumlaki mawinguni. Unachopaswa kufanya ni kukusudia tu kumkaribisha Yesu maishani mwako, kwa kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, na kuwa tayari kuyaanza Maisha mapya  ya wokovu.

Kama utamaanisha kufanya hivyo ni ahadi yake kuwa atakuja ndani yako na wewe kuanzia huo wakati utaanza kuona badiliko kubwa ndani yako, hivyo kama upo tayari kufanya hivyo sasa,

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana.

Tazama mada nyingine chini zinazoeleza Habari za kurudi kwa Kristo duniani..

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

MAONO YA NABII AMOSI.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/05/parapanda-italia/