by Admin | 24 July 2020 08:46 pm07
Shalom, mtu wa Mungu.. karibu tujifunze biblia Neno la Mungu, ambalo ni mwanga wa njia yetu na taa iongozayo miguu yetu.
Leo tujikumbushe umuhimu wa kuwa wakaribishaji, na wa kujitoa kuifanya kazi ya Mungu.
Kipindi kirefu kidogo nimekuwa nikiwasiliana na binti mmoja humu facebook, ambaye anaishi kwao na wazazi wake, kiukweli ni binti anayempenda Mungu na kujitoa kwa Mungu ingawa ni mdogo kiumri. Amekuwa akitutumia maswali kadha wa kadha na kumjibu..kama ni mfuatiliaji wa masomo ya humu utakuwa umewahi kusoma swali tulilolijibu linalouliza… “Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?”…na lingine “Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?”.. Maswali haya mawili yaliulizwa na huyu binti..Na yapo mengine aliyouliza ambayo majibu yake tulimtumia pasipo kuyaweka wazi.
Huyu binti ni mtanzania lakini anaishi Zambia, karibu na mpaka wa Tanzania. Japokuwa ni binti mdogo lakini amekuwa akituuliza maswali kuhusu siku za mwisho na pia maswali ya namna ya kwenda kuwahubiria wengine Habari za Yesu mitaani. Katika udogo wake tulimtia moyo asiache kuwashuhudia wengine kwa bidii zote, haijalishi mazingira aliyopo, na mambo mengine mengi tulimshauri. Alienda kuyafanyia kazi hayo tuliyomshauri..na baada ya muda akatuletea mrejesho kwamba ametoka kuwashuhudia baadhi… “Anasema ijapokuwa huku nilipo makanisa yamefungwa kutokana na hofu ya corona, lakini mimi nilitoka hivyo hivyo sikujali.. na niliowashuhudia wengine wametaka namba zangu niwaombee na kuwaongoza sala ya toba” (kama kawaida hizo ni Habari za furaha kwetu sisi kama wakristo)..
Ni binti pia ambaye anayepitia changamoto nyingi, na hata nyumbani alipo sio kwamba ni watu wa Imani sana, hata wale anaowashuhudia na kuokoka anaogopa kuwakaribisha nyumbani kwasababu ya vita vya nyumbani….yaani kwa ufupi ni binti aliyejitoa kweli, na mwenye upendo wa ki-Mungu, yupo tayari kwenda kuwasaidia watu roho pasipo kujali mazingira aliyopo.
Sasa siku kadhaa nyuma, alipata mgeni kama yule Ibrahimu aliyekutana naye wakati anatoka kumpiga Kedorlaoma (Mwanzo 14:8-18)..
Hebu msikilize…
“Jana asubuhi sana niliamka nikawa naosha vyombo asa nikaenda kumwaga maji machafu ya vyombo nje nikachukua funguo nikapitia kufungua geti kubwa la nje , nikasikia sauti ikiita jina langu kwa sauti ya mbaali niliisikia lakini nikajua labda Ni mawazo tu, ikaita Tena ile nataka kuingia ndani nikainua macho getini nikamuona Mtu nisiyemjua anabisha hodi nikafungua nilivyofungua nikamsalimia kwa Adabu na heshima ya Hali ya juu kama kawaida yangu japo alikuwa m-baba mrefu mweusi amevaa nguo mbaya mbaya za (kimasikini) Mimi simjui asa nikajua labda Ni mgeni wa Baba labda alimpigia simu aje , kumbe sio, akaniambia unahitaji nini nikamwambia hamna Baba, huku naendelea kumsikiliza kwa makini kwa karibu , akaniambia chukua pesa hizi usiwe na shida, akanipa na vyakula Kisha akatoa pesa nyingine akanipa Sasa ile nimeshapokea pesa na vitu, nikamwambia YESU anakupenda akasema ndio nawewe (Mimi) anakupenda pia nikamwambia Asante! ,Sasa nikaweka vitu chini nikwambie umeokoka?, unaitwa Nani? Ile nainuka sikumuona Tena yule m-baba” .
Mwisho wa nukuu.
Sasa Baada ya kumuuliza alikupa nini kingine tofauti na hizo pesa?…akaniambia alimpa BIBLIA, TENZI ZA ROHONI, DIARY Pamoja na KALAMU.
Ndipo nikajua ni malaika kamtembelea…Na bahati nzuri huyu binti anayajua maandiko na analijua hili andiko pia…
Waebrania 13:2 “Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua”.
Hivyo baada ya tukio hilo ajijua kabisa ni malaika wa Bwana, na amani ya ajabu iliingia ndani yake..
Ndugu, haya mambo sio hadithi, ni vitu vya kweli kabisa…Kwasababu hata Mimi binafsi vilishawahi kunitokea mara mbili katika mazingira yanayokaribiana kufanana na huyu binti. Malaika wa Mungu mamilioni kwa mamilioni wanazunguka ulimwenguni..na wala usitegemee watakuja wamevaa nguo nyeupe na mabawa…Hapana!. Wale waliomtembelea Lutu hawakuwa na mavazi meupe, waliomfuata Ibrahimu chini ya mialoni ya Mamre hawakuwa na mavazi meupe…wanakuja kama watu tu wa kawaida kabisa..Ndio maana Paulo anasema “wengine mnawakaribisha Malaika pasipo kujua”.
Huyu binti yeye kaletewa zawadi chache za kumtia moyo kwamba azidi kusoma Neno na kujifunza (Ndio maana kapewa biblia na diary) Pamoja na kuwashuhudia wengine, na Bwana amemfanyia vile kumwonesha kuwa anampenda na yupo Pamoja naye kumhudumia katika mahitaji yake hata ya chakula hivyo asiogope! Na zaidi alimpa pesa nyingi sana..ndio maana kamtuma Malaika wake kumfariji. Na ule ni udhihirisho mdogo tu wa mambo yanayoendelea katika roho, katika roho anazungukwa na hilo jeshi la malaika wengi sana. Popote anapokwenda wapo naye, kumlinda na kumtunza.
Jiulize je angekuwa si mtu wa kujali na kujitoa kwa ajili ya roho za wengine malaika wa Bwana angetumwaje kwake?..Biblia inasema malaika ni viumbe wa roho wanaofanya kazi ya kuwahudumia Watoto wa Mungu wale watakaoirithi ahadi..na si kila mtu tu!
Waebrania 1:14 “Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”
Sasa angetumwaje kumhudumia kama angekuwa si mtu wa kuifanya kazi ya Mungu?..Malaika wa Mungu angetumwa amletee zawadi gani ya kumfariji kama angekuwa ni binti wa kushinda tu kuzurula zurula mtaani au kuzungumza umbea au kutembea tembea na wavulana mitaani?..Unaona?..hakuna chochote angeambulia…
Na kitu kimoja ambacho hakifahamiki na wengi ni kwamba Malaika wana kazi ya kupeleka mambo yetu mema tunayoyafanya mbele za Mungu..Lolote zuri unalolifanya malaika wanalipeleka kama hoja mbele za Mungu..kama utapenda tukutumie somo juu ya hilo..utatutumia ujumbe mfupi inbox.
Naamini ushuhuda wa huyu dada ni darasa tosha kwetu!…Katika nafasi tulizopo, hebu tujitoe kwa Mungu…usijitoe ili utokewe na Malaika hapana!..jitoe kwasababu unaona umuhimu wa wengine kuujua ukweli na kupata wokovu maishani mwao. Nafasi ndogo unayopata kama ni shuleni, nyumbani, kazini, kwenye mitandano, usitengeneze visingizio vingi..kwamba siwezi kwasababu ya hichi au kile..kwasababu nipo bize..Ifanye kazi ya Mungu, wengi bado wanahitaji kuokolewa. Malaika wa mbinguni wanafurahi mtu mmoja tu anapotubu!
Bwana atubariki na Bwana atusaidie.
Kama hujaokoka!..Wokovu unaanzia hapa hapa duniani!..usidanganywe na shetani kwamba hakuna kuokoka duniani, usidanyike mtu wa Mungu…Tubu leo kama bado..na kisha acha yote machafu uliyokuwa unayafanya kama ulevi, uasherati, wizi, utazamaji pornograph, utukanaji, uuaji, usengenyaji na mengine yote..Na baada ya hapo, tafuta kanisa lililo hai, lililopo karibu na mahali ulipo, hakikisha unabatizwa hapo katika ubatizo sahihi wa jina la Yesu na wa kuzamishwa mwili wote(Matendo 2:38). Na baada ya hapo Roho Mtakatifu atakuongoza kufanya yaliyosalia.
Unyakuo upo karibu na hizi ni siku za mwisho..siku yoyote! Mambo yatageuka ghafla, unyakuo utapita, watakatifu watatoweshwa..dhiki kuu ya mpinga-Kristo itaanza, na ghadhabu ya Mungu itamwagwa duniani.. hakuna mtu atategemea, itakuwa ni ghafla tu!..kama vile corona ilivyozuka ghafla tu! pasipo ulimwengu kutegemea.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA.
MTU ASIYE PAMOJA NAMI YU KINYUME CHANGU.
UFUFUO TUNAOUSUBIRIA UTAHITIMISHA YOTE.
HUDUMU YA MALAIKA WATAKATIFU.
MAJESHI YA PEPO WABAYA.
SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?
KWANINI HUNA HAJA YA KUANDIKIWA JUU YA NYAKATI NA MAJIRA?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/24/jifunze-kujitoa-kwa-mungu-na-kuwa-mkaribishaji/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.