KWANINI HUNA HAJA YA KUANDIKIWA JUU YA NYAKATI NA MAJIRA?

KWANINI HUNA HAJA YA KUANDIKIWA JUU YA NYAKATI NA MAJIRA?

1 Wathesalonike 5:1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya NYAKATI NA MAJIRA, hamna haja niwaandikie.

2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa SIKU YA BWANA yaja kama vile mwivi ajavyo usiku”.

Shalom.

Katika mistari hiyo miwili, yapo mambo mawili pia ninataka uyaone. Jambo la kwanza ni “Nyakati na Majira” na Jambo la pili ni “Siku ya Bwana”..Mtume Paulo ameitenganisha hiyo mistari miwili, kwasababu inazungumziwa vitu viwili tofauti,

Kwamfano tukianzana na huo mstari wa Kwanza, unazungumzia Nyakati na Majira ya kurudi kwake Bwana, lakini huo wa pili unazunguzia siku yenyewe ya Bwana itakavyokuwa..

Sasa mpaka mtu anaposema kwa habari ya nyakati na majira sina haja ya kuwaandikia..anamaanisha kuwa suala la majira na nyakati ambayo Kristo atarudi ni jambo ambalo kila mtu anajua, sio siri lipo wazi!, limeshaelezwa kila mahali, sio jambo jipya..na ndio maana hawezi kuandika tena kuwakumbusha watu..

Nataka nikuambie ndugu yangu ikiwa wewe ni mkristo na mpaka sasa bado hujui majira na nyakati za kurudi kwa Yesu duniani kulinyakuwa kanisa lake, basi ujue kuwa kuna tatizo kubwa sana katika Imani yako tena sana ambalo utanatakiwa ulichukulie ‘seriously”…

Biblia imetuweka wazi kabisa na kutuambia tukishaona majira Fulani au nyakati zimebadilika basi tujue ndani ya hicho kipindi siku yoyote Kristo anarudi..Ili kuelewa vizuri tafakari mfano huu,

Leo hii labda unatafuta Kazi mahali fulani, kwenye shirika Fulani la utafiti wa kilimo, halafu ukapata, ukaitwa kwenye interview, ukafanikiwa kupita, lakini wakakwambia kazi yetu rasmi itaanza kipindi cha msimu wa masika, hivyo tutakupigia simu wakati huo ukifika hakikisha tu unakuwa hewani wakati wote, ili tusikukose pindi kazi zitakapoanza. Lakini ukiangalia wewe leo hii upo mwezi wa 9 na umeshajua masika huwa inaanza kuanzia mwezi wa 2-5 mwakani..

Sasa kwa namna ya kawaida hichi kipindi cha katikati utakuwa kawaida tu, lakini itakapofika mwakani kuanzia mwezi huo wa 2 hadi wa 5, utakuwa makini sana, utakuwa karibu na simu yako kwasababu unajua wakati wowote, utapigiwa simu ukaanze kazi,.Unaona hapo! hujapewa tarehe lakini umepewa majira na Nyakati..inaweza ikawa mwezi wa pili mwanzoni, au wa tatu mwishoni, au wa nne katikati hujui..bali utajiweka tayari muda wowote..

Vivyo hivyo na sisi wakristo, tumepewa majira ya kurudi kwa Bwana Yesu, lakini hatujapewa siku, wala saa. Na majira yenyewe ndio haya tunayoyaishi sasa.. Ndugu katika wakati ambao tungepaswa tuwe makini sana na wokovu wetu basi ni katika majira haya.. Kwasababu Bwana Yesu alituambia, mtakapoanza kuona milipuko ya magonjwa yenye mfano wa Tauni yanaipiga dunia (Corona) Luka 21:11 basi mjue yupo mlangoni, mtakapoona matetemeko ya nchi, basi mjue mpo ndani ya wakati huo, mtakapoona wimbi la manabii wa uongo wengi wakizuka duniani, mtakapoona watu wanapenda anasa kuliko kumpenda Mungu, watu wanapenda fedha, basi mjue hayo ndio majira yenyewe.

Mtakapoona maasi yanayongezeka kwa kasi (ushoga na uuajji), upendo wa watu wengi kupoa, kutokea kwa wimbi kubwa la watu wenye kudhihaki wakisema mbona huyo Yesu haji, dunia ipo vilevile wakati wote,(2Petro 3:3) basi tujue tupo katika hayo majira kabisa…

Na ndio pale sasa tukirudi katika ule mstari wa Pili anasema..

2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa SIKU YA BWANA yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

Tukiwa katikati ya majira hayo, ghafula wakati wowote, muda wowote, Bwana atatokea kama mwizi ajavyo usiku.. Kwa bahati mbaya kwa upande wao watasema mbona duniani tupo salama na kuna amani, Hapo ndipo Unyakuo unapita kwa ghafla sana na kwa haraka..wafu wanafufuliwa, na watakatifu wachache sana wanatoweka duniani..

Wakati baadhi ya watu wakipigwa butwaa kufikiri ni nini kimetokea mbona watu wachache hatuwaoni duniani..(wengi watajua ni kawaida watu kupotea potea na kuja kupatikana baada ya siku/miaka kadhaa hivyo watapuuzia) hapo ndipo mpinga-kristo ataanza kufanya kazi..wakati huo dunia haitakuwa na zaidi ya miaka 7, usitamani wakati huo ukukute kwasababu kutakuwa ni vilio na kusaga meno kwa watakaobaki.

Embu jiulize, ni kitu gani kinakufanya uishi maisha ya kubahatisha-bahatisha wakati huu wa siku za mwisho? Neema tuliyonayo haitakuwa hivi sikuzote, upo wakati utatamani ungerudi siku moja nyuma utengeneze mambo yako lakini haitawezekana, wakati huo wenzako wakiwa wanakula karamu ya mwana kondoo mbinguni wewe utakuwa umebaki halafu kibaya zaidi uliujua ukweli lakini hukuukubali kwa wakati.

Ndugu tubu dhambi zako, mgeukie mkuu wa uzima YESU KRISTO, azifute dhambi zako..Achana na mambo ya ulimwengu hayakufikishi popote, wala hayakupi faida yoyote wewe mwenyewe unajua. Hivyo fanya uamuzi mwema wa kugeuka na kumfuata Yesu ili uwe na amani katika kipindi cha maisha yako ulichobakiwa nacho hapa duniani.

Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Kristo awe pamoja na wewe, na pamoja na sisi sote.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments