by Admin | 11 September 2020 08:46 am09
SWALI: Nini maana ya huu mstari.. Mhubiri 7:10 “Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo? “
JIBU: Mstari huo kwa lugha ya kueleweka zaidi ni sawa na kusema, “Usiseme mbona siku za kale, au nyakati za zamani zina afadhali kuliko siku hizi au nyakati hizi nilizopo mimi? Kwani kusema hivyo hujatumia hekima kufikiri.”
Msemo huu, ni maarufu hata sasa, tunaona kama wale watu wa zamani walikuwa ni watu wa ki-Mungu sana kushinda sisi, Au Watu wa zamani walikuwa wanaishi kwa raha kuliko watu wa sasahivi..Tukiwa tunafikiri hivyo ni ishara kuwa tumeshindwa kuyatimiza majukumu yetu ya msingi tuliyokabidhiwa sasa na Mungu, kwa kisingizio kuwa majira yamebadilika.
Ukweli ni kwamba hata hao watu wa kale ungewafuata na kuwauliza, nao pia wangekuambia heri watu wa kale kuliko sisi wa kipindi chetu.. Hivyo sisi sote tumepewa nafasi sawa, biblia inaposema hakuna jipya chini ya jua, fahamu kuwa unachokipitia sasa, ndicho walichokipitia watu wa kale, unayoyaona sasa ndiyo waliyoyaona wale, kama maovu yalikuwepo, tena pengine mengi kuliko unayoyaona wewe leo, mpaka wengine wakafikia hatua ya kugharikishwa na wengine kuteketezwa na moto.
Hivyo kama unaona wengi wao walikuwa karibu na Mungu, basi ni katika shida kama ulizonazo wewe, ni katikati ya maovu kama unayoyapitia wewe. Hivyo kusema heri siku za zamani kuliko hizi, ujue kuwa hutumii hekima kuuliza hivyo.
Ikiwa tunaukataa wokovu sasa au unakataa kuitenda kazi ya Mungu kwa kisingizio kuwa shughuli zinatusonga nyakati hizi zimebadilika, sio kama zamani, tujue kuwa hiyo sio hoja mbele za Mungu.
Ikiwa hatujizuii na mambo ya ulimwenguni, kwa kisingizio kuwa tunaishi katika majira ya dhambi kuliko mengine yote, kisa tunazo Internet, na simu, basi tujue kuwa hizo bado sio hoja mbele za Mungu.
Biblia inasema wapo watakaoshinda ulimwengu vizuri katika siku za mwisho, kuliko hata wale wa kwanza,
Luka 13:29 “Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.
30 Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho”.
Kwahiyo mimi na wewe tusiwe na sababu za kulaumu nyakati na majira tuliyopo..Ni wakati wa kuyafahamu majukumu yetu na kuyatimiza katika huu wakati mfupi tuliobakiwa nao hapa duniani. Ili na sisi tufanye vizuri zaidi kuliko wale, tupokee taji lililo bora. Hivyo tubadilishe hii mitazamo,
Mwisho Bwana atubariki sote, tuliozaliwa nyakati hii ya Laodikia.. Kwasababu tukishinda thawabu yetu ni kuwa kuliko za wengine wote..Kwasababu sisi tumeahidiwa kuketi pamoja na Mfalme mwenyewe (Bwana Yesu Kristo) katika kiti chake cha enzi, katika ufalme wake unaokuja, hakuna kanisa lingine lolote lililoahidiwa thawabu nono kama hii (kasome Ufunuo 3:21-22).. Hivyo Tukaze mwendo tusiikose.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
https://wingulamashahidi.org/sala-ya-baba-yetu-sala-ya-bwana/
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/11/nini-maana-ya-huu-mstari-usiseme-kwani-siku-za-kale-kupita-siku-hizi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.