JE KUPOKEA CHANJO NI DHAMBI?

by Admin | 16 September 2020 08:46 pm09

Kupokea chanjo ni dhambi kibiblia?

Chanjo ni “ugonjwa dhaifu” unaoingizwa ndani ya mwili wa mtu, ambao mwili una uwezo wa kuudhibiti, na hivyo kuuachia mwili kumbukumbu ya ugonjwa huo pindi utakapokuja tena katika ukamilifu wote siku za mbeleni.

Ili kuelewa zaidi tafakari mfano huu “Mfanya biashara mmoja aliyefanikiwa katika biashara zake, alikuwa akihifadhi fedha zake nyumbani, na nyumba yake hiyo haukuwa na uzio zaidi ya mlango wake mmoja tu wa kuingilia ndani. Siku moja wahalifu walimvamia usiku na kujaribu kuvunja mlango wake, lakini kutokana na kwamba mlango wake ule ulikuwa imara sana na wahalifu wale hawakuwa na zana za kutosha walishindwa kuuvunja mlango ule, wakaondoka…hivyo tukio lile lilimtafakarisha sana yule mfanya biashara, na hivyo akatafuta suluhisho ili tukio kama lile lisijirudie tena, kwamba wasije wahalifu wengine wenye nguvu kuliko wale wa kwanza na kufanikiwa kuvunja mlango na kumwibia na kumdhuru, hivyo kulizuia hilo, kulipopambazuka aliita mafundi wakatengeneza uzio mkubwa kuizunguka nyumba yake yote, na pamoja na hayo akaweka na mlinzi getini pamoja na mbwa”.

Sasa ukilitafakari tukio hilo utagundua kwamba…kwa lile tukio la kwanza lililomtokea la wezi wasio na nguvu za kutosha kujaribu kuvunja mlango wake ni kama limemfungua akili mfanya biashara yule na kugundua kuwa kumbe yupo katika hatari na hivyo anapaswa kujilinda zaidi.

Sasa katika ulimwengu wa sayansi ya tiba, hao wezi dhaifu ndio  wanafananishwa na “chanjo” wanapowekwa ndani ya mwili, lengo ni kuupa mwili taarifa za hatari iliyopo na hivyo kujitengenezea kinga madhubuti kwa hatari itakayokuja kutokea mbeleni iliyo mfano wa hiyo.

Kwahiyo matabibu (madaktari) wakati mtoto anapozaliwa, ili kumnusuru wanamweka mtoto chanjo hizo mbalimbali za magonjwa tofauti tofauti..lengo ni ili ule mwili wa mtoto upate taarifa na ujitengenezee kinga mapema kabla huo ugonjwa haujaja kwa nguvu siku za mbeleni. Sasa hilo ndio lengo la kwanza la Chanjo. Na kwa lengo hilo basi sio dhambi kumpa mtoto chanjo, au mtu kupokea chanjo.

Lakini pia sio lazima, kwasababu viwango vya Imani vinatofuatiana. Wapo wengine waliopewa neema ya kumwamini Mungu, na hivyo huweza kuishi bila hivyo vitu, na wasipatikane na madhara yoyote. Hao ni wachache, na wanafanya vizuri zaidi. Lakini pia sio wote wenye imani hiyo, kwahiyo nao pia sio dhambi wakipokea chanjo.

Warumi 14: 1  “Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.

2  Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga.

3  Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali”.

Hivyo sio dhambi kupokea chanjo!.Na hata kama unayo Imani ya kutokupokea hiyo, hupaswi kuwafanyia hivyo watoto wako, wala kuwahukumu wale wanaopokea…Ni vizuri ukawapeleka watoto wako kwenye chanjo, wewe baki na imani yako..watakapokuwa watu wazima watachagua..

Pia kuna jambo la kuzingatia. Sio kila chanjo ni lazima kupokea au kumpa mwanao, Zipo chanjo za msingi kabisa, ambazo zinajulikana katika mahospitalini, ambazo ni chache sana. Chanjo chache ni vizuri zaidi kwasababu anayetupa afya ni Mungu, na si wanadamu, KİLA KİTU TUNAPASWA TUKİFANYE KWA KİASİ. Na si kuweka tegemeo letu huko asilimia 100, kwamba ndio uhai wetu na ulinzi wetu upo huko. Tukiweka mategemeo yetu huko asilimia 100, hiyo ni dalili tosha kwamba hatuna Imani kwa Mungu hata kidogo. Jambo ambalo ni dhambi na linamtia Mungu wetu wivu na huzuni kwasababu hizo ni sawa na ibada za sanamu.

Hivyo kwa hitimisho: Kupokea Chanjo sio dhambi, wala kumpa mwanao chanjo sio dhambi…Wala kuipa mifugo yako chanjo sio dhambi. Isipokuwa inapaswa itumike kwa kiasi, kwa mimi nionavyo chanjo 3 zinatosha zikizidi sana 4. Mengine tumwamini Mungu atupaye afya na uzima, na atuponyaye. (Zaburi 107:20).

Na chanjo tunayoizungumzia hapa ni ile ya HOSPITALINI na si ya kwa waganga wa kienyeji. Chanjo za waganga wa kienyeji ambazo zinahusisha “kuchanjwa chale” ni za kishirikina, ambazo ni machukizo makubwa kwa Mungu wetu, hizo zinahusiana na ibada za sanamu na Mungu kazikataza..(Soma Walawi 19:28)

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je Kutoa Mimba ni dhambi?

Naomba kujua nini maana ya kuteguka uvungu wa paja?

Mkatale ni nini katika biblia? (Matendo 16:24)

NJIA MOJAWAPO YA KUPATA MSAADA KUTOKA KWA MUNGU.

NAYE HERI AWAYE YOTE ASIYECHUKIZWA NAMI.

Jabari ni nini, kama linavyotumika kwenye biblia?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/16/je-kupokea-chanjo-ni-dhambi/