YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

by Admin | 9 October 2020 08:46 pm10

Adui yetu shetani, usiku na mchana anatafuta kutumeza, kama biblia inavyosema katika..1Petro 5:8 “ Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, AKITAFUTA MTU AMMEZE”.

Hivyo anazo njia nyingi za kummeza mtu, na kila siku anabuni njia mpya…Lakini anayo moja maarufu anayoitumia ambayo ni ya MAWAZO.Anachofanya ni kupanda mbegu Fulani mbaya ndani ya mtu, ambayo hiyo mbegu inavyozidi kukuwa ndani yake inamletea kukata tamaa na mwisho kuanguka kabisa. Sasa yafuatayo ni baadhi ya Mawazo ambayo, ukiona yanakuja ndani yako, fahamu kuwa ni mawazo ambayo yamebuniwa na ibilisi, hivyo Yakatae na kuyapuuza.

  1. Mawazo ya kwamba Umemkufuru Roho Mtakatifu, au una dhambi isiyosameheka:

Hii ni silaha moja maarufu ya adui shetani kwa watu wa Mungu. Anayatengeneza mawazo haya ndani ya mtu, na kumfanya aishiwe nguvu ya kuendelea kumtafuta Mungu na kuwa na amani.

Hivyo wazo lolote linalokuja ndani yako kwamba tayari umemkufuru Roho Mtakatifu, kwasababu pengine ulishawahi kusema maneno Fulani wakati Fulani, kuikejeli injili. Au ulifanya dhambi Fulani kubwa sana, ambayo haielezeki, au ulirudi nyuma baada ya wokovu wako, na sasa unataka kutubu uanze upya, Ukiona hilo wazo linakuja ndani yako, kukuambia kuwa ulishamkufuru Roho Mtakatifu, Fahamu kuwa hilo ni wazo la ibilisi asilimia 100, hivyo lipuuzie usilipe nafasi hata kidogo. Hakuna mwanadamu aliyemkufuru Roho Mtakatifu na bado ana hofu ya Mungu..Lakini usipolipuuzia hili wazo na kuendelea kukaa nalo moyoni, litazidi kukua na mwishowe litakufanya usiendelee kumtafuta Mungu, na litakufanya uwe unakosa amani na furaha kila wakati.

  1. Mawazo ya kujiona kama Mungu anakuchukia:

Hii ni silaha nyingine ya shetani, kuharibu watu wa Mungu..Ukiona upo kwenye hili tatizo kwamba unaona kama Mungu anakuchukia, hakupendi anawapenda tu baadhi ya watu Fulani, au watumishi wake..Jua tayari upo katika shambulizi la adui yako shetani, tayari upo katika anga

zake anakuharibu kidogo kidogo. Fahamu kuwa Mungu hamchukii mtu yeyote yule hata yule mwovu kuliko wote, ingekuwa anakuchukia sidhani kama angekuumba uishi katika hii dunia, mpaka umejiona umetokea kwenye hii dunia, jua ni kwaajili ya upendo wake kwako. Hivyo hilo wazo la kujiona hupendwi ni kutoka kwa adui.

  1. Mawazo ya kujiona kwamba Mungu hasikii maombi yako:

Mungu anasikia maombi ya kila mwanadamu..kama kilio cha dhambi tu kinamfikia mbinguni, kwanini maombi yasimfikie?. Yanamfikia isipokuwa majibu ya maombi yanatofautiana mtu na mtu. Wapo ambao watapeleka maombi yao watajibiwa kama walivyoomba na wapo ambao hawatajibiwa, sasa wale ambao hawatajibiwa maombi yao, ipo sababu, na Mungu wa upendo atahakikisha wanaijua hiyo sababu kwa njia yeyote ile, ili warekebishe wapokee majibu ya maombi yao.. Kamwe hawezi kumwacha mtu yeyote hewani tu!, bila kumpa sababu ya kwanini hajapokea majibu ya maombi yake..Kinachowakwamisha wengi ni kukata tamaa

kirahisi…Unapokata tamaa tayari umekatisha safari yako ya kupokea baraka zako ukiwa katikati.

Kwa mfano, mtu anaweza kwenda kumwomba Mungu naomba unipe mume bora, au mke bora..lakini ukimwangalia ni kahaba, hivyo Mungu mwema hawezi kumpa kitu kizuri kabla hajamtengeneza kwanza…Kwahiyo wakati anasubiria majibu ya maombi yake, Mungu anamletea mhubiri, ambaye atamhubiria wokovu, na njia bora ya kuishi Maisha ya kumpendeza Mungu, anapotii na kukubali kubadilika na kuacha njia zake mbaya..Mungu ndipo anamletea jibu la

maombi yake aliyomwomba, analetewa mwenzi mwema wa Maisha, ambaye hatamsumbua na aliye mcha Mungu kama yeye. Lakini kama hatatii bado anataka kuendelea kukaa na ukahaba wake ndio atakaa hivyo hivyo kwa muda mrefu mpaka siku atakapofunguka akili, atarudia kuomba yale yale maneno lakini hataona majibu…

Hizo tu ndizo sababu za Mungu kuchelewesha majibu, lakini si kwamba Mungu hasikii maombi… Anayasikia, isipokuwa katika ujubuji wake ndio suala lingine.

Hivyo ukikosa kujiamini na kufikiri Mungu hajawahi kusikia maombi unayoomba chumbani kwako, au barabarani unapotembea, au kazini unapofanyia kazi…basi jua umeshambuliwa rohoni na adui shetani. Kazana kujua kwanini hujapata majibu lakini usifikiri kwamba hujasikiwa kabisa. Tayari umeshasikiwa, na uliloliomba limeshafanyiwa kazi, wewe fuatilia ombi lako lipo katika hatua gani sasa.

Marko 11:24 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu”.

  1. Mawazo ya kufikiri kwamba Siwezi kumpendeza Mungu wala kuwa mtakatifu:

Ndugu ukifikiri kwamba unaweza kufikia kiwango cha utakatifu kiasi kwamba huna kosa kabisa..basi fahamu kuwa hutaweza kamwe kumtumikia Mungu, kumbuka bado tunaishi duniani,

na lazima tutakuwa na kasoro nyingi, ambazo nyingi hatuzijui kama tunakosea…Sasa kama Mungu angezihesabu hizo biblia inasema hakuna mtu angesimama. Baada ya kuokoka ukiamka asubuhi usianze kukaa kuhesabu makosa yako, ukifanya hivyo kamwe hutaweza kumtumikia Mungu, na shetani atakusumbua sana na kila dakika atakuletea mawazo wewe ni mbaya, wewe hustahili, wewe hufai, wewe umeshamkosea Mungu, hufai, hufai n.k

Ukiamka asubuhi anza kuhesabu ni mazuri mangapi umemfanyia Mungu wako, na kama hujafanya kabisa ndipo uhuzunike, na tafuta kufanya, na jioni ukirudi..Mwambie Bwana asante kwa hichi kizuri ulichoniwezesha kukufanyia siku ya leo, na pia naomba nisamehe makosa yangu

yote niliyokukosea wewe pasipo kujua siku ya leo. Na kama unayakumbuka baadhi uliyoyafanya hakikisha kesho unayarekebisha, na ukishatubu tu usianze kujilaumu laumu!..Ukifanya hivyo utaruhusu mashambulizi ya shetani kukuvamia na kukuletea mawazo yale yale kwamba Mungu

alichukizwa na wewe jana, hivyo hawezi kuendelea kutembea na wewe leo…Kwahiyo siku zote Vaa ngao ya Imani, ili uweze kuizima hiyo mishale ya adui. Mungu wetu wa upendo hakai huko mbinguni na karatasi na kalamu akitiki mabaya tunayoyafanya baada ya sisi kuokoka…hafanyi hivyo, yeye yupo kutazama mema yetu, maadamu tumeshaokoka na

kumwamini na tumeweka mbali Maisha ya dhambi. Basi tunakuwa tunahesabiwa haki kwa Neema na si kwa matendo. Na hivyo kidogo kidogo anatutakasa mpaka unafika wakati tunakuwa wakamilifu kabisa kwake.

Hivyo hizo ni silaha 4 za adui yetu shetani. Sasa kama hizi Habari ni mpya kwako, na kama zimekufungua macho, basi ni dalili ya kwamba ulikuwa huna Ngao mkononi mwako, hivyo

ulimfungulia shetani nafasi ya kukushambulia ndio maana husongi mbele kiimani, na hiyo ni kutokana na kwamba pengine nafasi ya kutafuta kumjua Mungu Zaidi katika Maisha yako ni ndogo, au ulikuwa umesongwa na hivyo kulifahamu Neno imekuwa ngumu kwako, kwahiyo nakushauri mtu wa Mungu usiruhusu tena kusongwa..Neno hili wakristo wote waliofanikiwa ambao umeona wamesimama na hawapelekwi ni kwasababu, wana ngao za Imani mikononi

mwao, ni kwasababu Hivyo vipengele 4 hapo juu wamevishinda tangu zamani. Hivyo ni wewe peke yako umebaki.

Anza kumtafuta Mungu kwa bidii, anza kusoma Neno kwa bidii, usipitishe siku bila kushika biblia, na usomapo usisome kwa kutimiza wajibu, Ukilisoma Neno la Mungu na kulielewa ndivyo linavyokaa ndani yako, na linakupa Imani na maarifa, na ndivyo linavyokuweka huru, Ukilikosa hilo kamwe usitegemee kumshinda shetani, na wala kamwe usitegemee kama utaweza kumtumikia Mungu. Kwasababu shetani hawezi kuruhusu umtafute Mungu kirahisi rahisi hivyo, ni lazima akuletee hivyo vita vya kimawazo, akishinda hivyo atakuletea na vya nje, sasa ni wajibu wetu kufahamu kuwa tupo vitani. Ni lazima upambane kumjua Mungu.

Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

KWANINI LEO HII KUNA KUNDI KUBWA LA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA?

NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/09/yafuatayo-ni-mawazo-ya-adui-hivyo-usiyasikilize/