KUNA WAKATI YESU ATAPITA NA WATU HAWATAJUA.

by Admin | 20 October 2020 08:46 am10

Jina tukufu la Bwana wetu Yesu libarikiwe daima.

Karibu tuzidi  kujifunza maneno ya uzima, kwasababu tupo katika nyakati za ukongoni kweli kweli, hivyo ni wajibu wetu kuzidi kujua mambo yahusuyo  ukombozi wetu kwa umakini zaidi..

Neno letu la leo linatoka katika vifungu hivi;

Marko 9:30 “Wakatoka huko, WAKAPITA KATIKATI YA GALILAYA; NAYE HAKUTAKA MTU KUJUA.

31 KWA SABABU ALIKUWA AKIWAFUNDISHA WANAFUNZI WAKE, AKAWAAMBIA, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka”.

Katika maneno hayo swali kuu unaweza ukajiuliza ni hili, ni kwanini Yesu hakutana watu wamwone , alipokuwa akipita Galilaya, ikumbukwe kuwa mji huo alishauendea mara nyingi na akafanya miujiza mingi kupita kiasi, lakini inafika wakati huu tena kwanini asijidhihirishe awahubirie na kuwaponya makutano kama kawaida badala yake, anaupita mji huo huo kimya kimya tena kwa siri kubwa.

Ukisoma hapo utaona biblia inatupa sababu ya yeye kufanya vile, inatuambia ni kwasababu alikuwa anataka kuwafundisha wanafunzi wake, hilo tu…Hiyo inatupa kuijua tabia nyingine ya Bwana Yesu ambayo pengine tulikuwa hatuijui. Hata sasa, wapo atakaowafundisha kwa wazi, na wapo atakaowafundisha akiwa sirini na mtu mwingine yeyote hatajua,.

Wakati wote makutano walifundishwa kwa wazi, lakini wale aliowaita, kisha baadaye wakawa wanafunzi wake, aliwavusha daraja lingine la rohoni, akawa anawafundisha mambo mengine tofauti kabisa na yale makutano aliyokuwa anawafundisha.

Na  baadhi ya mambo yenyewe aliyowafundisha, kama tunavyosoma habari ni yale ambayo yatakwenda kutokea kipindi kifupi mbele yao, yaani juu ya kukamatwa kwa Yesu, mpaka kusulibiwa na kufufuka na kupaa. Walikuwa wanapewa siri za ukombozi wote wa mwanadamu kabla ya wakati wenyewe kufika..mambo ambayo makutano hawakuelezwa, wala kudokezewa hata kidogo.. Na waliambiwa mengine mengi zaidi ya hayo. Kwamfano hizi habari zote tunazozijua zihusuzo siku za mwisho, hawakuambiwa makutano, hapana bali hicho kilikuwa ni chakula walichopewa wanafunzi wake tu walipokuwa kule katika mlima wa mizeituni, (Mathayo 24, Marko 13, Luka 21:5).

Na ndio maana Bwana Yesu mahali pengine aliwaambia, niliyowaambia sirini, utafika wakati mtayasema hadharani, na ndio haya yanayotufaidia sisi..

Kwahiyo, hata sasa huu sio wakati wa kuzunguka huku na huko, kufurahia Yesu anaponya, Yesu anafufua, Yesu anabariki, hatupaswi kuwa kama makutano tu, waliomfuata Yesu, kwa ajili ya mikate na miujiza, na ishara, tunapaswa sasa tuingie gharama za kufanyika kuwa wanafunzi wake,(hicho ndicho anachokihitaji) kwasababu yapo mambo yahusuyo siri za Ufalme wa mbinguni, na Unyakuo tunapaswa tuyajue kwa wakati huu mfupi tuliobakiwa nao, na hatutayajua kama hatutakuwa wanafunzi kweli kweli wa Bwana Yesu.

Yesu ni yeye Yule jana na leo na hata  milele, tusidhani alipojificha kwa wale, hawezi kujificha na kwetu pia..Hivyo tusipumbazwe na kitu chochote, kwa maana sisi tukizembea, wapo wengine  wakati wetu huu huu wamekaa katika vyumba vya siri na Bwana Yesu wanafunuliwa mambo ambayo yanahusu wokovu wetu.

Tusikubali kuachwa nyuma na Yesu, tusikubali apite kwenye mitaa yetu, na kwenye makanisa yetu, na kwenye mikutano yetu kwa siri, Embu leo tujiachie na kufanyika kuwa wanafunzi wake kweli kweli.

Na tunafanya hivyo kwa kujitwika misalaba yetu, na kuuacha ulimwengu nyuma, na kumkaribisha ndani yetu, Na baada ya hapo, yeye mwenyewe atahusika, kutufundisha.

Tuzidi kukumbuka kuwa; Hii dunia ipo ukingoni sana, hatutashangaa hata unyakuo ukiwa ni usiku wa leo, kwasababu hakuna chochote ambacho hakijatimia, hivyo tukiyajua hayo hatutakuwa na muda tena wa kuichezea chezea neema ya wokovu. Yesu sio kama tunavyomfikiri, Sio kama tunavyomwaza vichwani mwetu, Yesu ni hekima ya Mungu na Nguvu ya Mungu yenyewe kama biblia inavyotuambia (1Wakorintho 1:24), tukifanyika kuwa wanafunzi wake kweli kweli, hatutabaki kama tulivyo.

Hivyo tuanze sasa kufanyika wanafunzi wa Bwana.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

NANGA YA ROHO, YENYE SALAMA.

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

JUKUMU LA MUHIMU LINALOKWEPWA NA WENGI.

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/20/kuna-wakati-yesu-atapita-na-watu-hawatajua/