Neno Bildi linamaanisha nini kwenye biblia(Matendo 27:28) ?

by Admin | 21 October 2020 08:46 pm10

Bildi ni kitu cha kupimia kina cha maji,Mara nyingi huwa ni kamba ambayo wanaifungia kitu kizito kwenye moja ya ncha zake, kisha wanakishusha kitu hicho kwenye maji, aidha  ya mto, au ya ziwa, au ya bahari. na moja kwa moja mpaka kwenye sakafu ya bahari. Kikishafika kule wanapima urefu wa kamba ile na hapo ndipo wanapojua bahari hiyo ina urefu wa kina gani.

Neno hilo utalipata, katika ile habari ya mtume Paulo alipokuwa akisafirishwa kama mfungwa kuelekea Rumi. Kama vile tunavyoijua habari, walipokuwa katikati ya safari yao bahari iliwachafukia sana, mpaka wakakata tamaa ya kuishi, wakakaa siku nyingi bila kuona jua wala nyota. Lakini kama baada ya siku 14 walifika mahali ambapo walihisi kama kuna nchi kavu mbele yao, hivyo ikabidi wajaribu habati yao kwa kupima kina cha maji sehemu mbili tofauti ili waone kama ni kweli kina ndio kinapungua au kinaongezeka..

Hapo ndipo wakatupa bildi hizo kwenye maji, walipotupa ya kwanza  ikapima urefu wa “pima” 20, (Pima moja ni sawa na futi 6), hivyo urefu wa kwanza ulikuwa ni futi 120.

Wakaenda mbele kidogo wakatupa bildi nyingine tena, wakapata pima 15 ambazo ni sawasawa na futi 90. Hapo ndipo walipogundua kuwa kina cha bahari kinapungua na kwamba wapo karibu na nchi kavu. Ikawabidi watie nanga, wasisogee popote tena mpaka kukuche.

Matendo 27:27 “Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu.

28 Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano.

29 Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche.”.

Hata sisi wakristo kila mmoja rohoni anapaswa awe na bildi ya kuipima safari yake akiwa hapa duniani.

Ni lazima tupime mienendo yetu, kila wakati, je namna ya maisha tunayoishi leo na jana tofauti yake ni nini?. Ikiwa hali ya maisha tunayoishi leo ndio inatufanya tuende mbali zaidi na Mungu, tupoe kiroho kuliko ilivyokuwa hapo jana..Hapo tunapaswa tuchukue maamuzi ya haraka sana ya kubadili mfumo wa maisha yetu, ili tusiendelee mbele kwenye madhara zaidi. Tukapotea moja kwa moja.

Lakini kama tutaishi maisha ambayo kila siku yanatutupa mbali na Mungu na bado tunaona ni sawa tu, tunaruhusu  yaendelee hivyo hivyo , tujue kuwa mwisho wetu utakuwa ni mbaya sana.

Swali ni je mara ya mwisho kuishusha bildi yako ni lini?

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Shokoa ni nini katika biblia?

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Mkomamanga ni nini? Na katika biblia unawakilisha nini?

Mavyaa ni nani kibiblia?(Mika 7:6)

LAKINI USIKU WA MANANE, PAKAWA NA KELELE.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/21/neno-bildi-linamaanisha-nini-kwenye-bibliamatendo-2728/