SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

by Admin | 6 November 2020 08:46 pm11

Sala ya Uponyaji/Maombi ya uponyaji


Nakusalimu katika jina  la Bwana Yesu Kristo.

Kusudi lingine kuu tukiachilia mbali lile la wokovu wa roho zetu ambalo lilimfanya  Bwana Yesu aache enzi na mamlaka na ukuu kule mbinguni ashuke duniani, lilikuwa ni kutuponya na miili yetu pia.

Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa”,

Mathayo 8: 17 “Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu”.

Isaya 53:4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu;..”

Ni Yesu peke yake, ndiye mwenye uwezo wa kuyaondoa magonjwa yetu yote moja kwa moja, hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo, na ndio maana tunamtumaini yeye. Na ni mapenzi yake kuwa sisi tuponywe(Soma Mathayo 8:2-3). Inawezekana wewe unayeusoma ujumbe huu, upo katika hali mbaya wakati huu, inawezekana upo mahutihuti hospitalini,au umekuwa ukisumbuliwa na huo ugonjwa kwa muda mrefu, umejaribu kwenda huko na kule bila kupata mafanikio yoyote, umepoteza fedha nyingi kwa ajili ya matibabu lakini hakuna matumaini yoyote. Pengine hata ulishahudhuria katika nyumba za maombi lakini bado hali yako ipo palepale, nataka nikuambie usivunjike moyo, hilo bado halimfanyi Yesu asikuponye ugonjwa wako.

Inawezekana unao ugonjwa wa siri, na unaogopa hata kuwaeleza watu, inawezekana umepata ugonjwa usioponyeka,  Umepata Ukimwi, au Kansa, au Kisukari, n.k. Nataka nikuambie hayo yote si kitu kwa Bwana Yesu.

Kama Yesu alifanya  muujiza wa kuuponya mwili wa mtu ambaye alikuwa ameshakufa kwa ugonjwa mbaya sana(Lazaro) na mwili wake ulikuwa tayari umeshaanza kutoa mafunza kaburini, lakini akauridisha na ukiwa mzima bila shida yoyote.. Si zaidi wewe ambaye bado hata hujafa, bado hata mwili wako hujaanza kutoa mafunza? Atakuponya.

Anachotaka kwako ni kuamini tu! Basi.

Na imani inakuja kwa kusikia, hicho ndicho chanzo cha Imani, (Warumi 10:17)  Unapolisoma Neno lake, imani inajengeka, unasoma shuhuda mbalimbali za jinsi Bwana alivyowaponya watu katika maandiko ndipo imani yako kwake inavyojengeka, na kuwa kubwa zaidi,

Unaweza kufungua masomo haya, na shuhuda hizi mbili tatu, zitakusaidia kuiimarisha imani yako;

Zaburi 107:19 “Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao”.

Sala ya Uponyaji/Maombi ya uponyaji

Lipo kusudi la Mungu kukufikisha katika ukurasa huu kwa wakati huu; Kwa baada ya maombi haya mafupi ambayo tutakwenda kuomba pamoja amini kuwa kuna tendo linakwenda kutendeka ndani yako kuanzia huu wakati;

Tunapokwenda kuomba pamoja nataka mahali ulipo, weka mkono wako katika eneo la ugonjwa lilipo. Kisha zungumza maneno haya:

Bwana Yesu, wewe ni mponyaji wangu. Ulisema unalituma Neno lako ili uniponye(Zab 107:20).. Na pia ulisema Neno lako li hai tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga wowote ukatao kuwili (Waebr 4:12). Hivyo Bwana Yesu mponyaji wangu, naomba sasa ulitume Neno lako ndani ya mwili wangu likafanye uponyaji. Likaondoe magonjwa yote haya yanayonisumbua (yataje). Likakate kate kazi zote za ibilisi zilizopangwa ndani ya mwili wangu. Nikawe mzima kabisa sawasawa na maneno yako uliyosema katika Yeremia 30:17 ..kwamba utanirejesha afya yangu na kuniponya jeraha zangu. Naiita afya yangu sasa sawasawa na ahadi zako kwa jina la Yesu Kristo, nauita uzima wangu kwa jina la Yesu Kristo.

Asante Mungu wangu kwa upendo wako, na kwa  uponyaji wako. Amen.

Basi ikiwa umeomba sala hiyo fupi: Hapo hapo na mimi nitakwenda kukuombea.

Ee Mungu baba, nakushukuru kwa mwanao huyu ambaye ameona msaada pekee, unatoka kwako na si kwa mtu mwingine yeyote. Baba nakuomba ikiwa ametenda dhambi  iliyomstahili ugonjwa huo nakuomba Mungu wangu umsamehe, ikiwa amepata ugonjwa huo kwa nguvu za giza basi leo natangaza mwisho wake, kwa Jina la Yesu Kristo. Naomba kama mtumishi wako, umpe afya yake, ili akajue kuwa hakuna mwingine awazaye kutuokoa sisi isipokuwa wewe YEHOVA, na kwa kupitia ushuhuda huo akapate kwenda kulitangaza jina lako kuu kwa mataifa. Asante kwa uponyaji huo ambao tayari umeshaanza kuingia katika mwili wake. Amen.

Sasa kama nilivyosema, zidi kuamini kuwa tayari Kristo amekuponya. Lakini pia ikiwa bado hujaokoka, (Yaani bado hujampa Yesu Kristo maisha yako) Ni vema ukafanya hivyo sasa. Kwasababu hali nyingine haziwezi kuondoka ndani ya mtu, kama mtu mwenyewe hajaamua kukubaliana na Yule anayekwenda kumponya.

Kumbuka wokovu wa roho yako ni bora zaidi kuliko huo wa mwili wako. Ukiponywa mwili, halafu roho ikaangamia faida yake ni nini? Lakini vikiponywa vyote ni faida jumla jumla. Tukizingatia kuwa hizi ni siku za mwisho na Yesu yupo mlangoni kurudi. Hatuna muda tena kwa kuvumiliana na shetani nyakati hizi za hatari, Hivyo bila kuchelewa, fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba ya kupewa maelekezo mengine >>>>  SALA YA TOBA

Bwana akubariki sana.

Kama utahitaji maombezi zaidi, basi wasiliana nasi kwa namba hizi bure, +255 693036618/ +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/06/sala-ya-uponyaji-maombi-ya-uponyaji/