by Admin | 24 November 2020 08:46 am11
Choyo ni nini kibiblia?
Choyo ni tamaa ya hali ya juu, aidha wa mali, uongozi, au chakula, ambayo inaambatana na uchoyo. Kwa namna nyingine ni Tabia ya ubinafsi, tabia ya umimi. Kukataa kwa makusudi kuwapa wengine kile ulichonacho, au wanachostahili kukipata, kwa maslahi yako mwenyewe.
Mithali 21:26 “Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi”.
Jambo ambalo Bwana Yesu alituonya sana tujiepushe nalo, alilizungumza hilo siku ile alipokutana na yule mtu ambaye alimwomba amwonye ndugu yake, juu ya urithi wao. Pengine ni urithi walioachiwa na baba yao alipokufa na huyu ndugu yao mmoja anataka kuwadhulumu hataki kuwapa, au ni mashamba ya ukoo, na hivyo anataka ayamiliki yeye mwenyewe, au ayauze na ndugu zake wasipate kitu n.k.. Vyovyote vile, lakini Bwana Yesu alimwambia hivi,
Luka 12:13 “Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.
14 Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?
15 Akawaambia, ANGALIENI, JILINDENI NA CHOYO, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.
16 Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;
17 akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.
18 Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.
19 Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.
20 Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?
21 Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”.
Tabia hii ya Choyo ilitabiriwa kukithiri sana katika siku za mwisho,(Ambazo ndio hizi tunazoishi) kuwa watu watakuwa ni wa kupenda fedha, na wa kujipenda wao wenyewe.(2Timotheo 3:2). Jambo ambalo ni baya sana.
Hivyo, na sisi tunapaswa tujichunguze kama tabia hii ipo ndani yetu, Kristo ameshatuasa tujiepusha nayo, tuache ubinafsi, bali tuwe watu wa kuridhika, na watu wa kushea na wengine vile ambavyo Mungu anatubarikia navyo, kwasababu vya duniani vinapita, hatukuja na kitu na wala hatutaondoka na kitu.
Zaburi 10:3 “Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/24/choyo-ni-nini-kibiblia-luka-1215-zaburi-103/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.