KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

by Admin | 30 December 2020 08:46 am12

Shalom, biblia inasema..

Yohana 3:29 “Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi;..”

Huu ni wakati wa kupigania kwa bidii kuwa bibi arusi wa Kristo kwelikweli, kwasababu kama ukifa leo hii na sio bibi-arusi au unyakuo umekukuta na bado hujafanyika kuwa bibi arusi ujue kuwa unyakuo hautakuhusu hata kidogo, haijalishi utasema mimi ni mkristo wa miaka mingi, hutakwenda popote. kumbuka si wakristo wote ni bibi-arusi, jambo ambalo wengi wetu hatulijui, Wakati huu wa mwisho maandiko yanatuonyesha wazi kuwa kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu wanaojiita wakristo.

Na hao wamezungumziwa kwa marefu sana katika kile kitabu cha Mathayo 25, kama wanawali werevu na wapumbavu.  Hao kwa jina lingine ndio wanaojulikana kama bibi arusi na masuria. Suria ni mwanamke aliyetwaliwa tu na kuwekwa ndani, hana mkataba wala urithi wowote kwa mume wake, isipokuwa kupewa tu zawadi na kuondoka,  lakini bibi arusi yeye ni mke, ambaye si tu kupokea zawadi, na urithi, kutoka kwa mume wake, bali pia anakuwa na kitu kingine cha zaida, ambacho leo tutajifunza kwasababu ndio kiini cha somo letu la leo.

Na kitu chenyewe ni “Kufahamu ya sirini ya Bwana wake”. Kama vile tunavyojua mtu pekee anayeweza kumfahamu mtu ndani nje, ni mke wa mtu, au mume wa mtu. Kwasababu watu hawa walishaunganishwa na kuwa mwili mmoja, hivyo usishangae kuona mke au mume anajua mambo mengi ya mwenzi wake kuliko hata ndugu zake alioishi nao kwa miaka mingi tangu utotoni.

Ndivyo ilivyo katika wakati huu wa mwisho. Bwana Yesu analiandaa kundi lake dogo sana, ambalo linajulikana kama bibi-arusi, kumbuka hili sio suria, yaani sio watu tu wanaojiita ni wakristo lakini wanaishi maisha yao ya kidunia wanayoyajua wao, hapana bali ni kundi lingine kabisa. Ambalo tutaona tabia zake kidogo mbeleni.

Sasa Watu hawa ndio Kristo atakaowafunulia  baadhi ya siri ambazo si watu wote watazifahamu. Kwasababu  Biblia inatabiri wakati dunia inakwenda kukaribia kuisha, zipo siri ambazo Mungu alizihifadhi wala hakutaka ziandikwe kwa wazi kwenye biblia, siri hizo atakuja kuwafunulia watu wake.

Ufunuo 10:4 “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, YATIE MUHURI MANENO HAYO YALIYONENWA NA HIZO NGURUMO SABA, USIYAANDIKE”.

Kama tunavyosoma hapo, yapo maneno ambayo yalitiwa muhuri, lakini hayakuandikwa.. Yalisikiwa tangu zamani lakini hayakuandikwa. Unaweza ukajiuliza ni kwanini yasiandikwe kama tayari yalishasikiwa? Ni kwasababu sio kila jambo ni la kila mtu. Mengine ni ya siri, ya Kristo na bibi arusi wake tu.

Na siku hizo ambazo siri hizi zitakapomalizika kuachiliwa mioyoni mwa kundi hili dogo la watakatifu, ujue kuwa tayari mstari wa neema umeshavukwa, na makundi mawili yameshajinga.

Hivyo Wakati huu tunaoishi,ni wa kumaanisha sana ndugu yangu, kwasababu ukijidanganya mwenyewe umeokoka, na huku nyuma unafanya matendo yako maovu sirini, kwa kisingizio wewe ni mchungaji, au mwalimu, au mwana kwaya, au nabii n.k…ukweli ni kwamba unajidanganya tu mwenyewe, wala usipoteze  muda wako mwingi kujisiri sitiri. Kwasababu Kristo anawajua walio wake, anamjua bibi arusi wake wa kweli yupoje, tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Hana mzaha mzaha katika kuchagua.

Na tabia inayomtambulisha Bibi arusi wa kweli ni mataendo yake ya haki (yaani utakatifu). basi

Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; KWA MAANA KITANI NZURI HIYO NI MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.

Je! Na wewe utakatifu upo ndani yako?. Kama jibu ni hapana, basi anza kutengeneza taa yako sawasawa iwe na mafuta ya kutosha,. Kwasababu Bwana arusi wetu Kristo yupo mlangoni kuja kulinyakua kanisa lake. Na hakuna anayejua itakuwa ni lini, lakini kila dalili inatuonyesha ni hivi karibuni pengine ni leo usiku. Hivyo usiishi maisha ya kubahatisha. Maanisha kweli kumfauta Yesu.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/12/30/kwanini-unapaswa-uwe-bibi-arusi-nyakati-hizi-za-majeruhi/