“Kinga kilichotolewa motoni “Kinafunua nini kibiblia?

by Admin | 28 January 2021 08:46 pm01

SWALI: Kwanini Yoshua aliambiwa yeye ni kinga kilichotolewa motoni? Hichi kinga kilichotolewa motoni kina maana gani kibiblia?


JIBU: Kinga ni kama kijiti, hivyo inaposema kinga cha moto inamaanisha kijiti cha moto. Neno hilo utaliona sehemu kadha wa kadha katika biblia, na hususani wakati ule, Yoshua kuhani mkuu alipokuwa amesimama mbele za Mungu, na shetani naye amesimama pembeni yake kumshitaki, Lakini yule malaika aliyekuwa amesimama pembeni yake, aliyazungumza maneno haya;

Zekaria 3:1 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.
2 Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; JE! HIKI SI KINGA KILICHOTOLEWA MOTONI?
3 Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika.
4 Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi”.

Sasa ukisoma kwa ukaribu maneno hayo, utaona sio Yoshua anaambiwa yeye ni kinga kilichotolewa motoni, bali ni Yerusalemu ndio inayofananishwa na kinga kilichotolewa motoni.

Kama tunavyojua kipande chochote cha mbao kikiingia kwenye moto, huwa hakina namna ni lazima kiteketee tu, tofauti na vitu vingine kama chuma. Sasa kama kimetolewa motoni, inamaanisha kimenyakuliwa kutoka katika uharibifu uliokuwa unakila.

Hivyo Malaika wa Mungu alikuwa anamwambia shetani, kuwa Yerusalemu, ambayo Mungu alikuwa ameiteketeza ili ipotee kabisa milele, sasa ameihurumia na kuiokoa tena imsimamishie nyumba, na Yoshua huyu aliyesimama hapa ndiye atakuwa kuhani mkuu katika nyumba itakayojengwa Yerusalemu.

Israeli tangu ilipoasi Mungu  aliiweka katika  moto wa mfalme wa Babeli Nebukadreza, ili aingamize kabisa, Na ndio maana ukisoma Yeremia 29: 22 Utaona Mungu anatoa unabii kwa wale manabii wa uongo waliokuwa wanaitabiria Israeli habari za amani wakati hakuna amani, na kuwaambia kwamba huyu mfalme wa Babeli ndio atakuwa wa kwanza kuwaoka, hawa manabii katika moto.

Yeremia 29:22 “Tena katika habari zao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, kusema, Bwana akufanye uwe kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni”

Neno hilo utaliona tena, sehemu nyingine  kwenye biblia ambapo Mungu aliiadhibu Israeli kwa mapigo ya kila namna, mfano wa Sodoma na Gomora, aliitia katika moto wa uharibifu, lakini baadhi yao aliowapa neema ya kuokoka hawakutambua kuwa wamenyakuliwa katika moto, kama vinga vilivyokuwa vinateketea, bali waliendelea kutenda maovu..

Amosi 4:7 “Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika.
8 Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.
9 Nami nimewapiga kwa ukavu na koga; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.
10 Nimewapelekea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa matuo yenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

11 Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo MUNGU ALIPOIANGAMIZA SODOMA NA GOMORA, NANYI MKAWA KAMA KINGA KILICHONYAKULIWA MOTONI; LAKINI HAMKUNIRUDIA MIMI, ASEMA BWANA.

Soma pia Isaya 7:4

Hata sasa, dunia inapopitia katika majanga mengi ya maafa, lakini tukijiangalia sisi bado tupo hai, tujue kuwa ni Mungu anatutaka sisi tutubu, kama sio kwenda kumtumikia kama iliyokuwa kwa Yoshua.

Tunapoepushwa na matetemeko ya ardhi, vimbunga, magonjwa makali ya kuua kama hili la CORONA, tujue kuwa ni vinga vilivyo nyakuliwa motoni, tunapaswa tujue huu ni wakati wa kutubu na kumrudia Mungu wetu kwasababu ulimwengu upo motoni.

Lakini tukipuuzia tukajiona kama sisi ni wa kipekee sana, tujue kuwa tutakutana na adhabu kali Zaidi ya hizi tulizonazo sasa hivi. Mungu ni moto ulao.

Tuyatambue makosa yetu tumrudie Mungu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

 

 

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

Nini maana ya uvuvio?.

Kuwatema farasi, maana yake ni nini?

UFUNUO: Mlango wa 15

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/28/kinga-kilichotolewa-motoni-kinafunua-nini-kibiblia/