THAWABU YA UAMINIFU.

by Admin | 8 February 2021 08:46 pm02

Kwa kawaida Mungu huwa hatoi karama zake zote kwa mkupuo, bali huwa anakupa kwanza kidogo kisha anaupima auminifu wako au uadilifu wako katika hicho, kisha akishaona umekithaminisha ndipo baadaye anakumwagia vyote vilivyobakia kwa wingi.

Leo tutaitazama mifano miwili ya watu walioambiwa maneno hayo naamini kwa kuisoma itakuongeza nguvu katika eneo hili la uaminifu,, wa kwanza tutauona kutoka katika maandiko na wa pili katika shuhuda za watu walitutangulia kwenye Imani.

Katika biblia, tunaona mtu mmoja aliyeitwa Yoshua, kuhani mkuu, ambaye Mungu alimwambia maneno haya;

Zekaria 3:6 “Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yoshua, akisema,

7 Bwana wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, NAMI NITAKUPA NAFASI YA KUNIKARIBIA KATI YAO WASIMAMAO KARIBU”.

Huyu Yoshua alichaguliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu wakati ule ambapo wana wa Israeli wanaondolewa tena Babeli, kumbuka huyu si yule Yoshua aliyewavusha wana wa Israeli Yordani, kutoka jangawani hapana, bali ni mwingine kabisa.

Sasa wakati akiwa Yerusalemu, Mungu akamchagua na kumtakasa, akamtia mafuta, awe kuhani wake, kuwapatanisha wayahudi wote.. Lakini tunasoma ahadi nyingine hakuzipokea palepale, bali zilitegemea kwanza uaminifu wake, ndipo Mungu ampatie ahadi hizo baadaye..

Mungu alimwahidi kuwa ikiwa atakuwa mwaminifu, ndipo ataihukumu nyumba yake, na vilevile atampa nafasi ya kumkaribia yeye, kati ya hao wasimamao karibu yake. Ulishawahi kujiuliza ni wakina nani hao wasimamao karibu na Mungu?.. Hapa duniani sio watu wote watakuja kusimama karibu na Mungu tutakapofika kule ng’ambo hata kama watakuwa wameokoka.

Ni sawa na leo hii, si watu wote wanaweza kusimama karibu na raisi wa nchi, kama hawajaalikwa na yeye, au kama hawana nafasi yoyote au cheo chochote katika serikali. Utagundua ni mawaziri tu, na watu wakubwa wakubwa wa serikalini, au familia yake tu ndio wanaoweza kumkaribia yeye. Lakini wengine wote mtakuwa mkimtazama kwenye Tv, au majukwaani.

Na vivyo hivyo kwa Mungu, wapo watu tayari ambao wameshawekwa karibu na Mungu,kutokana na uaminifu wao wa juu walipokuwa hapa duniani, katika maandiko tunawafahamu baadhi, wa kwanza ni Ibrahimu,

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;”

Wengine wakiwemo, akina Musa na Eliya, Wakina Danieli, watu waliopendwa na Mungu, wengine ni Ayubu, Samweli, akina Daudi aliyeupendeza moyo wa Mungu, Henoko, Mitume 12 wa Yesu, ambao Bwana aliwaahidia wataketi katika viti 12 wakiyahukumu makabila 12 ya Israeli, Yohana mbatizaji ambaye katika uzao wa wanawake hakuna aliyewahi kuwa mkuu Zaidi yake, wengine ni kama Mtume Paulo ambaye alitenda kazi kuliko wakristo wote wa wakati ule. Na pia wale mashahidi wawili ambao tunawasoma katika  ufunuo ambao wanafananishwa na ile mizeituni miwili,N.k.

Ufunuo 11:4 “Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi”.

Sasa hawa wote, ni watu ambapo wanasimama karibu sana na Mungu.. Hivyo Yoshua naye kama kuhani mkuu aliahidiwa ofa hiyo, kwamba kama akiwa mwaminifu, na yeye pia ataingizwa katika kundi  hilo dogo la watu watakaosimama karibu na Mungu, tengeneza picha unasimama karibu na Mungu muumba wa Mbingu na nchi na malaika..si jambo dogo hilo. Na sisi pia tutamani nafasi hizo.

Vivyo hivyo, leo tutamtazama mtu mwingine ambaye alitokea katika kizazi chetu aliyeitwa WILLIAM BRANHAM.

Ikiwa hujawahi kumfahamu mtu huyu, ushuhuda wake ulikuwa ni wa kipekee sana, hatuwezi eleza habari yake yote hapa,  lakini, kwa ufupi ni kuwa alizaliwa mwaka 1909, huko Marekani, katika familia ya kimaskini sana, elimu yake iliishia darasa la saba tu, lakini tangu akiwa mdogo Mungu alianza kumuonyesha maono mengi, ambayo mengine hakujua tafsiri yake ni nini, mengine aliyaona yakitimia muda mfupi baadaye,..Lakini alipokuwa mtu mzima, akiwa kama mchungaji wa kanisa dogo la kibaptisti baada ya kupitia shida nyingi, ikiwemo kufiwa na mke na mtoto wake, hakuacha kumtafuta Mungu kwa bidii.

Siku moja usiku wakati anasali kama saa 9 hivi, kumuuliza Mungu ni nini maana kusudi lake duniani, alitembelewa na Malaika wa Bwana, akamwambia, nimetumwa kutoka uweponi mwa Mungu, kukuambiwa kuwa maisha yako ya kutokueleweka, ni kukuonyesha kuwa Mungu amekuchagua kulibeba kusudi lake kwa watu..Akaambiwa atapewa karama ya uponyaji, na kama akiwa mwaminifu utafika wakati utakuwa na uwezo wa kujua hata siri za mioyo ya watu, na hukuna ugonjwa wowote utakaoisimama mbele yako hata saratani yenyewe..(Kwa kipindi hicho ugonjwa wa saratani ndio uliokuwa tishio duniani)

Ni kweli mtu huyu baada ya hapo alionyesha uaminifu wake kwa Mungu, na yote aliyoahidiwa yalikuja kutimia muda mfupi sana katika huduma yake .. alianza kufahamu siri za mioyo ya watu, wote waliosimama mbele yake katika mstari kuombwa, Na Zaidi ya hayo Mungu akamzidishia na ishara za ajabu, ilifikia wakati nguzo ya Moto ilitokea na kutua Juu yake, mbele ya kanisa akiwa anahubiri, na ikapigwa picha na kuwekwa katika makumbusho za kihistoria huko Marekani, baada ya kuthibitishwa na FBI, kuwa picha hiyo ni ya kimiujiza, ndio hiyo hapo unayoina katika katika ujumbe huu.

Si hilo tu wakati Fulani akiwa anawabatiza watu katika mto mmoja huko Marekani mwaka 1933, ghafla kulitokea nuru kubwa kama nyota na kutua juu yake, watu wote waliokuwepo pale waliiona, habari hizo zilishapishwa katika magazeti mengi maarufu huko Marekani..Na wakati alipokuwa akiwabatiza watu anasema alisikia sauti ikimwambia kama vile Yohana mbatizaji alivyotumwa kutangulia kuja kwa kwanza kwa Kristo, vivyo hivyo na ujumbe wako utatangulia kuja kwa pili kwa Kristo.

William Branham mpaka sasa, ni mwinjilisti ambaye wanazuoni na wanatheolojia wa dini wanamkumbuka kwa ishara na maajabu yaliyokuwa yanafuata naye katika huduma yake. Ya kuhubiri injili ulimwenguni kote.

Ikiwa utapenda kupata historia yake ndefu..tutumie ujumbe inbox ..

Lakini hiyo yote ni kutokana na uaminifu aliokuwa nao kwa Bwana.. Hakuhubiri udhehebu, kinyume chake, aliikemea roho za kidhehebu ambazo zinawafunga wakristo wasimtambue Mungu, na hiyo ikampelekea kuchukiwa sana na watu wa dini. Injili yake iliegemea katika kuwaelekeza watu kwa Yesu, na sio kwake, au kwa mtu Fulani, alikemea dhambi, hususani katika uvaaji mbaya wa wanawake.. Na matokeo yake Bwana akamtukuza na yeye. Mafundisho yake yaliegemea katika Misingi ya Neno tu.

Hivyo Ujumbe wake umekuwa kama MBIU kwa kanisa la mwisho la Laodikia ambalo ndio sisi tunaoishi, kwamba tutoke huko kwenye Kamba za udini na udhehebu tumwabudu Mungu katika Roho na Kweli.William ni mjumbe wa kanisa la letu la Laodikia.

Sasa kwa mifano hiyo miwili ,nataka  uone ni jinsi gani, Mungu anauthamini uaminifu wa mtu. Hata Musa kule jangwani aliuthamini kwanza muujiza wa kijiti kuteketea moto, ndipo Mungu akampa na mingine kikubwa Zaidi.  Kila mmoja wetu anapaswa awe mwaminifu katika kitu alichopewa na Mungu. Leo hii utaona Mungu kampa mchungaji kanisa, na kwa neema zake limeanza kukua kidogo, lakini itapita miaka miwili, mitatu, utasikia amefumaniwa katika uzinzi, mwingine amejilimbikizia mali zote za kanisa.. huko ni kukosa uaminifu kwa kile ulichopewa na Mungu.

Mungu anaweza kukupa karama Fulani katika kanisa, lakini baada ya kipindi Fulani unaanza kujiona wewe ni wewe, unaanza kuonyesha kiburi, huko ni kukosa uaminifu kwa kile kidogo ulichopewa. Unabadilika kama Yeroboamu unasahau kuwa ni Mungu ndiye aliyekupa,.. Kila mmoja wetu alieyokoka, kuna kitu Mungu amempa lakini tukishindwa kuwa waamifu navyo, tukavidharau, tukawa hatuvitendei kazi, kamwe tusitazamie kuwa Mungu atakaa atupe ahadi nyingine za juu zaidi ambazo alikuwa amekusudia kutupa.

Hivyo kuanzia leo mimi na wewe tuanze kujenga uaminifu kwa vile vichache Bwana alivyotupa.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HISTORIA YA WILLIAM BRANHAM

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

UFUNUO: Mlango wa 19

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/02/08/thawabu-ya-uaminifu/