by Admin | 11 February 2021 08:46 pm02
Isaya, alionyeshwa maono mengine ya ajabu mbinguni, Pengine hakuelewa umuhimu na maana ya maono yale, lakini sisi wa leo ndio tunaweza kuelewa vizuri.. Alipochukuliwa katika maono mbinguni alimwona Mungu akiwa ameketi katika kiti chake cha enzi kilichonyanyuliwa juu sana, juu kweli kweli. Na moja ya vitu ambavyo vilishangaza macho yake, ni kuhusu lile vazi lake, kwani lilipofika chini, halikuishia palepale bali liliendelea kumwagika, mpaka kufunika hekalu zima juu mbinguni.
Maono hayo aliyoonyeshwa Isaya yalichukua picha ya ufalme wa kidunia, hususani kwenye zile ngome kubwa sana, kama vile Ashuru na Misri zilizokuwa zinaitikisa dunia wakati ule wa nabii Isaya. Wafalme wao walivaa mavazi ambayo yalimwagika kwa nyuma, kuashiria utukufu wa enzi zao, hivyo yalikuwa yakisogea umbali kadhaa tu. tazama mfano wa picha juu.
Lakini vazi hili aliloonyeshwa Isaya lilikuwa ni la kipekee sana, lenyewe lililijaza Hekalu zima mbinguni, kuonyesha utukufu wake ni Zaidi sana ya ule utukufu wa mavazi ya kidunia aliyoyazoea.
Isaya 6:1 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, NA PINDO ZA VAZI LAKE ZIKALIJAZA HEKALU.
2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake”.
Sasa, Isaya alionyeshwa tu katika lugha ya picha, lakini sisi tunaoishi agano jipya tunajua maana halisi ya Pindo la vazi la Mungu ni nini, na lina umuhimu gani kwetu. Mtu wa kwanza aliyelitambua hilo ni yule mwanamke aliyetokwa na damu kwa muda wa miaka 12 bila kupata tiba yoyote. Lakini siku alipokwenda kuligusa pindo la vazi la Yesu, alijua lilibeba ufunuo gani, japo alilipata kwa shida sana kwasababu halikuwa refu, na umati mkubwa wa watu ulikuwa unamsonga lakini alipobahatika kugusa tu, muda ule ule ugonjwa wake sugu, uliisha.
Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.
21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.
22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile”.
Mpaka baadaye watu wengi, walipoligundua hilo, kumbe hata katika pindo tu la vazi lake kuna uponyaji, na sio lazima upate vazi lake zima..wakawakusanyana makutano mengi, wakawa wanaomba Bwana akipita angalau awaruhusu watu wale waliguse pindo la vazi lake, wapone.. Na wote waliogusa kweli waliponywa..
Marko 6:56 “Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona”.
Ni nini Bwana alikuwa anawaonyesha?
Sasa kwa kipindi Yesu alipokuwa duniani, vazi lake lilikuwa ni la kawaida tu, haliburuzi kwasababu alikuwa hajawa bado mfalme, lakini sasa anaketi kama MFALME MKUU huko mbinguni, na kama tunavyojua wafalme wenye nguvu sana ni lazima wavae mavazi ambayo pindo zake zinaburuza chini,walau kwa mita kadhaa.
Lakini Isaya anaonywesha maono, ya Kristo akiwa kwenye kiti chake cha Enzi, na vazi lake halipo pale tu alipo, bali limeburuza mpaka kufikia hatua ya kulijaza hekalu zima. Haleluya..
Na kama tunavyojua HEKALU la Kristo ni Kanisa lake, yaani mimi na wewe.
1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu”?
Hiyo ni kuonyesha kuwa Kristo anaponya kweli kweli, na uponyaji wake sasa, si kama ule wa zamani, ambapo alikuwa bado hajaketi kama Mfalme mwenye vazi refu,.. Lakini Kama tu alivyokuwa duniani aliponya kwa namna isiyokuwa ya kawaida vile, vipi wakati huu ambapo, uponyaji wake umesambaa katika kanisa lake lote, mahali popote, sehemu yoyote, wakati wowote..Mwite tu Kristo atakuponya. Kama unao ugonjwa unakusumbua, mwite Kristo atakuponya hapo ulipo. Kwasasa huhitaji nabii Fulani, au mtume Fulani, au mchungaji Fulani, au mwalimu Fulani akuombee, wewe mwenyewe ulipo vazi lake, linakufikia ukiwa hapo chumbani kwako unamwomba..Vazi hilo limefika kwako.
Vilevile, ataiponya na Roho yako, ikiwa tu utamwita kwa moyo wa kweli wa kumaanisha. Kristo amemwaga utukufu wake kweli kweli, usiruhusu neema ya wokovu ikupite hivi hivi, kwasababu upo wakati atasimama katika kiti chake che enzi, na neema itakuwa imekwisha kabisa.. bali atasimama kuhukumu.
Je!, unatambua hilo? Unatambua kuwa kanisa tunaloishi ndio kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia? Na kwamba hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili kulingana na maandiko katika kitabu cha Ufunuo 1-3. Unasubiri nini mpaka neema ikupite, ukifa leo huko utakapokwenda utakuwa mgeni wa nani, mambo ya dunia ndio unayoyahangaikia lakini mambo ya ufalme wa mbinguni, umeyatupilia kando, hujui kuwa ndio shetani anavyotaka uendelee kuwa hivyo, ili siku ile ikujie ghafla uachwe. Yatafakari maisha yako, ufanye uamuzi sahihi, kwasababu hapa duniani hatuna muda mrefu rafiki yangu. Ulijue tu hilo. Unyakuo upo karibu sana.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?
kwanini yule kijana aliitupa ile nguo ya kitani chini na kukimbia uchi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/02/11/pindo-la-vazi-lake-sasa-limerefushwa/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.