2Samweli 24:1-14,inasema ni jambo la kutisha kuangukia katika mkono wa Bwana je! inakinzana na Waebrania 10:31?.

by Admin | 28 March 2021 08:46 pm03

SWALI: Katika 2Samweli 24:1-14, Hapo tunaona Daudi anasema, afadhali kuangukia katika mkono wa Bwana, lakini anapingana na Paulo katika Waebrania 10:31, anaposema ni jambo la kutisha mtu kuangukia katika mikono ya Mungu aliye hai.

Jibu: Shalom, ukisoma kwa makini utaona kuwa sio kwamba maandiko yanapingana, kwamfano

Tukijifunza hicho kisa cha Daudi kwanini aseme ni heri kuangukia katika mikono ya Mungu, ndipo tutaelewa vizuri.

Kama tunavyoijua habari, Daudi alifanya kosa na Mungu akamwekea mapigo matatu mbele yake achague moja; Taifa lake lipigwe na njaa miaka 7, au Taifa lake lipigwe na ugonjwa wa Tauni siku tatu, au yeye mwenyewe akimbizwe na maadui zake miezi 3.

Sasa katika hizo adhabu tatu alizoambiwa achague, mbili kati ya hizo ni mkono wa Mungu na moja ni mkono wa mwanadamu.. Kwamfano hiyo ya njaa miaka saba na Tauni siku tatu, ni mkono wa Bwana, lakini hiyo ya kukimbizwa na maadui zake miezi 3, ni mkono wa mwanadamu.

Hivyo Daudi kwa uzoefu alioupata katika maisha yake, kupitia kufukuzwa na Sauli nyika kwa nyika, alijifunza kuwa kuwindwa na mwanadamu ni kubaya sana kwasababu mwanadamu hana rehema wala huruma..atakutafuta usiku na mchana, na hata akikushika hatakuhurumia.. Lakini kwa Mungu zipo rehema, huwa anaghairi mabaya, hata kama kashayanena, huwa ana huruma.

Kwahiyo Daudi alipopewa adhabu hizo tatu achague moja, ndipo yeye akachagua kuangukia mikononi mwa Mungu, kwasababu kuna rehema, Maana yake aidha Taifa lake lipigwe na njaa miaka 7 au wapigwe na tauni siku 3, kwasababu pengine wakiwa katikati ya hiyo adhabu Mungu anaweza kuwahurumia na kuikatisha adhabu hiyo, lakini asiangukie mikononi mwa wanadamu wamfukuze na kumwinda, kwani huwa hawakati tamaa na hawanaga huruma.

Na kweli, alipochagua kuangukia mikononi mwa Mungu, Tunasoma Mungu aliwapiga kweli kwa Tauni, lakini tunasoma hazikumalizika  siku zote tatu, Mungu aliizuilia ile Tauni, kwasababu ni mwingi wa rehema.

Tusome kidogo,

2Samweli 24:13 “Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

14 Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na TUANGUKE KATIKA MKONO WA BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.

15 Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu.

16 LAKINI HUYO MALAIKA ALIPONYOSHA MKONO WAKE KUELEKEA YERUSALEMU ILI AUHARIBU, BWANA AKAGHAIRI KATIKA MABAYA, AKAMWAMBIA HUYO MALAIKA MWENYE KUWAHARIBU WATU, YATOSHA, SASA ULEGEZE MKONO WAKO. NAYE YULE MALAIKA WA BWANA ALIKUWAKO KARIBU NA KIWANJA CHA KUPURIA CHA ARAUNA, MYEBUSI”.

Umeona hapo?, Bwana kaghairi mabaya!!.. Lakini hiyo haizifanyi adhabu zake kuwa HERI, Hata kama ataghairi mabaya lakini tayari kashaadhibu wengi, (hapo wameshaanguka watu elfu sabini, pengine walikusudiwa kuanguka watu laki tatu), lakini pamoja na hayo watu elfu sabini si wachache..Ni wengi sana, ni heri Daudi angeangukia kwenye kukimbizwa miezi mitatu yeye peke yake kuliko kuruhusu vifo vya watu elfu sabini..

Hivyo suala bado lipo pale pale kwamba ni jambo la kutisha kuangukia kwenye mikono ya Mungu hata kama ana rehema nyingi, kwasababu ni kweli anaweza akaghairi mabaya, lakini tayari atakuwa ameshaadhibu na kuharibu pakubwa sana..(watu elfu sabi). Ndicho Mtume Paulo alichokisema katika kitabu cha Waebrania…

Waebrania 10:30 “Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.

31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai”.

Kwahiyo mistari hiyo haikinzani bali inakubaliana katika jambo moja…Na Daudi alipochagua kuangukia katika mikono ya Mungu, si kwasababu adhabu za Mungu ni ndogo, bali ni kwasababu zina rehema ndani yake, kulinganisha na zile za wanadamu. Lakini hukumu za Mungu zinatisha na za kuogopwa, na ni kubwa kuliko za wanadamu, kwaufupi si za kutamani kabisa, kama Mtume Paulo alivyosema.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! Daudi hakuwa mtoto wa ndoa wa Yese? (Zab 51:5)

AINA TATU ZA WAKRISTO.

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII?

JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/03/28/2samweli-241-14inasema-ni-jambo-la-kutisha-kuangukia-katika-mkono-wa-bwana-je-inakinzana-na-waebrania-1031/