saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada

by Admin | 6 April 2021 08:46 am04

SWALI: Nini maana ya “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada?”

Jibu: Unabii huo Bwana Yesu aliutoa kwa wanafunzi wake, pamoja na wote ambao watakuja kumwamini baadaye, kwamba utafika wakati kila ambaye atawaua, au kuwatesa atadhani kuwa anamtolea Mungu ibada.  Hiyo ni kuonyesha kwamba mateso ya watu wa Mungu, yanaanzia ndani  ya dini, au Imani, na si penginepo.  Na Bwana Yesu alisema tena, adui za Mtu ni watu wa nyumbani kwake mwenyewe (Mathayo 10:36).

Sasa tukirudi kwenye swali kwanini Bwana Yesu aseme, “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”. Ni kwasababu dhiki ya wakristo, itaanzia kwa watu wanaojiita wa dini.

Tukianza na Bwana wetu Yesu mwenyewe, watu waliomsulubisha ni Makuhani na wakuu wa dini, Hao ndio waliohusika wa kwanza katika dhiki zote za Bwana, mpaka Golgotha..Hawa makuhani, ndio waliomshawishi Pilato Mrumi, amsulubishe Bwana. Na walipokuwa wanafanya hayo, walidhani wanamfanyia Yehova ibada, (yaani wanampendezesha Mungu) kwasababu Torati ya Musa ilisema..

Kutoka 31:15 “Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa”.

Kwahiyo walipomwona Bwana Yesu, anatembea huko na huko kuifanya kazi ya Mungu, ikiwemo kuponya wagonjwa na kuwafungua, wakaamini anaivunja torati, hivyo ili kumpendezesha Mungu, ni lazima Bwana Yesu auawe kulingana na hilo andiko la Kutoka 31:15. Hivyo walimuua Yesu mioyoni mwao wakiamini kwamba wamelitimiza Neno la Mungu, kwamba kila mtu atakayefanya kazi yoyote siku ya sabato auawe.. kumbe wamepotea!.

Na sio tu Bwana Yesu, tunaona pia mitume wake na wanafunzi wake waliofuata baada yake, Mfano tunamwona mtu mmoja anayeitwa Stefano. Huyu aliuawa na wale waliomwua walidhani wanaitimiza torati.

Matendo 6:8  “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.

9  Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;

10  lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.

11  Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.

12  Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza.

13  Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;

14  maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.

15  Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika”.

Sheria ya mtu aliyemtukana/kumlaani Mungu, ilikuwa ni kifo.

Walawi 24:15 “Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake.

16 Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa”.

Kwahiyo kulingana na hilo andiko Stefano alistahili kupigwa mawe, kwasababu tayari walikuwa wamemwambia kuwa amemtukana Mungu (Ingawa alisingiziwa), hivyo wote walioshiriki kumuua waliamini kuwa wanalitimiza hilo andiko kwamba “yeyote atakayemlaani Bwana Mungu wake, sharti mkutano wote wampige kwa mawe mpaka afe”. Hivyo hao kwa kumuua Stefano walidhani wanamtolea Mungu ibada.

Kadhalika na vifo vya mitume karibia wote, ni hivyo hivyo, wote walioshiriki kuwaua walidhani kuwa wanamtolea Mungu ibada, na yote hayo yametokea ili litimie hilo Neno Bwana Yesu alilolisema. “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”.

Lakini pamoja na hayo, unabii huo wa Bwana haukuishia tu kwa mitume au wakristo wa kanisa la kwanza, bali pia unaendelea mpaka leo. Leo watu wa kwanza wanaotumika na shetani bila kujua kuwaletea wakristo wa ukweli dhiki ni watu wanaojiita watu wa imani, hao ndio shetani anaowavaa kuwaletea wakristo wa kweli dhiki, na hata kuwaua.

Leo hii akitokea mtu wa Mungu kajikana nafsi, na kaenda kasimama mahali Fulani anahubiri, kwa adabu yote, labda kwenye gari, au mahali Fulani penye watu, utaona watakaotokeza wa kwanza kwenda kumshitaki kwa wenye mamlaka, na hata kumweka ndani, kwamba anawapigia kelele na hana kibali ni watu Fulani wanaojiita wakristo, tena wanaoyajua maandiko au hata pengine ni kiongozi Fulani mkubwa wa kanisa. Na anafanya hivyo akitumia andiko linalosema…

Warumi 13: 1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu”

Na tena anafurahi kuona au hata akisikia Yule mtu kapotea kabisa, huku moyoni akiamini kwamba “anamfanyia Mungu ibada”, kumbe anamfanyia ibada shetani. Wakati yeye anafurahia Yule mtu kutiwa ndani, upande wa pili kuna mtu yale maneno yamemgusa na anakwenda kutubu..

Wakati Fulani Petro na Yohana walisimama hekaluni kuhubiri, wakakamatwa na wakuu wa dini, na kutiwa gerezani, wakiwa kule gerezani malaika akaja kuwatoa, na huyo huyo malaika akawaambia warudi kuhubiri kule kule hekaluni walikokamatiwa. Sasa huyo malaika hakujua kwamba wanapaswa watii mamlaka iliyo kuu, na wawe na vibali?? Kasome Matendo 5:17-21.

Bwana Yesu alisema katika Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19  Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi…”

Hivyo ni lazima tujihakiki kila siku, na tuwe makini tusije tukajikuta tunafanya mambo tukidhani kuwa tunampendezesha Mungu kumbe ndio tunakwenda mbali naye, na kumuudhi. Ukikuta mahali popote jina la Yesu linatajwa ni vyema ukafunga mdomo wako na kutulia, kwasababu hujui ni nini Mungu anafanya kwa wakati huo.

Bwana atusaidie.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/04/06/nini-maana-ya-saa-yaja-atakapodhania-kila-mtu-awauaye-ya-kuwa-anamtolea-mungu-ibada/