Mego ni nini kama tunavyosoma katika biblia? (Mithali 17:1)

by Admin | 12 May 2021 08:46 am05

Mithali 17: 1 Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.


JIBU: Mego ni neno linalotokana na  kitenzi “mega”,(kumega) kitu kilichomegwa, ni kama kimenyofolewa sehemu Fulani kwa udogo sana. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema ni kitu kidogo sana.

Sasa hapo anaposema Afadhali mego kavu, anamaanisha afadhali chakula kidogo sana (Mfano wa mkate mkavu), pamoja na utulivu, au amani, au furaha, kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi, hasira, wivu, fitna, yaani, nyumba ambayo, utapata kila kitu, utakula chakula chenye mboga saba mezani, utakunywa kila aina ya kinywaji, lakini nyuma yake kuna vikwazo, na mafarakano.

Hiyo inatufundisha pia katika mambo ya Maisha, ni heri ufanye kazi mahali utalipwa mshahara mdogo lakini, utapata nafasi ya kutulia na Mungu wako, au utafanya kazi halali itakayokupa amani, kuliko kukimbilia kazi zenye mishara mikubwa, lakini nyuma yake inakukosesha, au haikupi muda wa kutosha kumtafakari Mungu wako.

Na ndio maana sehemu nyingine biblia  inatumia neno “konzi” ikiwa na maana kipimo cha mkono tu, uridhike nacho kuliko vipimo vingi lakini unataabika rohoni na mwilini.

Mhubiri 4:6 “Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo”.

Kabla hatujaamua jambo lolote tunapaswa tujihakikishie kwanza usalama wa roho zetu, si kila aina ya fursa inayokuja mbele yetu ni ya kuikimbilia kisa tu inatupa donge nono, au inatupa Maisha mazuri. Wengi wamerudi nyuma kiimani, kama sio kuupoteza wokovu wao kabisa kisa tu tamaa ya “VINGI” au Tamaa ya mali.

Yupo mtu mmoja aliacha kazi ya uchungaji alioitiwa na Mungu, kisa tu haimlipi vizuri, akaingia katika biashara, akaanza kufanikiwa na kuzidi, mpaka akawa anaenda China kuleta mzigo, sikumoja akiwa njiani anaelekea katika miradi yake Daresalaam, akapata ajali mbaya sana, akafa.

Jiulize huko anatapokwenda atakuwa mgeni wa nani?

Hivyo na wewe ridhika na kile unachokipata hata kama ni mego kavu, maadamu  kinakupa amani, na Muda kwa Mungu wako. Ridhika tu na hicho, hapa duniani tunapita.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Wibari ni nani?(Mithali 30:26)

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Mkatale ni nini katika biblia? (Matendo 16:24)

Mpumbavu ni nani katika biblia? (Zaburi 14:1, Mithali 10:14)

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

Rudi nyumbani

WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/12/mego-ni-nini-kama-tunavyosoma-katika-biblia-mithali-171/