Nondo ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

by Admin | 25 May 2021 08:46 pm05

Neno hili utalikuta sehemu nyingi sana katika biblia,  kwa mfano hivi ni baadhi ya vifungu ambavyo utakutana na neno hilo;

Ayubu 13:28 “Nijapokuwa ni kama kitu kilichooza, kinachosinyaa, Mfano wa nguo iliyoliwa na nondo.

Isaya 50: 9 “Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala”.

Mathayo 6:19 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;

20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;

21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.

Yakobo 5:1 “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia.

2 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo”.

Soma pia Ayubu 4:19, Zaburi 39:11, Isaya 51: 8, Hosea 5:12

Nondo ni wadudu, jamii ya vipepeo, unaweza kuwaona kwenye picha juu. Wadudu hawa, huwa wakishafikia hatua ya kutaga mayai, tabia yao ni kwenda kwenye nyumba za watu, na kutaga maeneo ambayo yana nguo, au sehemu zenye asili ya vitu vya pamba pamba au manyoya kama vile kwenye makapeti, n.k. lengo likuwa ni siku vifaranga watakapototolewa wapate chakula, na chakula chao ndio hizo nguo.

Kwa kawaida wakishafikia hatua ya vipepeo hawana uharibifu wowote, lakini wakiwa bado ni “lava” ndio wanatafuna nguo, na vitu vyote vyenye jamii ya hiyo vilivyopo ndani.

Natumai hata na wewe ulishawahi kuwaona, tazama picha  chini, hao wanaoonekana kama vimbegu vya maboga ndio lava wenyewe.

lava wa nondo

Ndio hapo unashangaa suti yako nzuri uliyoiacha kabatini, umeinunua kwa bei ghali unaikuta na matobo tobo, unadhani ni mende, hujui kuwa ni kazi ya hawa wadudu.

nguo iliyoliwa na nondo

Sasa kibiblia wadudu  hawa walikuwa wanawakilisha uharibifu, wa aina yoyote. Na ndio maana Bwana Yesu alisema;

“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba”; ..Akiwa na maana kuwa haijalishi ni vitu vilaini au vigumu, kama ni vya chuma, vitaliwa na kutu,  vikiwa ni laini kama nguo bado vitaliwa na nondo. Hiyo ni kuonyesha kuwa hakuna hazina yoyote inayodumu ikiwa haikuwekezwa mbinguni.

Ni ajabu sana, kumwona Mkristo anayo mabilioni ya pesa kwenye account zake za benki, ukimuuliza zote hizo ni za nini atakuambia najiwekea akiba ya baadaye na watoto wangu. Wakati huo huo hajawahi kufikiria hata kumfanyia Mungu kitu. Hajui kuwa mali zina mbawa, kama biblia inavyosema. (Mithali 23:5)

Kunaweza tokea anguko kubwa la uchumi na fedha isiwe na thamani tena, kunaweza tokea wizi, na hazina zako zote zikachukuliwa na wengine, kunaweza tokea matatizo Fulani ya ghafla na hicho ulichojilimbikizia kwa miaka mingi ukakitumia chote kutatua matatizo hayo, au pengine unaweza ukafa na usifaidi chochote katika hicho ulichojikusanyia wakaja kula wengine, na hao wengine biblia inasema hujui kama watakuwa na hekima au wapumbavu, wakazitapanya kizembe, na hazina yako ikawa ni bure..

Lakini mtu anayejiwekea hazina kwa Mungu, Mtu kama huyo hazina yake ni lazima idumu milele. Kwanza itamwongezea ulinzi wa kiroho na kimwili akiwa hapa hapa duniani, pili itaandikwa mbinguni, na siku ile Bwana atakapomlipa kila mtu kulingana na kazi yake ,basi  na yeye pia atapokea thawabu idumuyo milele.

Jiulize ndugu, nguvu zako zote unazipeleka wapi? Au unamwandalia NONDO azile? Kama utashindwa leo hii kuifanya kazi ya madhabahuni, basi hakikisha kuwa nguvu zako unazozitaabikia huko usiku na mchana, unazielekeza kwa Mungu wako, ili Mungu awe na sababu ya kukukumbuka siku ile, aone kuwa hukwenda kutaabika bure, bali kwa ajili yake.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/25/nondo-ni-nini-kama-tunavyosoma-katika-biblia/