UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA.

by Admin | 7 June 2021 08:46 am06

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe milele. Karibu tujifunze Neno la Mungu.  Kuna wakati sisi wenyewe ndio tunakuwa kikwazo cha Kristo kujifunua kwetu katika utimilifu wake wote, na hiyo yote ni kwasababu tuna mioyo miwili miwili kwake. Leo tutaangalia makundi mawili ya watu. Moja ni wale mafarisayo, na la pili ni mitume wa Yesu likiongozwa na Nathanieli.

Kuna wakati mafarisayo walimwomba Yesu awaonyeshe Ishara itokayo juu ili waamini zaidi, Lakini Yesu akawaambia kamwe hawatapewa Ishara yoyote, isipokuwa ile ishara ya Yona.Akiwa na maana Ishara ya hukumu.

Mathayo 12:38 “Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.

39 Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.

40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi”.

Ili kufahamu kwa urefu alikuwa anamaanisha nini, juu ya hiyo  ishara ya Yona unaweza kufungua link hii kusoma >>> https://wingulamashahidi.org/2019/05/13/madhara-ya-kutafuta-ishara/ 

Lakini Bwana hakuwa na nia ya kutojifunua kwao zaidi, isipokuwa ile mioyo yao, ya kutokuamini, ya unafki, ndio iliyowapelekea kutoona utukufu wa Mungu mkubwa zaidi ya yale waliyoyaona, akiyafanya.

Lakini kulikuwa na wakati ambao Yesu yeye mwenyewe aliwathibitishia wale waliomwamini kuwa wataona mambo makubwa zaidi ya yale waliyomjua kwayo. Lakini hiyo yote ilihitaji kwanza watu hao kutokuwa na “HILA” ndani yao kama Nathanieli alivyokuwa.. Tusome..

Yohana 1:43 “Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.

44 Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.

45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.

46 Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.

47 Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, HAMNA HILA NDANI YAKE.

48 Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.

49 Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.

50 Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.

51 Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu”.

Kama tunavyoweza kusoma hapo, Nathanieli alipokutana na Filipo hakuona shaka ndani yake, juu ya habari njema alizoletewa, japokuwa zilikinzana na kile alichokifahamu hapo kabla..Lakini alikuwa radhi kwenda kufuatilia, kwasababu nia yake ilikuwa ni kupata jambo jema, na sio kitetea dini..

Leo hii ni watu wachache sana, wanaweza kuwa tayari kusikia au kufuatilia lile jambo linalokinzana na imani yao, au dhehebu lao, hata kama watajua ni kweli kiasi gani, bado watapuuzia tu, wakiambiwa katika maandiko hakuna ubatizo wa vichanga, wanadhani wanapelekewa dini mpya, ukiwaeleza habari za kuokoka watakuambia dhehebu lao haliamini hilo.. Unaona, hizo ni HILA zilizondani ya mtu. Lakini Nathanieli hakuwa hivyo? Yeye alipoelezwa tu habari za MASIHI, Akauliza, Je! Inawezekana kweli jambo jema kutokea Nazareti mji ambao haujaandikiwa chochote? Lakini yeye hakuacha kwenda kutazama, ajihakikishie.

Na matokeo yake Yesu alipomwona, hakuhitaji kujieleza mbele zake, Yeye mwenyewe alimtamkia habari zake. “Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake”. Hakuwa na wingu la udhehebu wala udini kama mafarisayo walivyokuwa..Yeye alikuwa radhi kwenda kutazama, mahali ambapo hata hapana uelekeo wa kutokea Kristo.

Na matokeo yake ikawa ni Yesu kuwaambia wataona makubwa zaidi ya yale.. Yaani atajifunua kwao kwa katika viwango vingine vya juu sana, kwasababu walikuwa tayari kumwamini na kumfuata. Na ndio utaona ni hao peke yao ndio walioweza kumwona Yesu mpaka hatua ya mwisho ya kupaa kwake.

Hata na sisi leo hii, tukumbuke kuwa Yesu ni yeye Yule jana na leo na hata milele. (Waebrania 13:8).  Yupo tayari kutuonyesha makubwa zaidi ya haya tunayoyajua, lakini ufarisayo wetu, uvuguvugu wetu, ndio unaotukwamisha tusimjue Kristo katika viwango vingine vya utukufu.

Tunadhani Yesu ni ile sura yake tu basi, hapana, Yesu ni Ufunuo wa Mungu mwenyewe. Na huwa hajifunui kwa watu wote sawasawa. Na ndio maana alivyotembea na mitume haikuwa sawa na alivyotembea na makutano, vilevile sio yote aliyowafunulia mitume aliwafunulia makutano au waandishi. Na sio kila mahali alipopita watu wote walijua. Hapana.

Hiyo yote ni kuonyesha kuwa anajifunua na kutembea katika viwango.

Hata sasa,  yatupasa tumwamini Yesu, tuiamini biblia, tuondoe HILA mioyoni mwetu. Tuwe tayari kutii kile ambacho biblia inatufundisha hata kama kitakinzana vipi na madhehebu yetu, tukiona maandiko yanatuambia tubatizwe kwa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO, tutii, tukiambiwa sanamu ni machukizo kwa Mungu, tutii, tukiambiwa hakuna njia nyingine yoyote ya kutufikisha mbinguni isipokuwa ya Yesu tu peke yake, na sio mtume mwingine fulani tuamini hilo, hata kama dini zetu zimetufundisha hivyo tangu tulipozaliwa kuwa kuna mtume mwingine.

Tukizingatia mambo kama hayo, ambayo ni maagizo ya Yesu mwenyewe kwenye BIBLIA yake. Basi tujue kuwa tupo kwenye daraja kubwa sana, na kumwona yeye katika viwango vingine vya tofauti sana, vya mbingu kufunguka juu yetu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI NI YESU KRISTO WA NAZARETI?

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

BIRIKA LA SILOAMU.

RABI, UNAKAA WAPI?

Rudi nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/07/utaona-mambo-makubwa-kuliko-haya/