Je Lutu alikwenda kuwahukumu watu wa Sodoma na Gomora? Kulingana na Mwanzo 19:9?

by Admin | 5 July 2021 08:46 am07

Jibu: Tusome kuanzia juu kidogo.

Mwanzo 19:4 “ Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote.

5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua.

 6 Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake.

 7 Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi.

 8 Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu”

9 Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, ANATAKA KUHUKUMU! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango.”

Kuhukumu kunakozungumziwa hapo sio kutoa hukumu ya adhabu.. hapana! Bali kunamaanisha “kutoa maamuzi” au “kuamua”.. Mtu anayetoa maamuzi kwa lugha ya kibiblia ni mhukumu. Watu wawili wanapopigana na akatokea mtu akawasuluhisha huyo mtu aliyewasuluhisha ni mhukumu wao, kadhalika mtawala wowote wa nchi mhukumu wa hiyo nchi.

 Mfano mzuri wa kujifunza katika biblia ni Sulemani… Mfalme Sulemani aliomba kutoka kwa Mungu moyo wa kuweza kuwahukumu/kuwaamua watu kwa adili.

1 Wafalme 3:7 “Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.

8 Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi.

9 Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili NIWAHUKUMU WATU WAKO, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?

 10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.

11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; BALI UMEJITAKIA AKILI ZA KUJUA KUHUKUMU;

12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe”.

Tukiendelea mbele kidogo.. tunaona uwezo wa kuhukumu wa Sulemani, ukidhihirika..

“22 Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.

23 Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.

 24 Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.

25 Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.

26 Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.

 27 Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.

28 Na Israeli wote wakapata HABARI ZA HUKUMU ILE ALIYOIHUKUMU mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ILI AFANYE HUKUMU”

Umeona?…maana ya hukumu ni pana, sio tu kutoa adhabu, au kauli ya kuadhibu…kama inavyoaminika sasa…

Kwahiyo hapo, hao watu wa Sodoma walitaka Luthu asitoe maamuzi yoyote juu ya shauri lao hilo, walilokusudia kulitenda.. Kwani walitaka watolewe wale malaika waliofika kwa Luthu ili walale nao. Na hawakutaka shauri lolote juu ya hilo, walichokisema wamekisema, na walichokiamua wamekiamua…

Sasa anatokea huyu Luthu ambaye kwanza ni mgeni tu katika hiyo nchi wa Sodoma, halafu anataka kuwapangia cha kufanya, “kwamba awape binti zake wawili walale nao badala ya wale malaika”…Jambo ambalo wao hawakulitaka.. Ndio maana wakasema maneno hayo.. “Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, ANATAKA KUHUKUMU! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa”

Na sisi katika maisha yetu  tuna mambo mengi ya kuhukumu, katika imani yapo mengi ya kuhukumu, katika familia zetu, katika shughuli zetu n.k kuna mambo mengi ya kuhukumu.. Na hivyo inahitajika siku zote hekima ya kiMungu ili kuhukumu kwa adili. Si lazima wakati wote tuombe tu mali na mafanikio ya kidunia kutoka kwa Mungu. Ni vizuri tukamwomba hekima ya kuhukumu kwa Adili kama Sulemani alivyoomba, na kwasababu Mungu anajua pia hayo mengine tuna haja nayo, hivyo atatuzidishia sawasawa na Neno lake, kama alivyomzidishia Sulemani.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Sodoma ipo nchi gani?

Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Biblia inamaanisha nini iliposema “wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa;?

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/05/je-lutu-alikwenda-kuwahukumu-watu-wa-sodoma-na-gomora-kulingana-na-mwanzo-199/