TUSIWE WAVIVU WA KUSIKIA.

by Admin | 5 July 2021 08:46 am07

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Karibu tena tuyatafakari maneno ya uzima.

Kuna wakati Mtume Paulo alifunuliwa siri nyingi sana zimuhusuzo Bwana wetu Yesu Kristo, hususani zile zinazomlinganisha yeye na Melkizedeki. Na hamu yake ilikuwa ni  kanisa zima lifahamu siri hizo, lakini alikumbana na kipingamizi kikubwa, ambacho kilimfanya asiweze kuzieleza zote, na kipingamizi chenyewe ni ule UVIVU WA WATU KUSIKIA.

Waebrania 5:10 “kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

11 Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia”.

Embu tengeneza picha kama Paulo angeendelea, kumwelezea Melkizedeki kama alivyokuwa anamwelezea katika sura hizo chache za kitabu cha waebrania, ungefahamu mangapi ya ziada yamuhusuyo Bwana Yesu, kuliko hayo unayoyajua sasa hivi, Lakini asingeweza kuwaeleza kwasababu hata yale ya mwanzo machache tu, bado watu walikuwa ni wavivu wa kufuatilia..Hivyo kama mwalimu asingeweza kufundisha hesabu za maumbo wakati hesabu kujumlisha na kutoa bado watu hawazijui.

Hata sasa tabia hii, ipo miongoni mwa watakatifu. Ni rahisi kusikia mkristo fulani akisema tena kwa ujasiri, “Aah huu ujumbe ni mrefu siwezi kusoma” lakini wakati huo huo anaweza kumaliza vitabu vitatu vya hadithi, na asione shida. Anaweza kusikiliza mahubiri dakika 10, lakini muvi za kidunia, akakesha nazo usiku kucha.. Anaweza akatumia dakika 2 kutazama video ya ki-Mungu, lakini akatumia saa 6 kuchat Instagramu, na Facebook. Huyo ni mkristo, hatuzungumzii mpagani. Na bado atagemea Mungu atajidhihirisha kwake zaidi ya hicho kiwango anachomjua.

Ndugu, kila siku Bwana anataka tujae maarifa, ili tuweze kuishi kulingana na viwango anavyovitaka yeye kwetu. Mtume Paulo japokuwa alipewa mafunuo makubwa sana yamuhusuyo Mungu, na kule mbinguni, mpaka Mungu akamwekea mwiba maishani mwake ili asijisifu kupita kiasi kwa wingi wa mafunuo hayo (2Wakorintho 12:7).. Lakini bado hakuwa mvivu wa kusoma Neno la Mungu, na kutaka kujua habari za Mungu, Na ndio maana utaona mpaka dakika yake ya mwisho anamwagiza Timotheo ambebee vile vitabu vya ngozi (torati na manabii) ampelekee.

2Timotheo 4:12 “Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso.

13 Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi”.

Sisi tumekuwa kikwazo cha Mungu kujifunua kwetu katika utimilifu wote, Kwasababu ya uvivu wetu wa kusikia/kusoma.  Leo hii Bwana atusaidie tuzidishe bidii, kumtafuta Mungu. Ili Bwana ajifunue kwetu zaidi. Bwana Yesu alisema..

Yohana 3:12 “Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni”?

Kumbe alitamani pia kuwaeleza watakatifu wa kipindi kile mambo ya mbinguni, lakini kwa ajili ya uvivu wao wa kutamani kujifunza, hawakuambiwa. Ndugu yangu Leo hii ua TV unazoangalia muda wote, ua huo muda unaokesha Instagramu, na facebook, kutazama video ambazo hazikujengi. Usipokuwa na instagramu, hupungukiwi chochote, si lazima uwe nayo, Muda utakuwa nao mwingi sana na wa kutosha,wa kusikiliza habari za Mungu, na kusoma, kama utaacha mitandao ya kijamii ikupite.

Kumbuka, Mungu anatazamia kile mkristo akue siku baada ya siku.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

Naomba kufahamu maana ya “sura ya kijiti” katika Marko 12:26.

Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika..

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/05/tusiwe-wavivu-wa-kusikia/