by Admin | 15 July 2021 08:46 am07
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, karibu katika kuyatafakari maandiko.
Katika biblia tunasoma Kisa cha mabinti wa tano wa mtu mmoja, wa kabila la Manase, waliokuwa mashujaa katika Imani, hata kuibadilisha taratibu ambazo zilikuwepo.
Zamani wakati wana wa Israeli wanatoka Misri, kuelekea Kaanani. Mungu alimpa Musa maagizo ya kuigawanya hiyo nchi watakayoiendea.. Kwamba kila kabila, lipate sehemu ya ardhi katika hiyo nchi ya kaanani wanayoiendea. Lile kabila lenye watu wengi, basi litapewa sehemu kubwa ya ardhi, na lile lenye watu wachache basi litapewa sehemu ndogo ya ardhi. Na kabila la Yuda ndio kabila lililokuwa na watu wengi kuliko kabila zote za Israeli, na kabila la Manase ndilo lililokuwa dogo kuliko yote (yaani lenye watu wachache).
Hivyo wakati wa kugawa urithi, walikuwa wanaangaliwa wale wazee wa ukoo ambao ndio vichwa vya ukoo, wanaomcha Mungu, hao ndio wanaopewa labda tuchukue mfano, hekari elfu moja, na hao ndipo wanagawa hizo ekari elfu kwa watoto wao wa kiume, kufuatia kila familia iliyopo chini yao. Hivyo mwisho wa siku kila familia ilikuwa inapata urithi wa ardhi katika hiyo nchi ya Kaanani waliyokuwa wanaiendea.
Lakini sasa katika hilo kabila lenye watu wachache kuliko kabila zote, yaani kabila la Manase, kulikuwepo na mtu mmoja ambaye alikuwa mashuhuri katika kumcha Bwana, ambaye naye pia alihesabiwa kama kichwa, ambaye aliandikiwa urithi katika hiyo nchi waliyokuwa wanaiendea.. Mtu huyo aliitwa SELOFEHADI.
Lakini kwa bahati mbaya mtu huyo alikufa kabla ya kuzaa mtoto wa kiume ambaye angerithi sehemu ya urithi huo, akawa anao mabinti tu!. Hivyo kutokana na jambo hilo, wana wa Israeli wakalitoa jina lake miongoni mwa watakaopata sehemu ya ardhi katika hiyo nchi ya ahadi wanayoiendea..Kwasababu wanawake hawawezi kupewa urithi!..
Lakini tunasoma jambo moja la kipekee lililotokea..kwa mabinti wa huyo Selofehadi, hatujui Baba yao aliwafundisha nini, lakini tunasoma kwamba walifanya jambo la kipekee kugeuza sheria na taratibu za Israeli kwa IMANI. Kwani walipoona tu! Baba yao amekufa na sehemu yake ya urithi imeondolewa, hawakuridhika, wakasema watamwendea Musa na kudai haki ya baba yao.. Kwamba sehemu ya urithi wa baba yao wapewe wao!.. jambo ambalo ni kinyume na utaratibu, kwani wanawake hawana ruhusa ya kurithi mali..Lakini wanawake hawa watano wa familia moja!, walishindana mpaka wakapata haki yao hiyo.
Hebu tusome kidogo..
Hesabu 27:1 “Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
2 Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema,
3 Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha Bwana katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume.
4 Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.
5 Basi Musa akaleta neno lao mbele ya Bwana
6 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
7 HAO BINTI ZA SELOFEHADI WANANENA LILILO HAKI; KWELI UTAWAPA MILKI YA URITHI PAMOJA NA NDUGU ZA BABA YAO; NAWE UTAWAPA URITHI WA BABA YAO.
8 Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, MTU AKIFA, NAYE HANA MWANA WA KIUME, NDIPO UTAMPA BINTI YAKE URITHI WAKE.
9 Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake.
10 Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake.
11 Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa”.
Kabla ya hapo hakukuwa na sheria kwamba mtu akifa, kama hana mtoto wa kiume urithi wake uende kwa mabinti wake, lakini Mabinti hawa watano, WALILIFUNGUA HILO KWA IMANI. Laiti wangeendelea hivyo, labda mpaka leo Israeli, mabinti wasingekuwa wanapata urithi wowote. Lakini kwa Imani ya hawa mabinti watano wa mtu mmoja ambao majina yao yalitajwa kama MALA, NOA, HOGLA, MILKA, na TIRSA, waliweza kubadili majira kwa Imani..na kuwafanya mabinti wengine wote wa Israeli wafurahi.
Mwanamke au binti, unayesoma haya…kabla ya kwenda kujifunza kwa akina Eliya, na Elisha, na Paulo walio wanaume, hebu jifunze kwanza kwa wanawake hawa!, jinsi gani walivyopata urithi wao!, hawakwenda kwa waganga!..wala hawakwenda kwenye vikundi vya kijamii, wala hawakuanzisha mgomo!, wala vurugu.. bali walikimbilia kwa Musa, aliye mtumishi wa Mungu pekee wakati huo, huku wakiwa na hoja zilizo shiba, ambaye huyo Musa alilipeleka hoja zao kwa Baba wa mbinguni, na Baba wa mbinguni akatoa majibu..
Lakini sasa aliyesimama kama Musa, ni Bwana Yesu, huyo ndiye wa kukimbilia ili kudai urithi wako..Ukienda na hoja zenye nguvu mbele zake, utapata haki yako.. Na hoja zenye nguvu tunazipata katika Neno la Mungu..
Isaya 41:21 “Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo”.
Isaya 43: 26 “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, UPATE KUPEWA HAKI YAKO”
Jambo lingine la kujifunza juu ya mabinti hawa watano ni UMOJA!. Hakutoka binti mmoja na kumfuata Musa.. hoja yake isingekuwa na nguvu.. Lakini walipojiunga mabinti wote watano na kuwa kitu kimoja..Ndipo hoja yao ilipokuwa na nguvu. Ni vile vile hata sasa, ili Hoja zetu ziwe na nguvu mbele za Mungu, ni lazima tuungane watu wa familia moja, ambao imani yetu ni moja, Baba yetu ni mmoja, na ndipo tukamsogelee.. Tukienda kwa umoja kama huo, basi nirahisi sana kupokea majibu kuliko kwenda mmoja mmoja..
Mathayo 18:19 “Tena nawaambia, ya kwamba WAWILI WENU WATAKAPOPATANA duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni”.
Umeona hapo, anasema “wawili wenu”.. maana yake ni zaidi ya mmoja.. watakapopatana… maana yake kinachotangulia ni kupatana na kukubaliana… na baada ya kupatana, wakiliomba hilo jambo watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.
Bwana atusaidie tuwe na imani kama ya mabinti wa Selofehadi pamoja na Umoja, ili tuweze kufungua milango iliyofungwa mbele yetu.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je! Israeli wote wataokolewa siku ya mwisho kulingana na Warumi 11:26?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/15/funguo-walizokuwa-nazo-mabinti-watano-wa-selofehadi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.