Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

by Admin | 25 July 2021 08:46 pm07

SWALI: Kwanini Bwana Yesu alisema watu wa kizazi kile wamefanana na watoto walioketi masokoni na kuitana,? Mfano huo unaelewekaje?

Na pia alikuwa na maana gani kusema maneno haya?

Luka 7:35 “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”


JIBU: Habari hizo utazisoma katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni Mathayo 11:16-20 na ya pili ni  Luka 7:31-35

Sasa tuisome hiyo ya Luka ndio yenye vifungu vya moja kwa moja vya swali lenyewe;

Luka  7:31 “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?

32 Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.

33 Kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo.

34 Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi.

35 Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.

Shalom.

Bwana Yesu alitoa mfano ambao ulikuwa ni wa kawaida na uliojulikana kwa wagalilaya wakati ule. Kwani ilikuwa ni desturi watoto wa aina mbalimbali  kukutana masokoni kwa ajili ya michezo kulingana na desturi zao, na walipokutana walikuwa wanaunda makundi mawili makubwa, lengo lao likiwa ni kuigiza mambo ambayo waliona watu wazima wakiyafanya aidha katika misiba au sherehe.

Sasa kundi la kwanza lilikuwa linaanza kwa kupiga filimbi za kwenye masherehe walizowahi kuzisikia mahali fulani zikipigwa huko nyuma, na lile kundi lingine kazi yake ilikuwa ni kuitikia kwa kucheza, kama watu wazima walivyofanya. ( Soma Luka 15:25)

Baadaye tena vivyo hivyo, wanarudia  kuigiza  nyimbo za misibani, wale wengine wanajifanya kama wanalia kwa kupiga piga vifua vyao. (Soma Mathayo 9:23).  Hivyo hata watu wazima walipowaona hawakuwazuia bali waliwaacha, kwani walikuwa wanaamini vitendo vile vinawajengea uzalendo wa kutambua tamaduni zao za kiyahudi.

Sasa kulingana na maneno ya Bwana Yesu ni kuwa, watoto hawa walipokusanyika, kundi lile la kwanza lilipopiga filimbi za masherehe, wale wengine hawakuonyesha mwitikio wowote walizira, pengine wakadhani wanataka za msiba, na walipowapigia wenzao za msiba, bado pia hawakujifanya kama wanaomboleza. Kitendo ambacho  pengine kiliwakasirisha wale waliojitoa.

Akifunua kuwa, Yohana alikuja kwa njia ya kujitenga sana na ulimwengu, hivyo pengine wangemwamini kwa maisha yake ya majangwani, na kutokula kula au kunywa, kama vile mtoto aliyewapigia filimbi za maombolezo, lakini hawakulia..Yaani mafarisayo na waandishi hawakuonyesha mwitikio wowote. Kinyume chake wakasema watu wenye mapepo, ndio wanaishi maisha ya namna hiyo, hakuna mtumishi mwenye akili timamu, akawa mchafu na mtu asiyejijali namna ile.

Labda hiyo ikaonekana kama ni njia ngumu kwao kuamini manabii wa Mungu, Hivyo Mungu akawapelekea mkuu wa uzima mwenyewe, Yesu Kristo, Bwana wetu, ambaye yeye alikuja kwa njia ya kula na kunywa, mtu wa watu, aketiye katikati ya wenye dhambi, hivyo mbele yao akafanana na wale watoto waliopiga filimbi, ili wenzao wacheze.. Lakini bado hawakuonyesha mwitikio wowote kwa injili ya Bwana, kinyume chake, wakamwita mlevi na mlafu. Hakuna mtumishi wa Mungu kweli anaweza kushinda bar muda wote na walevu kuwahubiria.

Kuonyesha kuwa hata sasa, Bado Mungu anaweza kutuma watumishi wake, katika wito tofauti tofauti, lakini bado watu wasiompenda Mungu wakapinga tu, wakadhihaki, wakakejeli, wakadharau. Akitumwa nabii wa Mungu anayehubiri injili ya kweli, ambaye pengine ni tajiri, na ana mali, watasema, tapeli huyu, anakula sadaka za waumini, wakipelekewa nabii ambaye muda wake wote anashinda sehemu za ibada, au milimani, mwenye nguo moja, asiye smati, hafanyi kazi yoyote isipokuwa kushinda uweponi mwa Mungu, watasema huyu mlokole maskini hatumtaki, kama Mungu wake ameshindwa kumfanya hata asivae viatu vilivyotoboka, atawezaji kunisaidia mimi?

Unaona?

Lakini sasa ukiendelea mistari inayofuata, Bwana Yesu ndio anasema..

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.. Ukisoma kwenye Mathayo 11:19 inasema “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”. Hii ikiwa na maana Hekima ya Mungu ya kuokoa watu, imejulikana kuwa ni ya kweli kwa watoto wake ambao ni (Yohana na Yesu Kristo mwenyewe).. Kwamba kwa vyovyote vile, iwe ni katika utajiri au katika umaskini, au katika kujichanganya au kutojichanganya..kama ni ya Mungu, basi itathibitika tu kwa kazi zake,(matunda yake).

Hata leo hii, usimuhukumu mtumishi wa Mungu kisa ni tajiri, au ni maskini, au anakula au hali, vilevile usihukumu huduma yoyote kisa ni kubwa, au ni ndogo, au inamfumo huu au ule.. kwasababu Hekima ya Mungu haichagui mfumo wa kutembelea. Bali ihukumu hiyo huduma kwa kazi zake baada ya hapo.

Ikiwa matunda yake, ni yale ya Kristo, basi muheshimu mtumishi huyo au huduma hiyo, ikiwa watu wake, wanauelekea wokovu wa kweli na wanaishi maisha ya kumpendeza Mungu basi heshimu hata kama ipo kinyume na matazamio yako.

Vilevile ukiona mtumishi ni tajiri, au ni Yule maskini anayeishi milimani, na anachokifanya hakina matunda Kristo anayoyataka sawasawa na Neno lake. Yaani watu wake ndio wanakwenda mbali na wokovu na utakatifu, maisha yako ni ya kidunia, wanafuata tu kuponywa, basi lakini upendo na Kristo hawana.. achana naye, hata kama atajiona ni wa rohoni kiasi gani..au ni mtu wa kijamii namna gani, au mwenye ushawishi namna gani, achana naye. Hekima ya Mungu haipo hapo.

Kwasababu hekima ya kweli ya Mungu inathibitika kwa kazi zake. Kama ilivyothibitika kwa Bwana Yesu na kwa Yohana, japokuwa mapito yao yalikuwa ni tofauti lakini matunda yao yalikuwa ni thabiti.

Hiyo ndio sababu Bwana Yesu aliwaambia wale mafarisayo maneno hayo..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Au bofya chini kujiunga na group la whatsapp moja kwa moja;

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

Mada Nyinginezo:

Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika? Ina maana gani?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/25/na-hekima-imejulikana-kuwa-ina-haki-kwa-watoto-wake-wote/