Sadaka ya kutikiswa ilikuwaje?

by Admin | 14 December 2021 08:46 pm12

Katika Agano la kale zilikuwepo aina za sadaka mbali mbali, ambazo Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wazitoe, ilikuwepo sadaka ya Amani, sadaka ya dhambi, sadaka ya kuinuliwa, kadhalika ilikuwepo sadaka ya kutikiswa na nyingine nyingi. Leo tutaitazama hii sadaka ya kutikiswa kwa ufupi na ujumbe wake katika roho.

Awali ya yote ikumbukwe kuwa makuhani peke yao ndio waliopewa dhamana na Mungu ya kutumika katika nyumba yake, na ndio waliopewa dhamana ya kufanya shughuli zote za kikuhani, ikiwemo kupokea sadaka kutoka kwa watu, walizomletea Bwana. Sadaka hizo zilikuwa za aina tofauti tofauti, zilikuwepo za wanyama, zilikuwepo  za ndege kama njiwa, zilikuwepo pia  za nafaka kama ngano, unga na nafaka nyingine.

Endapo Mtu akileta sadaka yake ya mnyama kama kondoo, basi alimleta kwa kuhani, kisha kuhani atamchinja Yule kondoo na kuichukua damu yako, ambayo hiyo ndiyo itakuwa kwaajili ya upatanisho wa Yule mtu, kisha viungo baadhi atavichoma juu ya madhabahu ndani ya Hema au hekalu mbele za Bwana, na sehemu ya nyama iliyobakia ambayo haijachomwa, Mungu aliruhusu Kuhani huyo iwe yake yeye na familia yake (Ndio mshahara wake). Makuhani walikuwepo wengi wanaofanya kazi hizo, na walikuwa wanafanya kazi hizo kwa zamu.

Na sadaka ya unga, ilikuwa ni hivyo hivyo, kiwango kidogo kilichomwa juu ya madhabahu mbele za Bwana na kiwango kilichobakia kilikuwa ni kwaajili ya Makuhani waliohudumu katika nyumba ya Bwana, Sadaka zote za dhambi na hatia ndio zilikuwa zinatolewa kwa utaratibu huo.

Sasa sadaka ya Kutikiswa ilikuwa ni tofauti kidogo, Kwani baada ya sadaka kupokelewa na Kuhani, kama ni Nafaka au Mnyama. Basi kuhani alichukua kwanza sehemu ndogo ya sadaka hiyo na kuinyanyua juu na kisha KUIPUNGA HEWANI MBELE ZA BWANA, kwa mfumo wa KUITIKISA TIKISA, Kisha baada ya hapo ataishusha chini, na kuendelea na hatua nyingine za kutekekeza baadhi ya viungo juu ya madhabahu, na sehemu iliyobakia ni riziki yao.

Sadaka ya kutikishwa ilihusisha aina zote za sadaka, yaani za Wanyama, ndege pamoja na Nafaka.  Sasa sio kila sadaka wana wa Israeli walizokuwa wanazileta zilitikiswa namna hiyo mbele za Bwana, la! Bali ni baadhi tu!.

Walawi 7:28 “Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

29 Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa Bwana, atamletea Bwana matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani;

30 mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa SADAKA YA KUTIKISWA MBELE YA BWANA.

31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe.

32 Mguu wa nyuma wa upande wa kuume mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka katika hizo sadaka zenu za amani.

33 Katika wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kuume kuwa sehemu yake.

34 Kwa maana, HICHO KIDARI CHA KUTIKISWA, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli.”.

Mistari mingine inayozungumziwa sadaka hiyo ya kutikiswa ni Kutoka 29:27,Walawi 8:27, Walawi 9:21, Walawi 10:14, Hesabu 6:20, Hesabu 8:11, na Hesabu 8:18.

Sadaka hiyo imebeba ujumbe gani kwetu?

Mungu aliruhusu baadhi za sadaka zitolewe kwa  njia ya kawaida na nyingine zitolewe kwa njia hiyo ya kunyanyuliwa juu na kutikiswa tikiswa, (yaani kuipungia hewani)

Kutufundisha kuwa na sisi hatuna budi kuzitofautisha sadaka zetu, Sadaka ya kumshukuru Mungu kwa matendo aliyokufanyia mwaka mzima, au mwezi mzima, au jinsi alivyokuokoa na majaribu makuu haiwezi kuwa sawa na sadaka ya kawaida unayomtolea siku zote, Ya shukrani ni lazima iwe ya juu kidogo, na uitangaze mbele zake, kwasababu ya matendo makuu aliyokufanyia, ni  lazima iambatane na kuinyanyua mikono yako juu na kumwimbia kwa kumshukuru, na kumtukuza, Sadaka ya namna hiyo inapendeza zaidi mbele za Mungu wetu..

Bwana atubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/14/sadaka-ya-kutikiswa-ilikuwaje/