FUNDISHO KUU LA NEEMA YA MUNGU KWETU.

by Admin | 26 January 2022 08:46 am01

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia, chakula cha uzima wa roho zetu.

Maandiko yanasema kuwa tunaokolewa kwa Neema na si kwa matendo,

Waefeso 2:8 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;

9 wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”.

Maana yake ni kwamba hakuna tunachoweza kukifanya sisi kwa matendo yetu, kikatufanya tuwe na haki ya kuokolewa, haijalishi tutajiona tunafanya mema kiasi gani, bado tuna mabaya mengi tunayoyafanya pasipo sisi kujijua. Mbwa anaweza kujiona yupo sawa katika njia zake zote, lakini wewe mwanadamu bado utamwona anazo kasoro nyingi. Na kwa Mungu wetu ni hivyo hivyo, kamwe hatuwezi kujisifu kwa matendo yetu kwake, haijalishi tutajiona ni wasafi kiasi gani, kwake yeye bado tutakuwa na kasoro nyingi tu!.

Lakini katika kasoro zetu hizo bado anatupa wokovu. Sasa kitendo hicho cha kupewa Wokovu bure! Pasipo matendo yetu ndicho kinachoitwa NEEMA!..

Lakini sasa hii NEEMA, ambayo inatupa wokovu bure pasipo matendo, inayo DARASA. Maana yake inafundisha!.. Kuna kitu inataka kutoka kwetu!. Ambapo ikikikosa hicho kitu kutoka kwetu basi na yenyewe inatukataa sisi.

Sasa kitu hicho ni kipi??

Tusome,

Tito 2:11 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;

12 NAYO YATUFUNDISHA KUKATAA UBAYA NA TAMAA ZA KIDUNIA; TUPATE KUISHI KWA KIASI, NA HAKI, NA UTAUWA, KATIKA ULIMWENGU HUU WA SASA;

13 tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu”

Umeona hapo mstari wa 12?. Kitu gani neema ya Mungu inatufundisha au inachotaka kutoka kwetu?.. inatutaka sisi KUUKATAA UBAYA NA TAMAA ZA KIDUNIA!!!. Hicho tu!.. Inatutaka sisi tuwe wanafunzi bora juu ya hilo!. Tukiweza kufanikiwa kujifunza jambo hilo basi Neema ya Mungu itakaa na sisi milele!..

Haitatazama kasoro nyingine ndogo ndogo tulizo nazo. Mbwa anayekubali mafunzo ya Bwana wake ya kutotoka nje kuzurura na anapokubali kuwa na nidhamu, Bwana wake atampenda, kasoro nyingine ndogo ndogo alizonazo atazifumbia macho!, lakini Mbwa anayekataa mafunzo machache ya Bwana wake, hataki kufundishika, ni mzururaji huko na kule, Bwana wake atamchukia na kumfukuza!.

Na neema ya Mungu ni hivyo hivyo, tukitii FUNZO lake hilo la KUUKATAA ULIMWENGU NA UBAYA WOTE!, Zile kasoro nyingine ndogo ndogo tulizonazo neema ya Mungu haitaziona, tutahesabika tu kuwa tumestahili mbele zake.

Wengi leo hawapendi kuishi Maisha ya kuukataa ulimwengu.. huku wakiamini au kuaminishwa kuwa “tunaokolewa kwa neema na si kwa matendo”..pasipo kujua NEEMA YA MUNGU, nayo kuna kitu inataka kutoka kwetu!

Ukitaka Neema ya Mungu ikae nawe ni lazima ukatae fashion za kiulimwengu.

Ukitaka Neema ya Mungu ikae nawe ni lazima ukatae anasa za kiulimwengu

Ukitaka Neema ya Mungu ikae nawe ni lazima ukatae kujichubua, kuvaa wigi, kuweka rasta, hereni, kupaka wanja, lipstick, kuvaa suruali kwa wanawake, kuvaa vimini na nguo za kubana.

Ukitaka Neema ya Mungu ikae nawe ni lazima ukatae ulevi, kusikiliza miziki ya kidunia, kujichua, kuzini kutukana, kuiba na mambo yote yanayofanana na hayo.

Usidanganyike kuwa NEEMA YA MUNGU, inakubaliana na UDUNIA!.. Neema ya Mungu na udunia ni vitu viwili tofauti!..

Je! Umeukataa ubaya?..umeukataa Udunia?

Kama bado, basi fahamu kuwa Neema ya Mungu inakufundisha hivyo leo. Tubu dhambi leo na mpokee Yesu, na ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo na Roho Mtakatifu atakuongoza katika kweli yote, na kukusaidia kulitii agizo hilo la Neema ya Mungu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

USIWE MSIKIAJI TU! BALI MTENDAJI.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Je! Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

Amri zilizo ndogo alizozizungumzia Yesu ni zipi?

Neema ni nini?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/26/fundisho-kuu-la-neema-ya-mungu-kwetu/