Upole ni nini?

by Admin | 23 February 2022 08:46 am02

Upole ni kitendo cha kutokuonyesha madhara, kwa mtu au kiumbe kingine, huwa unaambatana na utulivu . Upole unakuwa na maana Zaidi pale ambapo unaouwezo wa kuleta madhara kwa kiumbe kingine lakini hutumii uwezo huo, kumdhuru, Kwamfano ni kitu gani kinachomtafautisha nyoka na ng’ombe.

Nyoka ni kiumbe kidogo, dhaifu, hakina miguu, wala mikono, tofauti na ng’ombe, ambaye ni mkubwa, mzito,na mwenye pembe kiasi kwamba ukiwekwa naye katika mapambano ni rahisi kuuliwa naye. Lakini kwanini wewe itakuwa ni rahisi kumkimbilia ng’ombe na sio nyoka?.

Ni kwasababu ng’ombe ni mpole, si rahisi kutumia uweza wake wa pembe, na nguvu zake kukudhuru . Lakini ukimkaribia tu nyoka muda huo huo, atakuuma na utakufa.

Vivyo hivyo na katika wanadamu. Wapo ambao ni wapole lakini wapo ambao si wapole.

Katika biblia ipo mifano ya watu wawili ambao walishuhudiwa kuwa ni wapole. Wa kwanza ni Bwana wetu Yesu Kristo. Na wa pili ni Musa.

YESU KRISTO:

Bwana Yesu mwenyewe alisema.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Alikuwa ni mpole mfano wa mwanakondoo. Na kwasababu ya upole huo, ilimpelekea mpaka Roho Mtakatifu kushuka juu yake kipekee sana kama HUWA (Njiwa). Kumbuka sikuzote njiwa hatui sehemu isiyo na utulivu, wala hawezi kutua juu ya mnyama mkali kama vile mbwa mwitu, Bali anatua juu ya mnyama mpole kama vile kondoo, na ndio maana Bwana Yesu alitambulika kama mwanakondoo wa Mungu.

Hatushangai ni kwanini Mungu alimtukuza namna ile,kwanini leo hii watu wote wanamkimbilia Kristo, ni kwasababu alikuwa mpole sana rohoni. Sio kwamba alikuwa mnyonge, hawezi kuangamiza, au kuharibu watu, kumbuka Anaitwa pia “Simba wa Yuda”, Tunajua tabia za simba sio upole. Lakini yeye alikuja katika upole.. Hiyo ndio sifa kuu ya mtu mpole.

MUSA:

Mtu mwingine tunamsoma katika biblia aliitwa Musa. Utajiuliza ni kitu gani cha kipekee alichokuwa nacho Musa, mpaka kikamfanya awe karibu sana na Mungu kwa namna ile?

Ni kwasababu ya Upole wake, Tunasoma;

Hesabu 12:3 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi”.

Musa aliwazidi watu wote waliokuwa duniani kwa upole. Na hiyo ikamfanya awe karibu sana na Mungu, kuliko wanadamu wote walioishi duniani wakati huo.

Hata sasa, kanuni ya Mungu ni hiyo hiyo, Tukitaka tumkaribie Bwana sana, hatuna budi kuwa Wapole.

Tunakuwaje wapole?

Kwanza ni Kwa kujishusha: Unapokubali kuonekana wewe ni dhaifu, ni hatua nzuri sana ya kuelekea upole, Lakini unapotaka kujiona wewe ni Hodari wa mambo yote, ni ngumu kuwa  mpole. Usipokubali kuchungwa, , ujue kuwa utabikia kuwa mbuzi sikuzote na si mwanakondoo

Pili Kwa kuzizuia hasira zetu: Hatuna budi, kuwa watu wa kuvizuia sana vinywa vyetu. Hasira huwa ndio chimbuko la ugomvi na vita. Hivyo ukiweza kudhibiti hasira zako hata kama utaudhiwa kiasi gani, hujibu, basi upole taratibu utaanza kujengeka ndani yako.

Tatu Kwa kusoma Neno na kuomba: Hii ni tiba kubwa sana, ukitaka ujue hesabu soma kitabu cha hisabati, halikadhalika ukitaka uwe na upole, usikwepe biblia. Kwasababu hiyo ndio itakukumbusha, misingi ya kuwa mpole kama Kristo alivyokuwa. Vilevile kusali, kunaukaribisha uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yako, na hatimaye utafikia kiwango hicho.

Bwana atusaidie sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Furaha ni nini?

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

TUMAINI NI NINI?

Je aliyezungumza na Musa kule jangwani ni Mungu mwenyewe au malaika wake?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/23/upole-ni-nini/