by Admin | 11 September 2018 08:46 am09
{Mathayo 16:18 “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”}
Mwanzo 22:17 “katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; “ }
Uzao wa Ibrahimu ni uzao wa YESU KRISTO. Hivyo ili mtu ahesahiwe kuwa ni mmoja wa uzao wa YESU KRISTO ni lazima azaliwe mara ya pili katika uzao wake. Na kuzaliwa mara ya pili si katika mwili bali ni katika roho. Tutakuja kuona baadaye kidogo mtu anapaswa afanye nini ili azaliwe mara ya pili. Lakini sasa tutazungumza faida chache za kuwa mmoja wa uzao huu wa kikuhani wa Yesu Kristo.
1Petro 2:9 Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu,
Kama tunavyofahamu tabia za watoto nyingi huwa zinarithiwa kutoka kwa wazazi wao, ndio unakuta labda familia moja ni ya watu viongozi ongozi ukichunguza huko utakuta watoto nao wanarithi hizo tabia za kupenda kuwa viongozi na wakishakuwa wakubwa utakuta nao pia ni viongozi.
Tunaona pia jambo hilo hilo linajitokeza katikati ya makabila, utakuta kabila moja watu wake wote wanafanana tabia Fulani, aidha unaweza ukakuta kabila hilo watu wake wanapenda kusoma hivyo wengi wao utakuta ni wasomi, wengine ni wafanyabiashara, jamii nyingine unakuta ni za watu wakatili, nyingine za wa watu watulivu, nyingine ni za watu wakarimu n.k. Sasa hii haiji hivi hivi hapana bali ni tabia zilizorithiwa kutoka kwa mababa zao ambao ni ndio waanzilishi wa koo hizo.
Pia tazama…
Vivyo hivyo na katika UZAO wa YESU KRISTO. Wote wanaozaliwa humo, kuna roho na tabia zinazofuatana nao katika maisha yao yote. Hivyo wanajikuta zile tabia YESU alizokuwa nazo kama Baba wa ukoo wanazirithi nao pia wanakuwa nazo kwamfano, tabia ya kuchukia dhambi, tabia ya kuwa mtu wa sala, tabia ya upendo, tabia ya kujitoa nafsi yako kwa wengine ikiwemo kusambaza habari njema za ufalme kwa watu wengine.n.k.
Lakini pia ipo SIFA moja kuu leo tutaizungumzia inayotembea katikati ya UZAO huo kikuhani wa Yesu Kristo nayo si nyingine zaidi ya UWEZO WA KUMILIKI MALANGO YA ADUI.
Sasa Malango ya adui ni yapi?
Malango ya adui yamegawanyika katika sehemu kuu mbili.
1) Lango la Shetani kama MBWA-MWITU.
2) Lango la Shetani kama MBWA-MWITU ndani ya vazi la kondoo.
Hayo ndiyo malango makubwa mawili ya shetani anayoyatumia katika siku hizi za mwisho, na katika hayo amefanikiwa kuwapeleka wengi kuzimu na anazidi kuwapeleka wengi sana, hususani kwa njia ya lango hilo la pili
Tunajua siku zote mbwa-mwitu kwa kumwangalia tu utamgundua kiurahisi endapo akiwa katikati ya kondoo, Hivyo shetani jambo pekee leo hii linalomtambulisha kiurahisi kwamba yeye ni shetani si lingine zaidi ya UCHAWI. Hivyo basi huwa anafanya bidii sana kuushambulia uzao wa Mungu kwa njia hiyo. Amefanikiwa kuwadondosha watu wengi ambao sio uzao wa Mungu. Na watumishi wake anaowatumia hapa ni watu waovu, waganga wa kienyeji na washirikina.
Hii ndiyo njia kubwa na ngumu ambayo ndio shetani anaitumia sasahivi kwa bidii zote kuwapeleka wengi kuzimu. Anavamia kundi la Mungu akijifanya kama kondoo, Anafanya hivyo kwa kutumia mitume, waalimu na manabii wake wa uongo kuliangamiza kundi. Silaha yake kubwa ni mafundisho ya uongo, na dini za uongo, Na njia hii anatumia maumbile mengi ya uongo, lengo tu kuwaangusha watu ambao wamesimama katika Imani ya Kristo Yesu.
2Wakorintho 11: 13” Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.
14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.
15 Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”
Sasa kwanini biblia inasema UZAO wako utamiliki malango ya adui. Ni kwasababu Nje ya uzao huo, hutaweza kwa namna yoyote ile kumkwepa shetani na hila zake, kwa njia moja au nyingine utachukuliwa tu.
Wapo watu wadai wao hawadanganyiki katika imani yoyote ile, na huku hawajazaliwa bado mara ya pili hawajui kuwa hata hapo walipo wameshamilikiwa na malango ya kuzimu pasipo wao kujua.
Pia Kuna watu wanasema hawalogeki, na huku wapo nje ya uzao wa YESU kristo. Hawajui kuwa hapo walipo tayari wameshalogwa pasipo wao kujijua… wanadai ukoo wao haulogeki, hawafahamu kuwa ni UZAO mmoja tu ndio unaoweza kumiliki malango ya adui, na huo si mwingine zaidi ya UZAO wa YESU KRISTO.
Haumiliki kwa kukemea mapepo wala kwa maji ya upako au chumvi au mafuta, au udongo hapana bali unamiliki kwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU ndani yao. Pale tu mtu anapozaliwa mara ya pili kwa kumaanisha kabisa,moja kwa moja Roho Mtakatifu anaingia ndani yake, kisha yule Roho anamwongoza kumtia katika kweli yote. Sasa hii KWELI YOTE, ndio yale mafuta ya Roho ambalo ni NENO LA MUNGU.
Kwamfano uchawi unapotumwa kwa mtu ambaye ni MZAO WA YESU KRISTO, labda tuseme ni ugonjwa fulani..na unakuta yule mtu wa Mungu hana habari yoyote, sasa kwasababu yeye ni mzao wa Mungu, Mungu hataruhusu ule ugonjwa umpate, atamkingia pasipo hata yeye kujijua kama katumiwa ugonjwa, Au hata kama Mungu akiruhusu ule ugonjwa umfikie, lile Neno la Mungu lipo ndani yake lile Neno linalosema Mathayo 8: “.. Mwenyewe [Yesu Kristo] aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” ….
Basi atalitumia hilo Neno na kuanzia huo wakati anakuwa na amani akijua kuwa kwanza yeye ni mzao wa Mungu, na hakuna kilichopo juu yake,…Hivyo kule kuzimu wakitazama juu na kuona imani ya yule mtu imesimama, watajaribu kutupa ugonjwa tena na tena na wataona hakuna mafanikio hivyo wataacha kushughulika naye, na baadaye yule mtu anarudia katika hali yake ya kawaida.
Sasa huyo mtu anakuwa kaimiliki kambi ya adui, hakuna uchawi utakaosimama mbele yake, haihitaji maji, wala chumvi, wala mkesha wa maombi kumshinda shetani, ni NENO TU! (Waefeso 6:11-17)
Kwa kuwa shetani kazi yake ni kuakikisha anawaangusha wengi na kuwapeleka wengi kuzimu anajua kuwa akitegemea njia ya uchawi tu peke yake atawakosa wengi, hivyo alibadilisha mbinu na kuhamia kanisani, akijifanya na yeye kuwa mkristo, jambo analohakikisha ni kumtooa mtu katika mstari wa Neno la Mungu, na kumfanya aamini mafundisho mengine ya uongo nje ya Neno la Mungu. Na akishafanikiwa tu hivyo, basi ameshakumaliza…hapa ndipo watu wengi wanapoanguka, na anateleleza jambo hilo kwa kutumia wahubiri wa uongo.
Sasa kama wewe ni mazao wa YESU KRISTO, na yale mafuta yanakaa ndani yako ni rahisi kuwatambua,.Hutawatambua kwa miujiza, hutawatambua kwa karama, hutawatambua kwa chochote kile isipokuwa kwa matunda yao tu. Na matunda yao ni kile wanachokifundisha na kukizalisha, ukisaidiwa na Roho Mtakatifu kuwatambua.
Na ndio maana Bwana Yesu hakusema jihadharini na wachawi, au washirikina au mbwa-mwitu hapana..bali tujihadhari na mbwa-mwitu wanaovaa mavazi ya kondoo.
Mathayo 7: 15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua”.
Unaona hapo? Msisitizo mkubwa ni kwa hao manabii wa uongo, na hao wapo katika dini na madhehebu, wanaofundisha watu kinyume na Neno la Mungu, wanafundisha mafundisho ya ibada za sanamu na za wafu, wanafundisha watu kwamba hakuna kuzimu, wanaowafundisha watu kuwa Mungu haangalii mavazi bali roho, wasiowafundisha watu kurudi kwa Yesu Kristo mara ya pili, wasiowafundisha watu umuhimu wa ubatizo sahihi na kuzaliwa mara ya pili na kuishi maisha matakatifu na badala yake wanafundisha watu injili tu za mafanikio na faraja katika dhambi, wasiowaonya watu watubie dhambi zao n.k Hawa wote ni watumishi wa Shetani wa hali ya juu zaidi hata zaidi ya wachawi na waganga wa kienyeji na wana kazi moja tu ya KUWAPELEKA WATU KUZIMU katika daraja la kwanza.
Lakini mtu asipotaka kuingia katika ule uzao, hataweza kumtambua shetani kwasababu hana Roho Mtakatifu ndani yake, Warumi 8: 9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. ”
Sasa mtu anaingiaje katika ule uzao wa Yesu Kristo?
Kama tulivyosema mtu anaingia katika uzao huo kwa kuzaliwa mara ya pili tu!, na maana ya kuzaliwa mara ya pili ni KUZALIWA KWA MAJI na KWA ROHO (Yohana 3:3 na Yohana 3:5), ambako huku kunakuja baada ya mtu kudhamiria kutubu kabisa kwa kumaanisha kuacha dhambi zake, na kuanza kuishi maisha mapya katika Kristo na kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kisha kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu atakayemweza na kumsaidia kumwongoza katika kweli yote.
Ubarikiwe!
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine
Mada Nyinginezo:
MUNGU ALIVICHAGUA VITU AMBAVYO HAVIKO.
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU
“WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”
ULE MSALABA UNAOWEKWA KWENYE KABURI, NA ILE IBADA INAYOFANYWA VINA UMUHIMU WOWOTE KWA MKRISTO?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/09/11/uzao-wako-utamiliki-malango-ya-kuzimu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.