JINSI UNAJISI UNAVYOMGHARIMU MTU.

JINSI UNAJISI UNAVYOMGHARIMU MTU.

Bwana wetu Yesu Kristo atukuzwa. Ni siku nyingine tena tumepewa neema ya kuiona, hivyo nakukaribisha tujifunze Neno la Mungu, maadamu siku yenyewe inakaribia.

Kama vile “Utakatifu na utakaso” vinavyokwenda Pamoja, vivyo hivyo, “Dhambi na Unajisi” ni vitu vinavyokwenda bega kwa bega.

Tofauti na Dhambi na unajisi ni ipi?

Dhambi ni kitendo mtu anachofanya kinyume na Mungu, na huwa inaambatana na kuvunja sheria, au maagizo yake. Kama vile kuzini, kuua, kuabudu sanamu n.k.

Lakini unajisi ni kitendo mtu anachokifanya kinyume na yeye mwenyewe, ambacho mwisho wa siku kinampelekea, Mungu kujitenga naye au kumuacha kwa muda Fulani.

Mtu mwenye dhambi unajisi hauna nguvu kwake bali dhambi tu, ..Lakini mtu aliyeokoka vyote vina madhara kwake, yaani dhambi na unajisi.

Ni sawa na doa jeusi lililopo katika shati, jeupe, doa hilo lingekuwa katika shati jeusi, shati hilo lingeendelea kuvalika kwasababu doa halionekani, lakini likiwa katika shati jeupe hata kama litakuwa safi vipi, doa lile tayari limeshaharibu kila kitu. Sasa huo ndio unajisi. Ambao mtu mchafu, hauna madhara yoyote kwake, lakini kwa msafi ni pigo kubwa.

Sasa kabla kufahamu Zaidi, embu tuangalie kwa agano la kale baadhi ya unajisi ulikuwa katika mambo gani.

Zamani, ilikuwa ukila au ukishika mzoga wa wadudu, au Wanyama ambao ni najisi, adhabu yake ilikuwa na wewe unakuwa najisi, kwa muda wa siku nzima..

Walawi 11:23 “Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.

24 Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni;

Soma pia Walawi 11:29-32

Halikadhalika, kulikuwa na unajisi, wa kujifungua, ikiwa mwanamke atajifungua tu, kile kitendo cha kutokwa damu, tayari ni unajisi ambao  unakugharimu siku saba, Pamoja na hayo, unajisi huo ulimgharimu siku nyingine tena 33, au 66 ikiwa ni mtoto wa kiume.. Kufanya jumla ya siku 40 kwa wa kiume, na siku 80 kwa wakike.

Unajisi huu ulikuwa pia katika kugusa maiti, au kutokwa na uchafu mwilini Soma(Walawi 15:16-20). Ulikuwa unakuwa najisi kwa muda wa siku 7, baada ya kujitakasa.

Sasa nachotaka uone ni kuwa, makosa kama haya aliyafanya mtu juu yake mwenyewe, ambayo hata huwezi kuyaona katika zile amri 10, lakini Mungu aliyatazama sana.

Katika agano la kale, wapo ambao walikuwa wanajitahidi kutotenda dhambi, yaani hawazini, hawaabudu sanamu, hawaibi, wanazitunza sabato n.k.

Lakini walikuwa wanakoseshwa na vitu vidogo tu kama hivyo vya unajisi, Na hivyo vikawa vinatia doa ukamilifu wao. Na matokeo yake, wakawa hawaruhusiwi kuingia hemani kwa Mungu, au katika mkusanyiko wowote wa watakatifu kwa kipindi Fulani, kulingana na aina ya unajisi wenyewe.. kama ni siku moja, au wiki, au miezi..

JE! Katika agano jipya unajisi upoje?

Unajisi wa sasa sio kama ule wa zamani, wa kushika, au kuionja, au kutokwa na vitu mwilini hapana.. Unajisi wa sasa wa mtu upo moyoni, Bwana Yesu alisema hivi;

Mathayo 15:17 “Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18 Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano;

20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi”.

Kama tunavyosoma, hapo, yale mambo ambayo yanakutoka moyoni, kama vile tamaa, uzinzi, uasherati, n.k. Sasa kumbuka hasemi kufanya uzinzi, au uasherati, bali kukutoka..yaani mawazo ya uzinzi au ya uasherati, hayo ndiyo yanayokutia wewe unajisi, kama mtakatifu.

Unaweza kweli ukawa huzini na wanawake, lakini kuruhusu tu tamaa ndani yako, tayari umeshajitia unajisi, unaonekana kama vile tayari umezini sawasawa na maneno ya Bwana Yesu (Mathayo 5:28).

Na matokeo yake, inaweza kukuchukua kipindi Fulani kirefu, usiuone uwepo wa Mungu maishani mwako, kwasababu ya unajisi tu kama huo.

Pengine, unawasengenya wengine, unatukana, una chuki na wengine, kiburi, kijicho n.k.(Soma Marko 7:17-23) mambo kama hayo yanaweza kukufanya uikose furaha ya wokovu kwa kipindi kirefu sana, hata baada ya kutubu kwako.

Hivyo unajisi ni wakujiepusha nao sana wewe kama mtakatifu wa Mungu, unaweza ukawa hauuji lakini kitendo tu cha kumchukia ndugu yako, tayari ni sawa na muuji. Umeshajitia unajisi.

Ili uendelee kubaki katika uwepo wa Mungu wakati wowote, uulinde sana moyo wako.

Bwana atusaidie sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Lumbwi ni nini katika biblia?

JIEPUSHE NA UNAJISI.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

KUONGOZWA SALA YA TOBA

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Faustin Mndiga
Faustin Mndiga
1 year ago

Masomo haya ni mazuri uanaendelea kunitengeneza kila iitwapo Leo.Mungu akubariki mtumishi