Wokovu wa milele/ Ulinzi wa daima (eternal security) Je! ni neno la kimaandiko?

by Admin | 13 December 2019 08:46 pm12

Ulinzi wa daima (eternal security) ni neno la kimaandiko?


JIBU: Ulinzi wa daima, kama inavyojulikana kwa lugha ya kiingereza“eternal security”, linamaana kwamba mtu akishamwamini Kristo akaokoka, basi mtu huyo anakuwa tayari anao ulinzi wa milele wa wokovu wake, na kwamba hawezi kuanguka tena kwenda kuzimu hata iweje, kwani wewe tayari ni milki ya Mungu milele. “Once saved, forever saved”.

Wanaoamini hivyo wanasema, suala la wokovu ni la Mungu mwenyewe, anamwokoa mtu kwa neema na si kwa matendo yake mwenyewe. Na hivyo hata mtu anapochukua uamuzi wa kuupokea wokovu, hata hayo yaliyobakia pia ya kumlinda mtu huyo hadi siku wa mwisho yanakuwa ni ya Mungu..

Lakini Je! Mtazamo huo unatafsiriwa ipasavyo?

Ni kweli ulinzi wa daima/milele ni neno la kimaandiko, kwamba ni kweli mtu akishaokolewa, Saa hiyo hiyo Mungu anampa uhakika wa uzima wa milele, anakuwa ametiwa muhuri hadi siku ya ukombozi wake, (Soma Waefeso 4:30, Warumi 8:33-34, Warumi 8:38-39)..Lakini ahadi hiyo ni kama mtu akidumu katika hiyo neema tu!. Ikiwa atafanya hivyo Mungu hawezi kumwacha akaangamia, atamshikilia mkono kila anapokwenda kuhakikisha haanguki.. Lakini kama hatataka yeye mwenyewe kudumu katika neema (Imani) hiyo, wazo hilo ni la uongo.

Ni sawa umemshika mtoto mkono na kumwambia atembee huku umemshika mkono na ukamwakikishia kwamba akiwa katika mikono yako kamwe hataanguka atakuwa salama daima..Lakini Yule mtoto akasikiliza ushauri wa mtu mwingine kwamba anaweza kutembea peke yake hivyo kwa hiyari yake mwenyewe akakataa na kusema sitaki kushikwa na wewe na akatoka mikononi mwako kwa nguvu je! Akianguka atakulaumu..na kumwambia ulimwahidia hataanguka daima atakuwa salama?..Kitu kisichofahamika na wengi ni kwamba Mungu hawezi kuvuka maamuzi yetu..Huwa hatulazimishi kufanya kitu kama sisi wanadamu tunavyolazimishana..

Hivyo tunapookolewa, hatukai tu tukijitumainisha kuwa tumeshashinda vita moja kwa moja, na kwamba tupo mikononi mwa Mungu salama…Tunapaswa tufahamu kuwa ndio kwanza tumeanza vita kwasababu Adui yetu shetani atataka kutufanya tuamue kuiacha imani..

Mapambano yanaendelea;

Na ndio maana kuanzia huo wakati (baada ya kuokoka) mambo huwa hayawahi marahisi wakati mwingine tunakumbana na vita na majaribu mengi kutoka kwa adui, na misukosuko mingi ili tu tuiache imani,..Hivyo kama shetani angekuwa anajua kuwa kama mtu ameupata wokovu ndio kaupata milele, basi asingekuwa na haja ya sisi kutufuatilia tuiache Imani baada ya hapo, maana kwake yeye ingekuwa ni kazi bure.,Lakini kinyume chake kila siku anatupiga vita kwasababu anajua kuwa uwezakano wa kukipoteza kile tulichonacho upo!…Anajua pia bado kuna uwezekano wa kuupoteza ulinzi huo wa milele.

Hivyo ikiwa kama tutadumu katika mapenzi ya Mungu basi uhakika wa wokovu huo ni lazima.. Lakini ikiwa hatutailinda neema tuliyopewa kwa bidii, tukawa wazembe, yaani tunaishi tu kama tunavyotaka, uwezekano mkubwa wa kuupoteza wokovu wetu upo.

Mtume Paulo alikuwa ni mtu aliyetokewa na Kristo, aliyejitoa kweli kwa Mungu, aliyehubiri injili kwa mataifa mengi, maelfu au pengine mamilioni ya watu waliokolewa kwa kupitia huduma yake..Lakini kuna wakati alisema..

1Wakorintho 9:26 “Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;

27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”.

Unaona, alishaona kumbe anaweza akawa sio tu mkristo peke yake, bali akawa hata mtumishi wa Mungu aliyeitwa, lakini mwisho wa siku akawa ni mtu wa kukataliwa (akaenda Jehanamu ya moto).

Hatari ya kutoishindania imani;

Paulo alisema vile kwa kumaanisha, sio kama kujionyesha kuwa ni yeye ni mnyenyekevu..Aliona uwezekano huo wa kupotea bado upo kwa asilimia kubwa!.

Wapo watumishi leo hii, ni wazinzi, wanadhani bado wanao ulinzi wa daima ndani yao..Wapo wachungaji ni wanywaji pombe na wavutaji sigara, wanadhani bado wanao ulinzi wa daima ndani yao..Kwamba hata wakifa watakwenda mbinguni kwasababu maandiko yanatuambia tunaokolewa kwa neema.

Nataka nikuambie, Hata Yuda, aliyechaguliwa na Kristo, mwenyewe,..Na alianza vizuri lakini hakuilinda neema aliyopewa na mwisho wa siku akaangukia katika mikono ya shetani. Sasa kama Yuda aliyetembea na Yesu miaka 3 na nusu alikengeuka…Mimi na wewe ni nani ambao hata hatujawahi kumwona Yesu tujidanganye kuwa tukishaokolewa tumeokolewa?.

Hivyo usipoithamini neema uliyopewa bure kwa damu ya Yesu Kristo, hujibidiishi kuilinda Imani yako, huko nyuma ulimaanisha kuokoka kweli, lakini leo hii, unakwenda Disko,.. unavaa nguo za uchi uchi, unatazama picha chafu mitandaoni, unasikiliza miziki ya kidunia, unakula rushwa, unakwenda kwa waganga..Nataka nikuambie kwako ulinzi huo wa daima (eternal security) ulishaondoka!!..Na hata ukifa leo hii utakwenda kuzimu na adhabu yako itakuwa kubwa Zaidi ya wale ambao hawakumjua Kristo, Haijalishi wewe ni kiongozi mzuri wa kanisani kiasi gani,..haijalishi umeshahubiri kiasi gani, haijalishi umewaleta wengi kwa Kristo kiasi gani…Usipoyafanya mapenzi ya Mungu, utapotea tu.

Ezekieli 3:20 “Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa;”

Na ndio maana biblia inasema:

2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Uthamini wokovu wako, ili Mungu apate nafasi ya kukulinda..

Ubarikiwe.

Mada Nyinginezo:

CHUJIO HILI NI LA AJABU SANA!

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

 

KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/13/ulinzi-wa-daima-eternal-security-je-ni-neno-la-kimaandiko/