Jaribu kufikiria mtu amepata ajali ya bodaboda, mguu wake umekatika anatokwa na damu nyingi pale chini na kwa bahati nzuri anatokea msamaria mwema ili kutaka kumsaidia, lakini Yule msamaria alipofika kabla kutaka kumsaidia au kufanya jambo lolote alimtazama kwa makini, ndipo alipogundua mahali tatizo lilipo na bila kupoteza muda alikwenda moja kwa moja kwenye uso wake na kutumbua kipele kidogo, kilichokuwa kimejaa usaha pembezoni mwa shavu lake, na kusema afadhali nimekusaidia maana kipele hicho kama usingempata mtu mtulivu kama mimi, usingekiona, sasa nakuona upo sawa ninaweza kuondoka, nitakuja kesho tena kukutazama hali yako unaendeleaje … Na mara Yule mtu kweli akapanda gari lake na kuondoka.
Je! Hapo Ni kweli mtu huyo atakuwa amemsaida Yule alayepatwa ajali pale chini?. Ni kweli kabisa ametoa msaada lakini sio kwa tatizo lililokuwa linatawala kwa wakati ule, msaada kama huo ungemfaa zaidi saa mtu yule akiwa na afya yake na nguvu zake, lakini sio kwa wakati ule ambao amepata ajali mbaya ya kukatika mguu. Hatutakosea kusema mtu huyo ni MNAFKI kwasababu aliliona tatizo kubwa zaidi ya lile lililokuwa nalo lakini badala yake aliliacha hilo na kwenda kushuhulika na mambo madogo yasiyokuwa ya umuhimu kwa wakati huo.
Mambo kama hayo hayo Bwana Yesu aliyaona ndani ya viongozi wa ki-dini waliokuwa wakati ule..
Mathayo 23:23 ‘Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, ADILI, na REHEMA, na IMANI; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. 24 VIONGOZI VIPOFU, WENYE KUCHUJA MBU NA KUMEZA NGAMIA’.
Mathayo 23:23 ‘Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, ADILI, na REHEMA, na IMANI; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.
24 VIONGOZI VIPOFU, WENYE KUCHUJA MBU NA KUMEZA NGAMIA’.
Unaona Watu hawa walifanikiwa kuigeuza sheria ya Mungu nyuma mbele,..yaani yale mambo ya msingi waliyafanya yasiwe na msingi, na yale yasiyo ya msingi yawe ndio ya msingi. Na huku wakitumia kisingizio cha kwamba Mungu ametoa maagizo hayo yafanyike, na hivyo yanapaswa yatekelezwe kwa nguvu zote na kwa bidii…sababu hiyo basi wakaitwa vipofu kwa upambanuzi wao…
Walikuwa wanawafundisha watu utoaji wa zaka,(fungu la 10),katika kila mapato mtu ayapatayo..lakini hawakuishia hapo tu walipata ufunuo wa ziada na kwenda mpaka kwenye mboga mboga na viungo,vyote…Lakini mambo yale ya muhimu ambayo Mungu anayahitaji kwanza kuyaona ndani ya mioyo ya watu mambo ya ADILI na IMANI yaliyokosekana ndani ya watu wengi wao walikuwa hawana muda nayo wala hawakutaka kujishughulisha nayo, kwao waliyapa nafasi ya mwisho.
Walikuwa wanasisitiza utoaji mpaka kufikia hatua ya kuwaruhusu watu wafanye biashara katika nyumba ya Mungu ili tu walete zaka za kutosha nyumbani kwa Mungu..Lakini dhuluma na ufisadi vilikuwa vimejaa ndani ya mioyo ya watu. Tabia hiyo iliwapofusha macho sana.
Wanamwona mtu anatenda mambo maovu, hawamsemeshi chochote lakini wakimwona mtu hajaleta fungu la kumi anafuatiliwa kwa umakini na kuwekwa vikao, na kukemewa, na kuambiwa unamwibia Mungu na hivyo Mungu atamlaani. Lakini kuhusu dhambi wazifanyazo kwa siri Mungu hawalaani.
Wanawaona watu hawana maarifa ya mambo ya Mungu katika masuala ya imani, hawafahamu chochote juu ya siri za ufalme wa mbinguni, badala wazingatie hayo kuwafundisha kuwa na kiasi na kuishi kama wapitaji tu katika dunia hii, ya kitambo, hilo kwao halina umuhimu sana walipenda mtu awe tajiri ili alete zaka hekaluni.
Ndio hapo Bwana Yesu anawaambia, “Viongozi vipofu, wenye KUCHUJA MBU NA KUMEZA NGAMIA.”..Jiulize Inawezekanikaje, kumwona ngamia kwenye kikombe cha chai, lakini mbu usimwone, au ngamia anawezaje kupita kwenye chujio halafu mbu akwame..HILI CHUJIO NI LA AJABU SANA!!….. Tunaweza kusema halipo duniani lakini kumbe lipo..
Linawezekana kabisa kutokea kwetu kama na sisi tutakuwa na tabia kama hizo..Ikiwa mafundisho yetu yatelenga kwenye Utoaji, yatalenga kwenye mafanikio ya kidunia miaka yote, yatalenga tu kubarikiwa na kuwa na mali…mwaka mzima tunajifunza na kufundishwa hivyo, lakini siku hata moja hatugusii umuhimu wa Toba, hatugusii umuhimu wa ubatizo sahihi kwa mwaminio, hatugusii juu ya mbingu mpya na nchi mpya zinazokuja, hatugusii juu ya UPENDO kwa Mungu na kwetu sisi sisi kwa sisi, kama ndio amri ya kwanza tuliyopewa na Mungu.
Mathayo 22: 35 ‘Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; 36 Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? 37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako’’.
Mathayo 22: 35 ‘Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu;
36 Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?
37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako’’.
Unaona Kama hatutakaa kuyagusia mambo hayo ambayo ndio ya msingi Mungu anayotaka kuyaona ndani ya watu, na badala yake tunazungumza tu habari za sadaka au zaka au michango, na u-partinership tuliopo miaka nenda rudi..basi tufahamu kuwa na sisi pia tutaitwa viongozi-vipofu..
Sio kwamba kutoa zaka ni dhambi hapana ndio maana Bwana Yesu alisema “imewapasa kuyafanya hayo” lakini msisahau na yale mengine, ambayo ndio mambo MAKUU YA SHERIA. Hivyo hivyo na wewe unayekwenda kusikiliza, au kuhubiriwa huku unafahamu kabisa uhusiano wangu na Mungu unadorora kila siku, na mahali ulipo unaona kabisa hapakutoshelezi kiroho..Unaendelea kudumu hilo eneo?..Kwa faida ya roho yako ni heri ukatafute mahali patakapo kujenga roho yako sasa..Hakuna dhambi yoyote kufanya hivyo. Kristo ndiye aliyekuita na sio kanisa.
Ni sawa na wewe leo unaumwa na njaa ya siku sita hujala chochote, halafu mtu anakuletea suti nzuri kama kitulizo cha njaa yako, hiyo suti itakufaa nini kwa wakati huo, itakufaa kwa wakati mwingine lakini sio huo,hata kama ukipendeza pasiwe na mtu mfano wako duniani, lakini kumbuka kesho unakwenda kufa… kinyume chake Utamthamini zaidi Yule atakayekuletea sahani ya chakula, hata kama atakuwa amekinunua kwa bei ya chini lakini kinakufaa kwa wakati huo..Kisha baadaye ndio umrudie Yule wa suti kama utakuwa na uhitaji nao.
Hivyo ikiwa mahali ulipo, hapaudumishi uhusiano wako na Mungu, ndugu nakushauri ondoka kwanza hapo katafute mahali chakula kilipo ukishashiba vizuri basi urudi kama kutakuwa na umuhimu..Mafundisho ya mafanikio ya kidunia ni mafundisho madogo sana katika mafundisho ya Ki-Mungu, ambayo hata yakipuuziwa yasifundishwe kabisa hayawezi kuleta madhara makubwa kama yakavyopuuziwa mafundisho ya KI-ROHO Yanayohusu toba, utakatifu na uzima wa roho yako na kumpenda Mungu. Mafanikio ni mazuri na jambo la ki-Mungu kujifunza kufanikiwa, lakini sio jambo la kwanza..Jambo la kwanza ni kuutafuta kwanza UFALME WAKE NA HAKI YAKE, Na hayo mengine ndio yafuate.
Hizi ni siku za mwisho. Je! Umeokolewa?, Je unauhakika umejazwa Roho Mtakatifu?, Kumbuka Neno la Mungu linasema.. “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.”(Warumi 8:9)…Hivyo kama upo mbali na wokovu tubu sasa ukabatizwe kwa Jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako na Kisha Mungu atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu, ambaye atakulinda, kukufundisha, kukuongoza na kukusaidia kushinda dhambi. Na Zaidi ya yote yeye ndiye Muhuri wa Mungu, ukimpata yeye, ni sawa na Barua iliyotiwa muhuri, Utakuwa umehakikiwa kwa viwango vya kimbinguni.
Ubarikiwe sana na Bwana wa Majeshi Yesu Kristo.
Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine. Na Mungu atakubariki.
Mawasiliano: +255789001312
Na pia kama utapenda masomo haya yawe yanakufikia kila siku kwa njia ya Whatsapp Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.
UAMINIFU NI KIGEZO KIKUBWA CHA KUTUMIWA NA MUNGU.
WAKINYAMAZA HAWA, MAWE YATAPIGA KELELE.
KWANINI TUWE WENYE BUSARA KAMA NYOKA?
UPENDO
AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.
Nini maana ya ugonjwa wa kufisha? (Yeremia 17:9)
Rudi Nyumbani
Print this post
ole wetu wafarisayo kwani hukumu kubwa tutaipata
Nimefurahi jamani. Natamani kukufahamu. Nakupenda Sana. Yesu wa Mbinguni akubariki kwa mafundisho mazuri
Amen utukufukwa Bwana..
Nawe pia uzidi kubarikiwa