TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

by Admin | 11 January 2020 08:46 am01

Filipo na Nathanaeli, walikuwa ni marafiki wa karibu sana, wote wawili maisha yao yalikuwa ni maisha ya kuifuata dini, wakichunguza habari za Masihi na kuja kwake, Walikuwa ni watu wa kusoma torati na maandiko yote yanayomuhusu Masihi, maisha yao kwa muda mrefu yalikuwa ya namna hiyo, pengine walikuwa wanakutana kila siku au kila wiki, kuzungumza habari za masihi na kuja kwake, kutakuwa kwa namna gani, pengine wanasema, akija ataiokoa Israeli kutoka kwenye mikono ya maadui zao kwa kipindi kifupi sana, au akija ataifanya dunia kuwa na amani, au akija ufalme wake utakuwa ni mkuu sana n.k…

Waliishi maisha ya kutamani kumwona Masihi akija katika kipindi chao, mpaka siku moja ndoto ya Filipo inapokuja kuwa kweli akiwa katika kuzunguka zunguka kwake anakutana na mtu mmoja aliyeitwa YESU, halafu mtu huyo akamwambia Nifuate!..Filipo kumwona tu na kuona mambo aliyokuwa anayafanya moyo wake ulimwambia huyu ndiye..

Ndipo kwa furaha, hata bila kumwaga aliyemwita, pengine akasema moyoni mwake habari hii ni lazima imfikie rafiki yangu wa karibu ambaye maisha yake yote naye yalikuwa kama ya kwangu kutazamia tumaini la Israeli, ndipo akaenda kumtafuta Nathanieli kwa bidii mjini, akizunguka mtaa kwa mtaa, jaribu kufikiria pengine alikuwa na marafiki zake wengi na ndugu wengi lakini aliwapita wote na kwenda kumtafuta mmoja tu, ambaye ni Nathanaeli..Rafiki yake ambaye alijua tu akizisikia habari hizo moyo wake utaruka ruka kwa furaha, mtu ambaye, amekuwa na moyo wa kutaka kujifunza, asiyeshikiliwa na mapokeo ya kidini, asiye na hila, aliyetayari kugeuka anapoujua ukweli,.

Japokuwa Filipo alijua Masihi kulingana na maandiko hatokei Nazareti bali Bethlehemu ya Uyahudi, lakini hakusita kwenda kumpelekea habari hizo rafiki yake Nathanaeli kwasababu alimjua naye pia ni mtu msikiaji sikuzote ni mtu asiyekuwa hila moyoni mwake. Ni mtu ambaye yupo tayari kujifunza jambo jipya na kama ni kweli atalifuata kwa moyo wote bila kusita-sita,..

Sasa wakati Nathanaeli akiwa sehemu Fulani chini ya mtini, ghafla Filipo anatokea na habari ya kwanza anayomueleza inahusiana na ile ile habari ya siku zote ya Masihi.. Nathanaeli akiwa anamsikiliza kwa makini sana na kwa shauku, akamuuliza yuko wapi?

> Yupo Nazareti..Filipo akajibu.

Yohana 1:43 “Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.

44 Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.

45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti”.

> Nathanieli akamuuliza..

Yohana 1:46 “…Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone”.

Je! Inawezekana Masihi akatokea Nazareti kweli? Maandiko si yanatuambia atatokea Bethlehemu?…Filipo akasema hatuna haja ya kuongea mengi, wewe ni mtu ambaye ukiona ukweli upo tayari kubadilika twenda ukajionee..? Kwakuwa Nathanaeli alijijua kuwa yeye ni mtu ambaye si kasuku-wa-kidini asiye na hila ndani yake, akaondoka na Filipo kwa moyo mmoja, kwenda kuyahakiki hayo anayoyasema, kuangalia yamkini ndoto zake zinaweza kutimia kwa hayo aliyoyasikia….

Na alipofika tu na kukutana Na Bwana YESU mwenyewe tunaona habari ya kwanza ilikuwa ni hii:

Yohana 1:47 “Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake”.

Ndipo Nathanaeli akashtuka akajiuliza huyu mtu amewezaji kunijua kuwa Ndani yangu hakuna Hila?..Na mimi sijawahi kumwona hata siku moja, wala yeye kusikia habari zangu, kwanza anapokaa na mimi ninapokaa ni mbali, amewezaji kujua asili yangu ya rohoni..

> Ndipo Nathanaeli akamuuliza tena:

Yohana 1:48 “…. Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona”.

Akashangaa tena, mahali ambapo Filipo alimpata kwa shida, Huyu Yesu ambaye alikuwa hanijui alikuwa ananiona pale, basi ataachaje kujua na mambo yangu mengine yote yaliyobakia.? Hakika huyu ndiye Masihi, Mwana wa Mungu, Mfalme wa Israeli..Sihitaji kujua zaidi ya hapo ndani yangu hamna hila,”

Moja kwa moja Nathanaeli, akaamini na kusema.

Yohana 1:49 “…Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli”.

> Ndipo Yesu akamwambia…

Yohana 1:50 “…., Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya”.

Mwisho wa maneno yale Bwana Yesu akawaambia mitume wake…

Yohana 1:51 “Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu”.

Unaona waliahidiwa kuyaona na makubwa zaidi ya yale waliyoyaona, lakini hiyo yote ni kwasababu waliamini katika vidogo, walikuwa tayari kumfuata Yesu kwa udhihirisho mdogo sana, hiyo ndio maana ya kutokuwa na HILA ndani yao..Na kwasababu hiyo waka ahidiwa kuonyeshwa na makubwa zaidi ya yale..kwamba siku zitakuja wataziona mbingu zimefunguka na maelfu kwa maelfu ya malaika wakishuka juu na kupanda juu yake ..Yaani kwa namna nyingine watafunuliwa utukufu wa Bwana Yesu kwa viwango vya juu sana..

Mtume Yohana, alifunuliwa sehemu ya utukufu huo, na ndio tunasoma katika kitabu chote cha ufunuo, Vivyo hivyo na mitume wengine walifunuliwa kwa sehemu zao ni kwa vile habari zao kila mmoja haziwezi kuandikwa kwenye biblia yote, lakini katika maisha yao yote ya huduma walikuwa wakiuna utukufu wa Yesu tofauti na hapo walipokuwa wanauona mwanzo.

Ukiachia mbali siku ile alipofufuka na siku ile walipomwona akichukuliwa na mawingu juu. Na siku ile alipokuwa akiomba mpaka malaika akatokea kumtia nguvu (Luka 22:43)

Ndugu YESU KRISTO, si kama wengi tunavyomfikiria leo hii, Mungu hajatufunuliwa makubwa yamuhusuyo kwasababu ya HILA iliyopo ndani yetu, tunaona ishara na miujiza na kazi zake nyingi anazozitenda lakini bado hatuwi tayari kumfuata kwa mioyo yetu yote kama vile mitume walivyofanya..tunategemea vipi ajifunue kwetu. Tukiambiwa tujikane nafsi tumfuate Bwana tunasema kufanya hivyo sio lazima…tukiambiwa twende tukabatizwe, ubatizo sahihi wa kimaandiko tunasema dhehebu letu halitufundishi hivyo? Hizo ndio hila zenyewe, tukiambiwa tusivae vimini na suruali na ma-hereni tunasema imeandikwa wapi kwenye biblia, hizo ndizo hila, ambazo zitatukwamisha tusimfuate YESU,..

Nathanaeli alifahamu kabisa kuwa Masihi ni lazima atokee Bethlehemu lakini aliposikia yupo Nazareti hakujifanya anajua, bali alikwenda kumsikiliza na baadaye ndipo alipojua kuwa ni kweli Bwana Yesu alizaliwa Bethelemu..Vivyo hivyo si kila jambo ulibishie tu kwa mara ya kwanza unapohubiriwa, Ondoa hila ndani yako na utii, mfuate kwanza Yesu na yeye mwenyewe kwa Roho wake mtakatifu atakafunulia kuwa hicho unachokifanya sasahivi ni sahihi au sio sahihi. Usiwe mtu mkaidi.

Yule ni Mfalme Mkuu sana, malaika wanamsujudia usiku na mchana huko mbinguni, ameketi sehemu ambayo kiumbe chochote hakiwezi kufikia, lakini pamoja na uweza wake, na nguvu zake nyingi namna hiyo, bado anatupenda na kujishughulisha na watu wanyonge kama sisi. Sasa kiburi cha nini mbele zake?

Kwanini leo hii usimkaribishe huyu Mfalme Mkuu ndani yako, ayageuze maisha yako?. Kama aliweza kufanya kwa Filipo na Nathanaeli, atafanya na kwako, kwasababu yeye ni Yule Yule jana na leo na hata milele..Unachopaswa kufanya ni kumfungulia mlango tu, na muujiza mkubwa utaanza kuona akiufanya katika maisha yako.

Kama upo tayari kufanya hivyo sasa. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI, NAYE NDIYE MFALME ATAKAYEKUJA. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo. Ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo kuanzia sasahivi, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Fanya kwanza hayo na YESU KRISTO ataanza kutembea na wewe katika maisha yako kwa namna ya ajabu sana.

Ubarikiwe.

Tafadhali share na wengine ujumbe huu.

Mada Nyinginezo:

MTUMAINIE YESU ASIYEISHA MATUKIO.

RABONI!

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

YESU MPONYAJI.

KIWANGO CHA TATU CHA IMANI.

TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

LITANIA YA BIKIRA MARIA JE! NI SALA YA KIMAANDIKO?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/11/tazama-mwisraeli-kweli-kweli-hamna-hila-ndani-yake/